Thomas Isidore Nöel Sankara Taa ya Afrika iliyozimika ghafla!



Mnamo august 1983, vijana wawili, makapteni wa jeshi na wanamapinduzi, Thomas Sankara  na Blasius Compaore, waliipindua serikali ya Rais wa wakati huo katika nchi iliyokuwa ikijulikana kama Upper volta, rais huyu aliitwa Baptiste Ouedraogo...


Vijana hawa wakiwa katika fikra za Karl Max, wakiwa na ndoto nyingi za kuijenga Upper volta.., walibadili kabisa historia ya taifa hilo, walibadili jina la nchi na kuitwa Burkina faso, manake nchi ya watu, country of honorable citizen..


Uchapa kazi wa vijana hawa (Sankara na Compaore), Thomas sankara akiwa ndiye rais unaweza kufananishwa na ule wa Fider Castrol na Che Guavera, kabla haujachuja kule Cuba..


Haiyumkini Sankara alikuwa anatumia baiskeli kutembelea vijijini kuhimiza maendeleo, wakati pacha wake (Compaore) wakiwa kama pete na kidole..
Urafiki wa makapteni hawa wa jeshi la Burkinabe, ulikuwa mkubwa kiasi ambacho, wakati wanausalama walipomwambia Sankara kuwa Compaore ana mpango wa kumpindua na kumuua, yeye aliwajibu kuwa compaore asingeweza kufanya hivyo, labda mtu mwingine...


Blaise Compaore alikutana na Thomas Sankara mwaka 1976 katika mafunzo ya kijeshi Morocco na hapo walianza urafiki wao uliokuwa wazi kwa karibu watu wote waliokuwa wakiwafahamu nchini Burkina Fasso na nchi jirani.
Thomas Sankara alikuwa akiwaeleza wanausalama wake kuwa, hata kama Compaore angetaka kufanya hayo, hakuna wa kumzuia. 
Ni wazi kuwa Kapteni Thomas Isidore Sankara alikuwa karibu sana na Blaise Compaore, kwa kiasi ambacho Blaise Compaore alikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Sankara...


kama ilivyotabiriwa na watu wengi wa karibu wa Thomas Sankara, Blaise Compaore aliongoza mapinduzi yaliyosababisha kifo cha Sankara mnamo mwaka 1987, na yeye mwenyewe (Compaore), huku akishuhudia rafiki yake kipenzi Sankara akiuuwa, Akawa ndiye mrithi wa kiti cha Urais wa iliyokuwa Upper Volta baadaye Burkina Fasso..


Thomas Isidore Noël Sankara ni nani?? 
Isidore Noël Thomas Sankara alizaliwa tarehe 12.12.1949 Mjini YOKO katika nchi iliyokuwa ikiitwa Upper Volta (Volta ya juu) na kuuawa tarehe 15.10.1987 na wanajeshi wenzake wakiongozwa na rafiki yake Rais Blaise Compaore katika mapigano ya usaliti yaliyotokea Mjini Ouagadougou akiwa katika kikao cha utendaji wa kazi...


Thomas Sankara alipanda ngazi za kijeshi hadi cheo cha kaptenu pamoja na mwanajeshi Rafiki yake Blaise Compaore ANAYEJUA SIRI YA KIFO CHA CHA THOMAS SANKARA .


Kuna nyakati ambazo Blaise Compaore alipata kunena kwa kinywa chake katika shirika la kutetea haki za Binadamu duniani kwamba “kifo cha Thomasi Sankara kilikuwa ni ajali tu...


Mwaka 1981 Thomas Sankara alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kijeshi ya Rais wa wakati huo wa Burkinabe ya zanani (Upper Volta) Jean Baptiste Major. Dr. na baadaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Januari 1983 mpaka mwezi Mei alipokamatwa na kutiwa mbaroni na serikali ya Rais Major Jean Baptiste Dr kutokana na msimamo wake juu ya ukombozi kwa watu wote wa Volta ya Juu na kupendelea Marxist Revolution theories..


Thomas Isidore Noël Sankara alikuwa Rais wa Upper Volta  (Volta ya Juu) kuanzia mwezi Agosti 4 1983 hadi mwezi Octoba 15 1987 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Major Dr Jean Baptiste yakiongozwa na Blaise Compaore na kuwa Rais wa TANO wa VOLTA YA JUU au BURKINA FASO baada ya kubadilishwa jina na Sankara.


Thomas Sankara aliyejulikana kama Che – Guevara wa Afrika alianzisha Program mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika. Alibadilisha Upper Volta na kuwa Burkina Faso (land of Upright Men).


Alianzisha kampeni ya kuboresha Elimu na kutanua Huduma za Afya kwa watu wa Burkina Faso maeneo ya vijijini hasa kwa watoto walio athirika na magonjwa ya Uti wa mgongo , Homa ya manjano, na surua.. na watoto karibu milioni 3 walipata tiba hizo..


Pia alianzisha kampeni ya upandaji wa miti kitaifa, na takribani miti Milioni kumi ilipandwa nchi nzima..


Pia alianzisha kampeni ya usafi nchini kote, kila mwananchi alipaswa kufanya usafi eneo alipo.. na Sankara mwenyewe alikuwa anashika fagio na kuingia barabarani kufanya usafi.. Hiyo ni kampeni iliyoitwa mfagio wa mwananchi (le balai citoyen).


Aliongeza idadi ya wanawake katika serikali yake, ikiwa ni kampeni yake nchi nzima kupinga tohara kwa wanawake, pia alianzisha kampeni na baadae utaratibu wa kisheria wa kuwataka wasichana waliopata mimba wakiwa mashuleni kuendelea na masomo... pia akaajiri wanawake jeshini, akawapa ajira katika sekta za umma.. ili kupunguza unyanyasaji wa kijinsia na kuleta uwiano na usawa nchini Burkina Fasso.


Pia ndoa za wasichana wadogo na za kulazimishwa haswa za kimila katika maeneo mengi ya Burkina Fasso zikapigwa marufuku..
Thomas Sankara ambaye hakutaka makuu kabisa na wananchi wa Burkina Fasso. Akiwa kama Rais wa nchi, alivaa nguo zilizotengenezwa Burkina Faso badala ya suti kutoka Paris na London.. mara nyingi alionekana akiwa kwenye gwanda la jeshi..


Pia.. Thomas Sankara alifuta matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi na watumishi wote wa umma, yeye kama Rais alikuwa akitumia baiskeli au miguu kwenda kwa wananchi vijijini kuhimiza na kusimamia shughuli za kimaendeleo..


Alijikita sana kwenye kusimamia na kukuza sekta ya afya katika Burkinabe, alihimiza watu kujihusisha na kilimo.. akiwapelekea zana za kilimo na pembejeo bure kwa watu wa vijijini na kugawa ardhi kwa wananchi ili wajihusishe na kilimo..


Kwa muda mfupi sana akiwa kama Rais wa Burikna Fasso, aliweza kuifanya nchi hiyo kuagiza chakula kutoka nchi za nje na kuifanya nchi hiyo kuanza kuuza vyakula vyake nje.. akaanza kuifanya Burkina Fasso kuwa imara kiuchumi.


Sankara aliwahimiza watawala wa Afrika waache kuwaibia wananchi, waache kutegemea sadaka kutoka nje.


Sankara akawaambia madeni ya Afrika hayana uhalali kwa vile yalitokana na mikataba mibovu.


Ndio maana hakuna maendeleo yaliyotokana na mikopo ya kigeni. 
Sankara akataka Afrika iache kulipa madeni yasiyolipika. 
Mwalimu Nyerere naye wakati huo alisema mtu hawezi kulipa madeni wakati watoto wanakufa njaa.


Thomas Sankara alisema ukitaka kujua maana ya ubeberu angalia sahani yako ya chakula, utaona kila aina ya chakula unachokula kinatoka nje. Ndipo akahimiza Afrika ijitegemee kwa chakula, akisema: "Anayekulisha anakutawala"


Thomas Isidoré Nöel Sankara ni wazi aliwakasirisha sana mabeberu wa kimagharibi, hasa ubeberu wa Kifaransa uliokuwa ukitawala kupitia vibaraka wake wa Afrika kama Rais Felix Houphouet- Boigny wa Ivory Coast...


Chini ya uongozi wake (Thomas Sankara), Burkina Faso ililima chakula chake badala ya kuagiza kutoka nje...


Kwa hatua hiyo, Thomas Sankara akawa amewaudhi wakubwa wa dunia (mabeberu) kwa kukataa kwake mipango ya kurekebisha uchumi ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) huku hoja kubwa ya sankara ikiwa ni kwamba, mipango hiyo ni ya kinyonyaji.


Thomas Sankara aligawa ardhi kwa wakulima wadogo baada ya kuchukua kutoka kwa wawekezaji wa nje ambao walikuwa wameipora baada ya kupewa na uongozi uliopita..


Katika huduma za jamii alileta mabadiliko makubwa katika huduma za elimu, afya, maji na kuboresha miundombinu ya barabara kuunganisha sehemu mbalimbali za nchi hiyo.


Sankara katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinahudumia wanachi wa kawaida, Sankara alipambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, huku akimtaka kila mwananchi kujituma kulijenga taifa.


Thomas Sankara alikuwa mtu anayechukia rushwa na ufisadi, uvivu, uzembe, dhuluma na unyonyaji wa wananchi na rasilimali zao. Alitaka kuona watu wake wakifaidika kwa rasilimali za nchi yake.


Huyu ndiye Thomas Sankara ambaye alipunguza mshahara wake hadi dola 450 kwa mwezi, ambaye alitembea kwa baskeli katika mitaa ya Ouagadougu bila ya kulindwa.


Alipoulizwa kwanini hana walinzi alisema wananchi ndio walinzi wake, hivyo hahitaji kuambatana na wanajeshi wenye bunduki.


Washauri wake mara kwa mara walimshawishi aachane na matumizi ya baisikeli. Akaamua kutumia gari lenye bei ya chini (Renault 5) badala ya msururu wa mashangingi kama tuonavyo leo katika Afrika...


Hata hivyo alibaki na baiskeli yake mpaka alipokutwa na mauti, na akaunti yake ya benki ilikutwa na akiba ya dola 400 ambayo ni sawa na Tsh 850, 550/= (laki nane elfu hamsini na tano namia tano hamsini), kwa sasa, badala ya mabilioni mengi kama wanayoficha huko Uswisi watawala wetu leo...


Kumbuka, Thomas Sankara amedumu kwenye uongozi kwa kipindi cha miaka 4 pekee kabla ya mapinduzi yaliyoongozwa na Rafiki yake kipenzi... Blaise Compaore.. ambayo yaliondoka ba uhai wake, lakini kwa kipindi hiko cha miaka 4 akihudumu kama Rais, alitengeneza mageuzi makubwa sana..


Ndoto kubwa ya kila siku ya Thomas Sankara, ilikuwa ni kuifanya Burkinafasso kuwa moja kati ya mataifa makubwa Afrika kiuchumi..


Thomas Sankara alikataa hata picha yake (yeye kama Rais) kutundikwa katika majengo, na taasisi za serikali.. alisema hataki kutukuzwa..


Sankara alikuwa akipokea mshahara wa dola 450 kwa mwezi, mshahara mdogo kuliko viongozi wote barani Afrika kwa wakati huo..


Huyu ndiye Thomas Isidore Noël Sankara anayejulikana kama Ernesto Che Guevara wa bara la Afrika (alikuwa akivaa mavazi kama Che Guevara, mwenendo, matendo na malengo yake yalifanana na Ernesto Che Guevara, pia walikuwa marafiki wakubwa).., aliyeiongoza nchi kwa muda wa miaka minne kabla ya kuuliwa na maadui wa mapinduzi wakiongozwa na kapteni Blaise Compaoré Aliuliwa nyakati za usiku na mara moja akazikwa kwa haraka.


Ernesto Che Guevara naye alikuwa mwanamapinduzi wa Marekani Kusini aliyeuliwa na majasusi wa Marekani (CIA) na kisha kuzikwa kisirisiri.


Thomas Sankara aliyekuwa muumini wa fikra za kupigania Umoja wa Afrika au Pan Africanist mara nyingi alionekana kutopendwa na mataifa ya magharibi kutokana na fikra zake za kupinga dhuluma za wakoloni kunyonya watu wanyonge.


Mwaka 1985, Thomas Sankara alikaririwa akisema kuhusu falsafa yake kisiasa iliyokuwa maarufu, ilikuwa ikisema;

‘you cannot carry out fundamental change without a certain amount of madness’, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi, hauwezi kuleta mageuzi ya msingi bila kuwa na kiasi fulani cha ukichaa... ndiyo maana mabeberu walieneza propaganda kwamba Sankara ni kichaa anayeingoza Burkina Fasso..


Pamoja na yote na mengi mazuri.., wapinzani ndani na nje ya nchi ya Burkinafasso, walisikika wakimlaumu Sankara kwa kupiga marufuku vyama huru vya wafanyakazi na vyama vya siasa.


Pia Sankara alianzisha Mahakama za wananchi ‘people’s revoluntionary tribunals’ ambazo zililenga kutoa hukumu kwa wapinga mapinduzi, wafanyakazi wazembe... Jambo ambalo lilileta hamasa ya watumishi wa umma kufanya kazi kwa nguvu wakiogopa hukumu..


Ila hatua hiyo ilipigwa vita saba na wapinzani wake.. Kumbukumbu kubwa ya wananchi wa Burkinabe  (Burkina fasso), kuhusu Kapteni Thomas Sankara, ilikuwa ni wiki moja kabla ya kuuwawa kwake alitabiri, na alikaririwa akisema:

“Wanamapinduzi wanaweza kuuliwa, lakini fikra za kimapinduzi zitaendelea kuishi daima”


Hapo alikuwa akinukuu maneno ya Mwanamapinduzi maarufu Duniani, Ernesto Che Guevara ambaye aliwahi kusema..


“Revolutionaries and individuals can be murdered, but ideas never die.”


Thomas Sankara alifariki Oktoba 15 mwaka 1987 baada ya kupinduliwa na Blaise Compaore kuchukuwa utawala nchini Burkina Faso kwa muda wa miaka 27..


Inafahamika kwamba, kwa mara ya kwanza mwaka 1997, familia ya marehemu Thomas Isodoré Noël Sankara, ilifikisha ombi la kutaka mwili wa Sankara ufukuliwe ili ufanyiwe uchunguzi..


Taarifa zinafahamisha kuwa serikali ya Blaise Compaore ilitupilia mbali ombi kutoka familia ya Thomas Sankara la kutaka kufanyike uchunguzi kuhusu kifo cha Sankara.


Kwa mujibu ya ripoti ya kifo cha Thomas Sankara, serikali ilifahamaisha kuwa Thomas Sankara alifariki kifo cha kawaida.


Familia ilitaka kufahamu kama ni kweli katika kaburi hilo ndipo mwili wa Thomas Sankara ulipohifadhiwa..


Blaise Compaoré ni nani??

Compaoré alizaliwa katika mji wa Ziniaré, uliopo umbali wa kilomita 43 kutoka Jiji la Ouagadougou, ambao ndiyo mji mkuu wa Burkina Faso, alipitia mafunzo ya kijeshi akiwa amefikia cheo cha kapteni.


Ni mwanzilishi wa chama chake cha Congress for Democracy and Progress, akihusika katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1983 na yale ya mwaka 1987.


Miaka mitatu baada ya kufanya mapinduzi na kuingia Ikulu, alichaguliwa rasmi Rais wa Burkina Faso kwa kura mwaka 1991, katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani na kisha alichaguliwa tena kwa njia hiyo ya kura katika chaguzi za mwaka 1998, 2005 na 2010.


Alikuwa gwiji wa kushiriki mapinduzi ya kung’oa na kupachika watu madarakani na katika kuthibitisha hilo, akiwa na umri wa miaka 33, Blaise Compaoré aliratibu mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa madarakani Meja Jean-Baptiste Ouedraogo nchini Liberia, hiyo ilikuwa Agosti 4 mwaka 1983.


Wakati huo Burkina Faso ilikuwa ikiitwa Upper Volta.


Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliungwa mkono na Libya chini ya Muammar Gaddafi rafiki wa Compaore, kwa wakati huo, Libya ikiwa katika msuguano na Ufaransa kuhusu Chad.


Washirika wengine wa mapinduzi hayo ya Agosti 4, mwaka 1983 ni Kapteni Henri Zongo, Meja Jean-Baptiste Boukary Lingani na Kapteni Thomas Sankara— aliyetangazwa Rais kuwa katika mapinduzi hayo ya kijeshi.


Compaoré wakati huo alipofanya tena mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987, alizungumzia mauaji ya rafiki yake wa jeshini zamani (Rais Sankara) ambaye alimsaidia kuingia Ikulu (mwaka 1983) akisema ilikuwa ajali tu.


Hata hivyo licha ya kuongoza mapinduzi ambayo si tu yalimng’oa rafiki yake huyo madarakani bali hata kumuua, licha ya kukaa kwake Ikulu kwa miaka 27, Compaore hakuwahi kuchunguza sababu za mauaji hayo ya Sankara, jambo linalozua hisia kwamba alishiriki kuhakikisha Sankara anauawa ili mapinduzi yatimie bila
Katika utawala wa rafiki yake (Sankara), ulioanza mwaka 1983 hadi mwaka 1987, Compaoré aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, akiwa amepata kutumikia cheo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Naibu Waziri wa Sheria..


BLAISE Compaoré aliyeitawala Burkina Faso kwa muda wa miaka 27 alilazimishwa na wananchi kuikimbia nchi hiyo tarehe 31-10-2014.. Amekimbilia Ivory Coast (Cote d’Ivoire) ambako anahifadhiwa na rafiki yake Rais Alassane Ouattara...


Hii ni baada ya wananchi wenye hasira walipojitokeza kwa maelfu mitaani katika mji mkuu wa Ouagadougou.


Tatizo lilianza pale Blaise Compaoré alipotaka kubadili Katiba ili aendelee kutawala. Bunge lilikuwa tayari kutii amri yake. Ndipo wananchi wakalichoma moto jengo la Bunge na ofisi za serikali pamoja na makao makuu ya chama tawala cha CDP (Congress of Democracy and Progress).


Baadhi ya nyumba za wabunge waliokuwa mstari wa mbele katika kutetea Compaoré aongezewe muda nazo zilichomwa moto.
Mkuu wa majeshi ya ulinzi nchini Burkina Fasso Honoré Traore akajitangaza kuwa Rais mpya. Wananchi wakamkataa.


Baada ya muda Honoré Traore akapigwa kikumbo na Luteni Kanali Isaac Yacouba Zida akashika madaraka. Wananchi wakaendelea kudai serikali watakayoichagua wenyewe kidemokrasia, wakisema hawakumfurusha Blaise Compaoré ili jeshi lishike hatamu...


Wimbo mkubwa wa wananchi wa Burkinabe ni kwamba... Blaise Compaoré alimuua kipenzi chao.. na hivyo kusaliti mapinduzi ya haki ya awali yaliyoongozwa na Thomas Sankara dhidi ya serikali ya Jean Baptiste Ouedraogo.


Vyombo vya propaganda chini ya serikali ya Blaise Compaore wa kwamba Thomas sankara hakuwa muhimu sana katika uwepo wa taifa hilo,...


Hata mapinduzi ya wananchi wa Burkina Fasso dhidi ya Compare walihamasishwa na kumbukumbu za Kapteni Thomas Sankara. Ingawa watawala wanajaribu kufuta kumbukumbu zake lakini wananchi wa kawaida wangali wanamkumbuka.


Ni vizuri ikumbukwe kuwa hii ni mara ya tisa kwa majeshi kuvamia urais wa Burkina Faso tangu nchi hiyo kupata uhuru wa bendera kutoka Ufaransa mwaka 1960. Ni uhuru wa bendera kwa vile leo nchi hiyo inaendelea kukaliwa na majeshi ya Ufaransa, na utajiri unaporwa na wawekezaji.


Kwa sababu hata mapinduzi ya Blaise Compaore kumuondoa rafiki yake Thomas Sankara yaliongozwa na Compaore akisaidiwa na Ivory Coast, ufaransa na wakafanikiwa kumuua Sankara..


Wanamapinduzi na wana mageuzi wote Duniani, ni watu wanaojulikana kama wapinga ubeberu waziwazi na ndiyo maana wengi wao wamekumbana na ukatili wa mabeberu.


Wako wana mapinduzi na wana mageuzi waliouawa kama akina Thomas Sankara wa Burkina Fasso na Patrice Lumumba wa DR Congo na wengine kutumikia vifungo virefu na vya maisha maisha kama Nelson Mandela.


(Makala hii imeandikwa kwa msaada mkubwa wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa).



Martin Maranja Masese,
Mwananchi wa kawaida,
martinchizzle@gmail.com
+255719715520

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI