Ufaulu hauji kwa kufanya kazi kama watumwa!
NA RUSTON MSANGI.
Shughuli yoyote ile ya kimaendeleo inapofanyika, hutegemewa kuwa na matokeo chanya.
Hadi kufikia matokeo yanayohitajika, njia za aina tofauti tofauti hutumiwa kufikia mafanikio.
Ubora au ubaya wa njia itakayotumika inategemeana kwa kiasi kikubwa na uongozi wa wa shughuli au eneo husika.
Vivyo hivyo katika mfumo mzima wa elimu nchini Tanzania, shuleni tunapopeleka vijana/wanafunzi wetu kupata maarifa tunatarajia wapate matokeo mazuri na kufaulu mitihani yao.
Ili ufaulu unaotarajiwa uweze kupatikana kwa wanafunzi wetu, wasimamizi wa elimu na viongozi wa Shule wanategemewa kuwa na mbinu, maarifa, weledi na ushirikiano wa kutosha kutoka kwa walimu ambao ndiyo watekelezaji wakuu wa sera na mipango ya elimu.
Hivyo kukiwa na mipango mizuri kwa ushirikiano, hata matokeo yatakuwa mazuri.
Kutokana na umuhimu wa elimu nchini, nalazimika kuzungumzia ufaulu, namna ya kufanikisha na vikwazo vilivyopo kwa wasimamizi hasa mashuleni kama ambavyo kila kukicha yanajitokeza mambo mapya.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, wengi tumejionea barua ikizunguka kutoka idara ya sekondari wilaya ya Mkinga, na hadi sasa haijakanushwa.
Ikiwa na kichwa cha habari ''mkataba wa kuboresha elimu na kufuta alama F kwa shule za sekondari Halmashauri ya wilaya ya Mkinga'' mkoani Tanga.
Barua hii imeelekezwa kwa walimu wa masomo husika, ikiwa ni mkataba wa makubaliano ya kufuta alama F na atakuwa tayari kuwajibishwa pale itakapopatikana alama chini ya D.
Ikitaja jina la mwalimu, somo na kidato.
Na mwisho inaonekana sahihi ya mwalimu wa somo.
Mbali na hilo, baada ya wadau wengi kusoma makala zangu za kuhusu walimu na elimu kwa ujumla, nimepokea maoni na malalamiko kutoka kila kona ya nchi hasa kwa walimu ikiwemo Kagera, Rukwa, Arusha, Kigoma nk.
Kwa mfano walimu wa halamshauri ya Maswa kwa baadhi ya shule wamekuwa wakifanyishwa kazi nje ya muda wa kazi tena kwa lazima, kupitia matangazo ya Wakuu wa shule yenye Mhuri na maelekezo ya kufundisha jioni kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi na mbili jioni bila posho au malipo yoyote ya ziada.
Haya yote pamoja na mengine mengi yanaweza kufananishwa na utumwa katika kazi, kwa kuwa mtumwa hana haki, hajaliwi, hasikilizwi, Bali atafanya tu vile ambavyo mkuu au bosi wake anataka kifanyike kwa muda wowote.
Katika ulimwengu wa sasa wa karne ya ishirini na moja, taasisi za elimu hasa shule za sekondari, njia za kufanikisha ufaulu zenye muonekano wa utumwa na kulazimisha mambo zinaweza kusababisha mambo yafuatayo,-
Mosi, kusababisha walimu kuwa na nidhamu ya woga katika kutekeleza majukumu yao ya kufundisha.
Hii hupelekea kufanya kazi ili kuridhisha tu mamlaka na sio ufanisi, na matokeo yoyote ya kazi inayofanyika kutokana na nidhamu ya woga huwa hasi, na ni ngumu kufikia malengo.
Mbili, huweza kusababisha migogoro na kutokuelewana baina ya walimu na wakuu wa Shule za sekondari au walimu wakuu wa Shule za msingi.
Kwa kuwa maamuzi mengi yanatokana na kulazimisha ili kuridhisha mamlaka husika bila kukaa na kushauriana kwa walimu wote.
Tatu, kujitokeza uvunjwaji au kwenda kinyume na mikataba ya ajira.
