Bodi ya mikopo kwa hili Hapana



NA RUSTON MSANGI.

Mataifa mengi ulimwenguni yaliyoendelea na yanayoendelea, serikali zina  utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi katika nchi zao kwenye masuala ya Elimu.

Utaratibu huu hupelekea kuundwa kwa vyombo na taasisi mbalimbali zinazoshughulikia mikopo hasa ya Elimu ya juu.

Vivyo hivyo nchini Tanzania tuna utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa, sifa kuu ikiwa ufaulu na fani husika.

Bodi ya mikopo nchini ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 9, ya mwaka 2004 na Bodi ilianza rasmi mwezi julai, 2005.

Moja ya Majukumu muhimu ya bodi ya mikopo yakiwa yafuatayo,-

Mosi, Kusimamia mchakato wa Uombaji mikopo/kuwapata wanufaika stahiki wenye kukidhi vigezo baina ya waombaji.

Mbili, utoaji wa mikopo.

Tatu, Kukusanya mikopo iliyokopeshwa tangu mwaka 1994.

Bodi ya mikopo pamoja na mapungufu makubwa iliyokuwa nayo na ambayo inayo,  imekuwa msaada mkubwa kwa familia masikini nchini. Wanufaika ni mashahidi wa hili.

Taarifa ya habari ya Septemba 14, iliyoripotiwa na kituo cha ITV kuhusu bodi ya mikopo imeshangaza wengi ikiwemo mimi.

Katika taarifa hiyo Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu imesema inatarajia kubadilisha Sheria inayoagiza mkopeshwaji kukatwa na mwajiri wake asilimia nane (8%) ya Mshahara kwa mwezi, na kufikia asilimia kumi na tano (15%) ya mshahara wa mnufaika wakati wa kurudisha mkopo huo.

Hii inamaanisha kwamba makato yataongezeka kwa Karibu mara mbili, yaani kwa mnufaika anayepokea 700,000 akikatwa 8% ya sasa ni shilingi 56,000.

Na ikibadilika kama bodi inavyopendekeza kukata 15% kwa mshahara wa 700, 000, mfanyakazi atakuwa anakatwa 105,000, hii ni kwa bodi tu ya mikopo kwa mfano wa mshahara huo, ila makato yatakuwa zaidi ya hapo kutegemeana na viwango vya mshahara vya wafanyakazi husika.

Huu mzigo wa bodi ya mikopo wanaotaka kutwika wafanyakzi ni mzito sana,  ikizingatiwa kuna makato mengine makubwa kama kodi, hifadhi ya jamii, vyama vya wafanyakazi,  bima ya afya nk.

Bodi ya mikopo inasema sababu kuu za madiliko haya ni ili kurahisishwa urejeshwaji wa mikopo na kusaidia wanufaika wengine kuweza kupata mikopo.

Sababu ni nzuri Sana lakini utekelezaji wake unakwenda kuumiza wafanyakazi wanufaika wa mikopo pamoja na wanafunzi,  Kwa mambo kadhaa yafuatayo yanaweza kujitokeza,-

Mosi, wafanyakazi wengi ambao ni wanufaika wa mikopo watakuwa na ongezeko la ugumu wa maisha kutokana na makato kupanda kwa mara mbili ya kile cha awali.

Mbili, inaweza kujenga uadui Kati ya upande wa wanufaika na upende wa bodi ya mikopo pamoja na Serikali,  Kwa kuwa badala ya bodi kuwa msaada itageuka kuwa mateso kwa wanufaika.

Tatu, wanufaika wengi wa mikopo wanaweza kukwepa kulipa na kuamua kufanya shughuli ambazo zitawaepusha kulipa marejesho hayo ya mikopo.

Haya ni machache yanayoweza kujitokeza, lakini inaweza ikawa zaidi ya hapo kutegemeana na wakati husika kwa wanufaika hawa ambao wengi huwa ni wa kutoka jamii zenye maisha ya kawaida sana.

Hivyo bodi ya mikopo na Serikali kwa ujumla naishauri ifanyie kazi mambo kadhaa yafuatayo,-

Mosi, serikali iangalie vyanzo vingine vipya na maalumu kwa ajili ya mikopo ya Elimu ya juu, kwa mfano tuna gesi asili,  madini,  mafuta, bahari,  mbuga za wanyama, na vingine vingi. Kwa kuwa elimu ni msingi wa taifa, basi rasilimali mojawapo inaweza kuwa maalumu kwa ajili ya mikopo tu na ikasaidia.

Mbili, bodi ya mikopo iache makato hayahaya ya asilimia 8% ya urejeshwaji kwa mshahara wa mwezi, waboreshe usimamizi wa urejeshwaji wa mikopo hiyo ili kuhakikisha inarudi kwa wakati na kunufaisha wengine.

Tatu,  serikali kwa kushirikiana na bodi ya mikopo, iitishe mkutano wa Wadau wa elimu nchini ikiwemo na taasisi zote za elimu na wawakilishi wa wanufaika na wanaotarajiwa kunufaika, Wakutane na kujadililana kwa kina kabla ya mabadiliko yoyote kutokea. Hii itasaidia sana kutoka na maamuzi mazuri yenye maslahi kwa wanafunzi, wafanyakazi na taifa kwa ujumla.

Bodi ya mikopo ya Elimu ya juu ni muhimu sana kwa uhai wa taifa letu kwenda kwenye teknolojia ya juu, kupitia mikopo inayowanufaisha wanafunzi kusoma fani mbalimbali.

Kwa mantiki hiyo, mabadiliko yoyote Yale hasi yana athari kubwa sana kwa taifa hili na maendeleo yake kwa ujumla.

Kwa kutumia kalamu hii ninawaomba na kuwasihi watanzania wazalendo, wanufaika wa mikopo na wabunge wote wenye nia njema kwa taifa hili, wapaze sauti zao bila kuchoka na kutoruhusu mabadiliko haya.  Ni hatari, yatanyonya wengi sana hasa familia masikini.

Kwa pamoja tuiambie bodi ya mikopo ya Elimu ya juu, hapana kwa hiyo 15%.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI