Posho hii ifike hadi kwa walimu




NA RUSTON MSANGI.



Kila mfanyakazi anapoajiriwa huwa kuna utaratibu maalumu wa malipo, yaani mshahara kwa mwezi au vyovyote vile kutokana na mkataba wa kazi.

Mbali na malipo ya mshahara katika ajira, pia huwa kuna namna tofautitofauti ya kuwapatia fedha ya ziada wafanyakazi wa eneo au taasisi fulani ili kuongeza morali ya ufanyaji kazi, kupunguza makali ya maisha,  kufidia muda wa ziada katika kazi nk. Hii fedha hujulikana kama posho.

Posho hii inaweza kutolewa kwa mwezi, siku, saa nk.  Posho huweza kuwa kwa ajili ya chakula, usafiri, malazi,   utendaji au namna yoyote ili itakavyokuwa imepangwa na mwajiri kwa makubaliano maalumu.

Watumishi nchini Tanzania katika serikali na mashirika binafsi wanapokea posho kutokana na majukumu Yao.
Kwa mfano, madaktari na polisi.

Kwa upande wa walimu kwa muda mrefu imekuwa ni tofauti sana kuhusiana na suala la posho, japokuwa mwalimu mbali na jukumu kubwa na muhimu la kufundisha,  hufanya kazi nyingi nyingine akiwa kazini.

Kilichonisukuma kuitumia kalamu hii kuimulika posho kwa wafanyakazi hususani WALIMU, ni waraka wa serikali ulioeleza mabadikiko makubwa kuhusiana na posho kwa baadhi ya watumishi idara ya elimu.

Waraka huo wa serikali kupitia TAMISEMI wa mwezi Agosti 2016, unaeleza kuanza kulipwa kwa posho ya madaraka kwa viongozi wa elimu.

Waraka huo ni wa mwezi Agosti 2016 na unaelekeza kwamba posho hizo zimeanza kuingia mwezi Julai kwenye akaunti za baadhi ya shule kwenye kata husika zenye shule za msingi na sekondari.

Waraka huo unabainisha wazi nyadhifa za  viongozi wa elimu watakaopata hizo posho na viwango vya posho hizo,  kama ifuatavyo,-


Mosi, Wakuu wa shule, kwa maana ya shule za sekondari posho yao ya madaraka itakuwa laki mbili na elfu hamsini (250,000).


Mbili, Waratibu elimu kata ambao katika kata zao kuna shule za msingi za sekondari, posho yao ya madaraka itakuwa shilingi laki mbili na elfu hamsini (250,000).


Tatu, Walimu Wakuu wa shule za msingi posho yao ya madaraka itakuwa shilingi laki mbili ( 200,000)


Posho hii ya madaraka kwa viongozi wa elimu imekuja wakati ambapo kuna elimu bure, maana yake ni kwamba shuleni hakuna michango ya aina yoyote ile inayomhusisha mwanafunzi moja kwa moja, kwa maneno rahisi mashuleni hakauna chanzo cha pesa zaidi ya miradi midogomidogo ya shule ambayo hauwezi kuitegemea.

Hii ni tafsiri kwamba posho hii imekuja wakati muafaka kwa utendaji wa hao wahusika.


Pamoja na kwamba posho hii ni msaada mkubwa kwa viongozi elimu, yaani wakuu wa Shule,  walimu wakuu na waratibu elimu kata, LAKINI ikumbukwe kwamba viongozi hawa wa elimu hawafanyi kazi peke yao,

Bali kuna kundi kubwa la walimu nyuma yao ambao ndiyo watendaji na watekelezaji Wakuu wa mipango na mikakati ya elimu.

Sasa ni dhahiri kwamba kundi hili kubwa la watendaji Wakuu ambao ni walimu, ni muhimu sana kumulikwa kwa kuwa ndiyo kila kitu katika elimu ya taifa letu.


Kama hali itabaki hivi kwa kusahau hili kundi kubwa la walimu kwa posho ya aina yoyote ile, kuna hatari ya mambo kadhaa kutokea ambayo sio mazuri kwa maslahi mapana ya elimu ya taifa letu, kwa mfano,-

Mosi, itasababisha walimu wengi kuona huu ni muendelezo wa kusahaulika, kudharaulika na kutokutambiliwa kwa mchango wao na serikali. Hii itapelekea walimu kutokufanya kazi kwa hari ya kutosha na hata matokeo hayatakuwa ya kuridhisha.

Mbili,  ikiendelea hivi itasababisha mgawanyiko baina ya viongozi wa elimu na walimu, kwa kuwa viongozi wana posho na walimu hawana posho. Huu mgawanyiko hujenga makundi,  na makundi hukinzana, na mwisho hatutapata matokeo tunayoyatarajia.


Tatu,  Hii inasabisha serikali kuonekana haisemi ukweli, na inakandamiza haki za wengine, kwa kuwa kuna walimu wengi wakiwemo wapya na wazamani ambao wanadai malimbikizo, mishahara yao, pesa za likizo, madai mbalimbali mengine.

 Haya yote yamekuwa sugu kwa visingizio vingi ikiwemo uhakiki kwa sasa, lakini tunashuhudia migawanyo mipya ya hela kila kukicha.
Hii inadhihirisha na kuonesha jinsi ambavyo dhamira ya serikali kwa walimu ni ya kutiliwa mashaka makubwa sana.

Haya yote na mengine mengi yanaweza kuendelea kudhoofisha hari ya walimu katika kazi na kupoteza muelekeo wa elimu ya taifa letu, lakini vilevile yakifanyiwa kazi kwa nia na dhamira ya dhati inaweza kuinua hari ya walimu na kuleta matokeo chanya katika elimu yetu.

Hivyo ni muhimu kwa serikali kupitia wizara ya elimu na TAMISEMI kufanyia kazi ushauri ufuatao,-

Mosi, Kushirikiana na Wadau wa elimu ikiwemo walimu wenyewe ili kutambua ni kipaumbele gani muhimu cha walimu ili kifanyiwe kazi kwa namna itavyowezekana. Kwa nyakati tofauti walimu wameongelea sana posho ya katikati ya mwezi, posho ya makazi nk.

Lakini kwa kujadiliana na kutambua kipaumbele cha walimu inaweza kuleta matunda.
Na posho ya aina yoyote itakayopunguza ugumu wa maisha kwa walimu itakuwa msaada.

Mbili, serikali inapofanya mabadiliko yoyote katika sekta ya elimu hususani inapogusa maslahi ya walimu, ni muhimu kuzingatia na lile kundi kubwa kwa kuwa mchango wa walimu hauelezeki.

Tatu,  Serikali iepuke kuwagawa walimu ili kuwatawala (divide and rule) , kwa maana kwamba kama viongozi wanapewa posho na walimu wao hawapewi inawaweka viongozi wengi kwenye mtego na ugumu wa kudai haki za wengine.


Hiki kilio cha posho Mimi sio wa kwanza kukisema, na nina imani sitakuwa wa mwisho. Kila atakayeona umuhimu wa hili atapaza sauti na kulisemea bila kuchoka.

Viongozi wa elimu kupewa posho ni muhimu sana na ni hatua nzuri kwa sekta ya elimu, LAKINI kuwasahau walimu katika posho ya aina yoyote ile ni sawa na kumlipa kocha wa timu ya mpira vizuri sana wakati wachezaji wake wanataabika kwa njaa,  hapa unategemea matokeo gani uwanjani?

Ili kuleta ufanisi wa utendaji katika madaraka ya viongozi wa elimu, ni muhimu walimu wapate posho ili kazi zifanywe kwa hari baada ya kuwa maumivu na ugumu wa maisha umepungua kwa kiasi.

Kwa pamoja tuseme posho hizo zisiishie kwa Wakuu wa shule, Waratibu elimu kata na walimu wakuu, Bali zifike hadi kwa walimu.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA