Adui mkubwa wa walimu ni CWT.
NA RUSTON MSANGI.
Adui ni kiumbe au mtu anayemtendea mwingine uovu, kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili sanifu.
Uovu unaweza kuwa wa moja kwa moja au hata kwa njia ya kutotimiza majukumu vizuri.
Chama cha walimu Tanzania CWT, ni miongoni mwa vyama vya wafanyakazi nchini, kinachoshughulika na walimu.
Kwa mujibu wa katiba ya CWT, pamoja na madhumuni mengi ya chama hiki, jukumu kubwa na la pekee ni kusimamia hadhi, haki na maslahi ya walimu kitaaluma, kiuchumi, kijamii nk.
Ni ukweli usiopingika kwamba ni vigumu kwa mwalimu mmojammoja kujitetea lakini kupitia umoja au taasisi ya CWT inakuwa rahisi zaidi.
Kauli mbiu ya CWT ni HAKI na WAJIBU. Kwa miaka mingi kinachoangaliwa ni WAJIBU huku HAKI ikiwa imezikwa na kuachiwa kila mmoja kujitetea.
CWT inaendeshwa kwa pesa za wanachama wake ambao ni walimu, kwa makato ya 2% ya mshahara kila mwisho wa mwezi. Hivyo kama ni rasilimali fedha ipo ya kutosha kufanya kazi kwa maslahi ya walimu. Nitakupa mfano kiduchu wa mapato ya CWT:
Nchini kuna Halmashauri zaidi 130. Tuchukue halmashauri 130 pekee.
Idadi ya walimu tuchukue makadirio ya 500 kwa kila halmashauri. Makato ya 2% kila mwalimu tuchukue 7,000 tu (minimum).
130 × 500 × 7,000 = 455,000,000 Tshs. (Milioni mia nne hamsini na tano) Hii ni kwa mwezi mmoja pekee.
Kwa mwaka mmoja, 455,000,000 × 12 = 5,460,000,000 Tshs. (Bilioni tano milioni mia nne sitini ) Hii ni kwa mwaka mmoja pekee.
Mbali na mapato haya kwenye mishahara ya wanachama (walimu), bado CWT ina vitega uchumi vingi vinavyoingiza mapato ndani ya chama, Kama vile jengo la mwalimu Dsm, benki ya mwalimu, majengo katika mikoa mbalimbali ambayo huingiza pesa kutokana na ukodishwaji.
Vilevile kuna misaada kutoka katika vyama rafiki na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi. Na bado katika kila mkoa hadi wilaya kuna magari kwa ajili ya utendaji kazi kwa manufaa ya walimu.
Hivyo kwa suala la rasilimali fedha ndani ya CWT si tatizo kabisa. Kuna vyama na taasisi mbalimbali nchini zinashindwa kutimiza majukumu yao vizuri kutokana na ukosefu wa fedha.
Kwa mfano chama cha walimu nchini Kenya kina nguvu, na hata pale serikali inapotishia kufukuza walimu, chama chao huwa tayari kuwalipa wanachama wake mishahara.
Lakini kwa CWT nchini ni kinyume kabisa, ina pesa za kutosha kuweza kufanya kazi ya utetezi wa walimu kwa kiwango chochote kile, labda nadhani tatizo la CWT haina watu wa kufanya hiyo kazi licha ya kuwa na rasilimali za kutosha.
Kutokana na hali hii ndani ya CWT tunapata tafsiri nyingi vichwani ikiwemo zifuatazo,-
Mosi, Inaonesha CWT iko kwa ajili ya maslahi yao binafsi na si kwa wanachama wao, yaani wanajilipa vizuri na kutumia magari na rasilimali nyingine kama watakavyo bila kuangalia lengo kuu.
Mbili, Inaonesha CWT ina viongozi dhaifu wasio na uwezo wa kuwasemea na kuwapigania wanachama wao katika kila jambo baya linaloathiri kazi yao na maisha kwa ujumla.
Tatu, Labda Viongozi wa CWT wanafurahishwa na matatizo yanayowapata walimu nchini, hivyo wanaona ni sawa tu na bora liende.
Nne, Inaonesha viongozi wa CWT wana woga wa kukemea maovu kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje. Na hata kufungua kesi kwa niaba ya wanachama wake imekuwa kitendawili. Hii ni dalili ya kuigopa serikali na watendaji wake huku walimu wakiendelea kuteswa na kunyanyaswa.
Tano, Ni dalili kwamba sasa rasmi CWT imepoteza malengo yake ya msingi ya uanzishwaji wake, hasa hasa katika kutetea maslahi, haki na hadhi ya walimu nchini. Kwa mantiki hiyo wanachama wa CWT wanapaswa kutafuta mbadala wa kudumu mbali na CWT, ni dhahiri kwamba chama hiki kimepoteza uhalali wa kuwakilisha walimu.
Kwa dalili hizi na mengine mengi, ni wazi kwamba CWT ni mojawapo ya adui mkubwa kwa walimu wa Tanzania.
Nyaraka nyingi kandamizi na ambazo ni kinyume na haki kwa walimu zinatoka kila siku, matamko mengi ya kinyanyasaji yanatolewa na watendaji mbalimbali kwa walimu, vitendo vya aibu vingi vinafanyika kwa walimu.
Lakini hatua zinazochukuliwa na CWT juu ya haya yote hayaendani wala hayana uzito na masaibu yanayowapata walimu.
Hakika CWT ni adui kwa walimu, inatendea walimu uovu kwa kutokutimiza majukumu yake sawasawa.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment