HOFU NI SEHEMU YA UTASHI WA BINADAMU.. UOGA NI DHAMBI UKITAWALA.
Kwa kawaida mtu mwenye wasiwasi akionyesha wasiwasi wake ni vizuri kumpatia majibu ya kumwondoa katika wasiwasi huo ili kuepusha migongano inayo weza kuleta migogoro.
Nakumbushwa kuwa Mwanafalsafa wa kutoka Derbyshire, England Thomas Hobbes, alizaliwa 1558 na kufariki 1679 akiwa na umri wa miaka 91 alibainisha, kuwa migogoro mingi miongoni mwetu hutokana na ushindani wa kugombania kisichotosha.
Kwa vile sote tuna mahitaji yenye kufanana, basi Mwanafalsa huyu alisema kuwa migogoro hii itaendelea.
Mwanafalsafa huyu aliamini kuwa kutokana na hatari hii, basi jukumu muhimu na kubwa kwa Serikali yeyote ile iwe ni kulinda amani ya nchi.
Kwamba kwa kutofanya hivyo, jamii itarudi katika hali ya kutokuwa na taratibu.
Nitaendelea kuamini kuwa siku zote, pasipo haki na usawa hakuna amani,...
Ingawa katika jamii yeyote ile, uwepo wa amani na utulivu ni msingi mzuri katika kutafuta haki na usawa, kwa njia ya majadiliano.
Nilipata kusoma kisa cha mtego wa panya uliosababisha madhara hata kwa wasio panya.
Panya kwenye nyumba aliubaini mtego wa panya uliowekwa na mwenye nyumba uvunguni mwa
kitanda.
Panya yule akamwendea jogoo wa mwenye nyumba.
Akamwambia:
“Ewe jogoo, kuna mtego umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane namna ya kuutegua kabla haujatudhuru wote."
Jogoo akajibu
"Ondoka zako, mie mtego wa panya unanihusu nini wakati sina kawaida ya kufika uvunguni mwa kitanda?"
Panya yule akaenda hadi kwa mbuzi wa mwenye nyumba.
Akamwambia: "Ewe mbuzi mwema, unajua kuna mtego wa panya uvunguni mwa kitanda cha mwenye nyumba. Tusaidiane mawazo yakuutegua
kabla haujatudhuru sote."
Mbuzi akajibu
"Hivi tangu lini ukaniona nikiingia chumbani kwa mwenye nyumba? Mtego huo wa panya haunihusu mie mbuzi."
Panya akaenda hadi kwa ng'ombe wa mwenye nyumba.
Akamwambia:
"Ewe ng'ombe wa Bwana, kuna mtego wa panya umewekwa uvunguni mwa kitanda. Tusaidiane mawazo namna ya kuutegua kabla haujatuletea madhara."
Ng'ombe akajibu akionyesha mshangao;
"Sijapata kusikia jambo la ajabu kama hilo. Yaani, mie
ng'ombe nidhurike na mtego wa panya ulio uvunguni mwa kitanda! Hilo halinihusu."
Basi, ikatokea siku moja, nyoka akaingia chumbani kwa mwenye nyumba.
Katika kutambaa kwake uvunguni mwa kitanda, mkia wa nyoka ukanasa mtegoni.
Kishindo kilisikika.
Mwenye nyumba alikwenda kwa furaha akiamini hatimaye panya aliyekuwa akimsumbua sasa amenaswa.
Hapana, kumbe ni nyoka aliyenaswa mkia. Na ni nyoka mwenye hasira pia.
Akamng'ata mguu. Sumu kali akamwachia. Mwenye nyumba akapatwa na mauti muda mfupi tu uliofuata..
Jirani wakafika msibani. Siku ya kwanza watu walikuwa wachache.
Wakahitaji kitoweo.
Akakamatwa jogoo wa mwenye nyumba. Jogoo akachinjwa...
Siku ya pili watu wakaongezeka.
Kilihitajika kitoweo pia....
Akakamatwa mbuzi wa mwenye nyumba. Mbuzi akachinjwa...
Na siku ya maziko watu wakawa wengi zaidi. Akakamatwa ng'ombe wa mwenye nyumba. Naye akachinjwa!
Ni jogoo, mbuzi na ng'ombe wa mwenye nyumba walioamini kuwa madhara ya mtego ule wa panya yasingewahusu wao.
Walikosea sana...
Panya alikuwa sahihi,..
Na wala mtego haukumdhuru panya!
Kuna cha kujifunza kutoka kwenye kisa hiki....
Kama ukiruhusu akili yako ikawa kubwa na kuwa huru katika kufikiri..
Chukua yanayoendelea Zanzibar sasa kama mfano... Zanzibar ikichafuka, na hata Tanzania Bara itachafuka haitakuwa salama.. Tunapaswa kushirikiana katika kuutatua mgogoro wa Zanzibar, na siyo kunyosheana vidole.. sisi sote ni WATANZANIA..
Amani ya Zanzibar na Bara ikichafuka.. CCM, CDM, ACT, TLP, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD wote tutapata madhara na hata maafa.., sasa nashindwa kuelewa dhana ya kusema..
'Hatuwezi kuwapa Hizbu Zanzibar na hata kama wameshinda CUF katika uchaguzi'..
Kauli mbaya na haramu sana hii...
Tutafakari hili tukiyaangalia na ya kwetu tukiyatazama yanayoendelea kutokea nchini kwetu.. mfululizo, kwa kupangwa na watawala wenye hila, ubinafsi na uchu katika utawala..
Martin Maranja Masese,
Mwananchi wa kawaida,
martinchizzle@gmail.com
+255719715520
Comments
Post a Comment