Hii huambatana na ukiukwaji wa haki za msingi za walimu, kwa mfano, kwa baadhi ya walimu kunyimwa ruhusa hata pale wanapofuata taratibu wakiwa na matatizo ya kifamilia na kijamii kwa ujumla, kisingizio kikiwa ni kufanya kazi.
Hii ni kwasababu njia zinazotumika kufanikisha mambo huwa ni matakwa ya viongozi na sio makubaliano ya walimu wote kwa kushauriana na kuona uhalisia wa jambo fulani.
Nne, hupelekea kutogundua kiundani matatizo na changamoto muhimu zinazojitokeza katika mchakato wa ufundishaji.
Hii ni kutokana na kwamba hakuna hali ya kuheshimiana katika mawazo na mapendekezo, hivyo wahusika wakuu ambao ni walimu mwisho wa siku wataona hakuna haja ya kuwasilisha mapendekezo yao, ambayo hayatasikilizwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa maslahi ya wanafunzi na elimu kwa ujumla.
Tano, husababisha kuwanyima wanafunzi haki yao msingi ya kupata elimu bora, na kuishia kupata bora elimu.
Kwa maeneo ambayo hakuna kushirikishana katika kufanya kazi ya ufundishaji, hata maarifa yanayotolewa huwa hayakidhi vigezo vinavyohitajika bali inakidhi matakwa ya kundi la watu fulani.
Hii sio afya kwa elimu ya vizazi vya leo, kesho na kesho kutwa.
Kufanikisha ufaulu kwa njia zenye uelekeo wa utumwa na kulazimisha mambo hata yasiyowezekana, huwa hazina matunda kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Hivyo ili kuweza kupiga hatua na kufanya kazi kwa ufanisi, nashauri yafuatayo kwa viongozi wa elimu hasa kupitia kwa wakuu wa shule,-
Mosi, wakuu wa shule kwa kushirikiana na walimu kuandaa kwa pamoja mipango ya muda mrefu na mfupi, hii itasaidia walimu kujua ni nini kifanyike, kwa wakati gani na kwa kutumia muda gani.
Waingereza wana msemo wao unasema, ''If you fail to plan, you plan to fail'' ikiwa na maana kwamba, ''ukishindwa kupanga, umepanga kushindwa'' (kwa tafsiri yangu)
Hivyo ili tufanikiwe katika masuala ya elimu, ni muhimu kuwa na mipango.
Mbili, kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango yote ambayo shule imepanga kuifanya.
Kwa kufanya hivi katika shule, itasaidia wakuu wa shule na walimu kwa ujumla kujua katika walivyovipanga ni kipi kimefanikiwa na ni kipi hakijafanikiwa na kwasababu gani.
Hapa itawawezesha walimu kujua wapi pa kufanyia marekebisho.
Tatu, wakuu wa shule na viongozi wa CWT (ambao hawaonekani kwenye matatizo ya walimu) kuyajua, kuyapokea na kuyafanyia kazi matatizo yanayowakabili walimu kwa ujumla, kwa mfano, madai ya mishahara, malimbikizo mbalimbali, manyanyaso na uanzishwaji wa posho maalumu kwa walimu inayodaiwa kila kukicha.
Haya yakifanyiwa kazi kwa dhati kabisa, hata utoaji wa maarifa kwa wanafunzi kutoka kwa walimu utafanyika kwa kiwango cha kuridhisha sana.
Tunapozungumzia elimu ya taifa lolote ulimwenguni ikiwemo nchini kwetu, ni lazima tumzungumzie mwalimu ambaye ndiye mwezeshaji mkuu wa kutoa maarifa kwa wanafunzi.
Mwalimu huyu ili afanye kazi kwa ufanisi, morali, na moyo wa dhati haihitaji kumfanya au kumtumikisha kama mtumwa.
Bali ufanisi utatokana na ushirikiano wa dhati kutoka kwa wakuu wa idara za elimu na kukubali kusikilizana na kushauriana kwa pamoja, hata pale mawazo yanapotofautiana.
Hivyo ni rai yangu kwa walimu na wadau wote wa elimu nchini, kupinga na kukataa namna yoyote ile ya ukandamizaji wenye muelekeo wa utumwa katika eneo la kazi kwa walimu.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment