HUU NI UHAKIKI AU UDHALILISHAJI?
NA RUSTON MSANGI.
Serikali ya awamu ya tano tangu iingie madarakani takribani mwaka mmoja uliopita, imekuwa ikiratibu na kutekeleza mengi nchini. Hivyo kuna mfululizo wa matukio mengi yaliyojitoleza.
Matukio hayo yapo mazuri, mabaya na zaidi yapo yakushangaza na kustaajabisha machoni na masikioni mwa watanzania.
Zoezi la uhakiki wa vyeti ni mojawapo ya mambo yaliyovaliwa njuga na serikali. Leo Naomba nizungumzie zoezi hili linaloendelea la kuhakiki vyeti vya watumishi walipo kazini. Nieleweke kuwa sipingi uhakiki wa vyeti nchini kwa namna mpya ambayo licha ya kushangaza wengi, lakini pia imewaacha wengi na maswali bila majibu.
Nikiri kutoka moyoni zoezi la uhakiki likifuata kanuni, sheria, taratibu, utaalamu na ushirikishwaji wa taasisi tofautitofauti, Ni zoezi zuri kwa maslahi ya taifa, LAKINI kinyume na hapo inakuwa fujo na udhalilishaji.
KAMA taifa nilitegemea tuwe na mfumo mmoja wa namna ya uhakiki, na pia sio dhambi kutofautiana kwa baadhi ya Halmashauri katika namna ya kufanikisha zoezi la uhakiki.
Leo hii katika muendelezezo huo wa uhakiki, limejitokeza jipya ikiwemo kwenye Halmashauri ya UKEREWE mkoani MWANZA kama mfano.
Katika kinachoitwa Tangazo la taarifa muhimu ya uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma, yanelezwa yafuatayo kwa ufupi,-
Mosi, mtumishi ataje majina ya walimu walimfundisha shule ya msingi
Mbili, mtumishi ataje walimu waliomfundisha sekondari na wanafunzi aliosoma nao.
Tatu, mtumishi ataje walimu walimfumdisha na wanafunzi aliosoma nao sekondari ya juu
Nne, mtumishi ataje walimu na wanafunzi katika Ngazi ya cheti, stashahada , shahada , nk.
Kichekesho zaidi ni pale unapoambiwa utaje na mahali walipo, haya ni masihara sasa.
Ukisoma vizuri Tangazo hilo, unaona hadi kutaja ulikosoma, mwaka na cheti ulichotunikiwa, Wakati haya yapo kwenye vyeti.
Tangu juzi nimepitia mitandao mbalimbali kuona na kusikia maoni ya watanzania wenzangu wanaopinga na kutofautina vikali na namna zoezi hili linavyoendeshwa, Nipende kuungana na wote wanaopinga namna hii ya uhakiki kwa mfano hili la UKEREWE.
Namna zoezi hili linavyoendeshwa linatoa tafsiri mbalimbali kwa jamii na taifa kwa ujumla kama ifuatavyo,-
Mosi, Inasababisha usumbufu mkubwa sana kwa watumishi na kuwafanya waanze kuhangaika kutafuta majina ya watu waliopotezana nao zaidi ya miaka kumi.
Mbili, Inadhihirisha ni kiasi gani katika mfumo wetu wa elimu na utaalamu ulivyo dhaifu hasa katika mambo ya msingi ya kitaaluma kwa watumishi wake.
Tatu, Hii inadhalilisha walimu na watumishi kwa ujumla, kwamba katika kinachoitwa uhakiki wa vyeti vya elimu taaluma, inakuwa ni utajaji wa majina. Watumishi walikwenda kusomea fani zao na sio majina, sasa unapohakiki watumishi kwa kigezo cha kutaja majina inakuwa udhalilishaji.
Nne, Inakatisha tamaa ya watumishi wengi wa serikali na wanaotarajia kufanya kazi serikalini kwa namna mambo yanavyoendeshwa kienyeji na kwa matakwa ya watu waliopewa dhamana ya kusimamia watumishi wa umma na maendeleo nchini.
Haya yote ni mapungufu makubwa sana katika zoezi la uhakiki namna linavyorndeshwa, hadi inafikia kulifananisha na udhalilishaji na unyanyasaji wa watumishi wa umma, kwa kuwa kila kukicha uhakika wa namna tofauti na Jana, na kesho tofauti na leo, KAMA taifa hatuwezi kusonga mbele kwa mtindo huu wa kuviziana na kuangalia wapi pa kupatia umaarufu.
Kwa mapungufu haya naishauri serikali kupitia Halmashauri ifanye yafuatayo,-
Mosi, vyombo vya serikali na taasisi zinazohusika zifanye uhakiki wa aina moja unaofanana kwa watumishi wote nchini, haiwezekani nchi moja lakini kila Halmashauri inakuja na namna mpya ya kufanya uhakiki, Sio dhambi kutofautiana lakini zoezi lolote la kitaifa na rasmi ili lifanyike kwa ufanisi ni muhimu kuwa na ulingano.
Mbili, Serikali ishirikiane na shule na taasisi zote za elimu nchini kufanikisha zoezi la uhakiki, hii itasaidia kwa kuwa katika mashule na taasisi za elimu ndiko ambako watumishi wote wametoka huko.
Tatu, Serikali inapoazisha zoezi lolote muhimu kama hili la uhakiki, Ni vyema vilevile kutoa habibu za rejea kwa watendaji wake hasa katika Halmashauri, kwa kuwa kusipokuwa na rejea yoyote ni rahisi sana kwa kila mtendaji kufanya kwa matakwa yake na washauri wake. Hili ni tatizo kubwa kwa taifa.
Nne, Serikali ishirikiane na watumishi wote wa umma katika mazoezi yote muhimu yenye maslahi kwa elimu na taifa letu kwa ujumla, kwa kuwa hawa ndio watekelezaji Wakuu kwa vitendo mipango yote ya serikali nchini, unapowatenga watumishi wa umma na kufanya mambo kwa kuwakomoa Haina afya kwa maendeleo ya taifa, Ni vyema washirikishwe wana mchango mkubwa Sana kwa Tanzania tuitakayo.
Ni dhahiri kwamba uhakiki ukifanyika kwa ufanisi, Ni hatua kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa tutakuwa na watumishi wenye sifa na pia kama taifa tutakuwa tumeokoa pesa nyingi zilizokuwa zinalipwa kwa watumishi wasiostahili.
LAKINI kitu kikubwa kinachotakiwa na wapenda maendeleo pamoja na watumishi wenyewe ni kufuatwa kwa sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika katika zoezi hili la uhakiki linaloendelea.
Hivyo dalili yoyote ile ya unyanyasaji na udhalilishaji katika zoezi hili la uhakiki na mengine yanayofanana na hili, unapaswa kupingwa kwa NGUVU zote na watanzania wote bila kuchoka.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment