Serikali yawaweka walimu mtegoni.
NA RUSTON MSANGI.
Ualimu ni kada pekee nchini yenye watumishi wengi kuliko kada nyinginezo. Waswahili husema penye wengi kuna mengi pia.
Ni ukweli usiopinginga kwamba kila kada ina changamoto zake, lakini ualimu umekuwa na zaidi ya changamoto, ni matatizo.
Tumeshuhudia mara nyingi sana walimu nchini wakinyanyaswa kwa kupigwa, kunyimwa haki zao za msingi zilizipo kisheria, kufedheheshwa, na kudhalilishwa kwa kudekishwa na watendaji wa serikali. Mara kadhaa pia wazazi na wanafunzi wamekuwa watu wasiojali walimu.
Wakati haya yanafanyika kuna mwalimu mmoja aliwahi kutamka, nanukuu ''Hata nikipigwa ilimradi mshahara unaingia'' mwisho wa kunukuu. Kwa kauli hii inadhihirisha wazi hata walimu wenyewe hawathamini utu wao, na kazi wanazofanya wanaona ni hisani na huruma ya serikali na si haki zao.
Serikali inayokata kodi ya mwalimu 11% hadi 12% na bodi ya mkopo 15% katika mshahara kiduchu wala haimjali mwalimu.
Chama cha walimu CWT kinachokata 2% ya mshahara wa mwalimu kila mwezi, imekuwa butu kwa kipindi kirefu katika kushughulikia kero za wanachama wake (walimu). Wanajinufaisha viongozi pekee.
Lakini mwalimu husika anayebakishiwa mshahara kidogo baada ya makato mengi karibia nusu ya mshahara, naye hajithamini, hajijali na wala hatambui haki zake.
Kama ilivyo kawaida ya utendaji wa matamko, mnamo Januari 19 mwaka huu serikali kupitia kwa katibu mkuu OR TAMISEMI, ametoa agizo kwa wakurugenzi wote nchini kwamba wahamishe walimu wote wa masomo ya sanaa wa ziada wenye shahada na stashahada kutoka sekondari kwenda kufundisha shule za msingi. Na pindi ifikapo tarehe 15 Februari apate mrejesho wa zoezi hili. Siku kadhaa baadae waziri alitoa kauli bungeni kwamba zoezi hili litawahusu walimu waliowahi kufundisha shule za msingi na baadae kujiendeleza. Lakini haieleweki lipi ni lipi.
Hii ziada ya walimu wa sanaa ya kwenye makaratasi inayosema na serikali haina ukweli kiuhalisia katika mazingira ya kazi. Pamoja na haya kuna baadhi ya halmashauri walimu kadhaa wameanza kupokea barua za kubadilishiwa vituo vya kazi kutoka sekondari kwenda msingi. Mbali na zoezi hili kutokuwa na mantiki wahusika wameambiwa kabisa hawatapata malipo yoyote.
Wakati serikali inasema kuna upungufu wa walimu, serikali hiyohiyo ilisimamisha kuajiri walimu tangu mwaka 2015 kwa kisingizio cha uhakiki. Hivyo kama kweli shule za msingi zina upungufu serikali itatue tatizo kwa kuajiri watu wenye sifa na mahususi walisomea kufundisha shule za msingi.
Je suala hili limepokelewaje na walimu husika? Walimu wengi kama ilivyo kawaida wanaona kila kitu ni sawa bila kutafakari jambo kwa kina. Wanaona hakuna badiliko lolote kama tu mshahara utabaki palepale. Wanaona kila kitu ni sawa tu. Naomba niwakumbushe walimu mambo kadhaa yafuatayo ambayo yanapaswa kutafakariwa kwa kina na kwa weledi wa kutosha;-
Mosi, Kuna mkataba wa ajira ambao unabainisha wazi kwamba unaajiriwa kama mwalimu wa sekondari na si vinginevyo. Imekuwa kawaida kuvunja mikataba ya walimu kama ambavyo increments zilisimama tangu 2015 na baadae likaja ongezeko la danganya toto. Kisheria si sawa kuvunja mkataba wa mtumishi unavyotaka.
Mbili, Taaluma/utaalamu/fani/elimu, mwalimu wa sekondari ameandaliwa muda wake wote alipokuwa shule katika ngazi mbalimbali ili kufundisha kuanzia shule za sekondari na kuendelea. Hivyo si sahihi na haileti maana kumrudisha mwalimu huyu msingi badala ya kuajiri watu husika ambao wamejaa nje ya ajira na vyuo viko wazi wanaendelea kusoma.
Tatu, Jambo hili linaathiri kisaikolojia kwa kiasi kikubwa sana kwa mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Mwalimu leo anafundisha sekondari miaka kadhaa alafu leo unakuja kumpeleka shule ya msingi. This is a kind of demotion. Ni kumshusha mtu kwa kumdangaya mshahara utabaki palepale. Wengi matarajio yao ni kusonga mbele na sio kurudi nyuma.
Nne, Jambo hili litasababisha walimu kukosa stahiki zao mbalimbali. Kwa mfano, kuna marupurupu ya usimamizi wa mitihani ya sekondari na usahishaji ambao hufanywa na walimu husika wa sekondari kutoka maeneo mbalimbali. Unapompeleka mwalimu msingi anakuwa ameagana rasmi na posho hizo, na anakwenda kukutana na mitihani ya siku mbili na usahishaji wa kompyuta. Kumbuka kwa walimu wengi walioajiriwa mwaka 2015 ndo kwanza wanatimiza vigezo vya kusimamia na kusahihisha mitihani ya sekondari, alafu wengi wao lazima watakuwa kwenye orodha inayodaiwa ni ya ziada.
Tano, Jambo hili litasababisha usumbufu mkubwa sana katika kukusanya data na uhamishaji wa taarifa kwa wahusika. Kwa mfano tu kwa sasa kuna walimu wanaidai serikali mishahara yao ya miezi hata zaidi ya minne na malipo yanasumbua ikiwemo taarifa mbimbali. Hii itazidisha usumbufu maradufu.
Sita, Kama kweli zoezi litafanyika, litaleta shida kubwa kwa watakaobaki kwakuwa kazi zao zitakuwa ni mara 2 na zaidi ya kazi za awali. Hao walimu wanaoitwa wa ziada wapo wanaofundisha masomo mawilimawili na wengine darasa zaidi ya moja. Mbali na hapo shule kama taasisi sio ufundishaji tu, kuna majukumu mengine mengi.
Katika jambo hili serikali inahitaji kutumia busara ya hali ya juu sana. Ikiwemo kukaa chini kutafakari faida na hasara ya jambo hili, bila hivyo tutakuwa tunaichimbia elimu yetu kaburi.
Watu wa kuajiriwa wapo, hivyo waajiriwe wakafanye kazi ambayo waliandaliwa mahususi kwa ajili hiyo. Elimu haichezewi.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment