SEMA SASA BAAASIIIIII MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI (ALBINO)

KUKITHIRI KWA VITENDO HARAMU VYA MAUAJI YA ALBINO KWAITIKISA  TANZANIA.

Na Shindo Kilawa
Pichani ni baadhi ya matukio yaliyofanywa kwa wenzetu hawa wenye ulemavu wa ngozi


👉KEMEA ,PAZA SAUTI ,SEMA VIFO VYA MAALBINO SASA BAAASIIIIII KWA NGUVU👈
           Kumekuwa na mtikisiko mkubwa nchini Tanzania kwa vitendo haramu na vya kikatili  vinavyoendelea ndani ya jamiii zetu kwa hawa ndugu zetu Albino.Vitendo hivi  vinaendelea kuwatia hofu wananchi wenzetu na kujikuta kama wao ni wakimbizi ndani ya nchi yao ,pia wazazi wao hawana raha kila kuchwao .Hakika inasikitisha ,inahuzunisha,inasonosha,inagadhabisha pale unaposikia au kuona katika vyombo vya habari binadamu mwenzako kakatwa viungo au kauwawa na binadamu wenzetu ,wala sio fisi wala sio  simba mmmmmmmh.
Naomba tuangalie kwa kifupi maana halisi ya Albino.
       
           Albino ni nani?
Bila shaka kila mmoja wetu neno hili sio geni sikioni kwake na hata kama hujasikia basi uliona sehemu limeandikwa.

          Albino ni neno lililotokana na neno la kilatini "Albus" kwa lugha ya wazungu wanasema "White" likiwa na maana ya weupe ,hivyo basi Albino ni mtu mwenye ulemavu wa ngozi unaotokana na ukosefu wa melanin ambayo inaweza ikawa haijatengezwa kabisa au imetengezwa na kushindwa kusafirishwa hadi sehemu husika kwa ajili ya kuifanya rangi ya ngozi kuwa kama ilivyotakiwa. Watu hawa huathiriwa sana kwenye ngozi,nywele na macho
Tatizo hili ni la kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine hivyo basi wakikutana wazazi wawili wenyevinasaba hivyo vya ualbino basi wanaweza pata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi bila kujali wao sio walemavu.Kwa maneno hayo naweza nikawa mimi au wewe tukapata mtoto mwenye ulemavu wa ngozi endapo tu mm na ww katika uzao wetu walishazaliwa watu wenye ulemavu wa ngozi na vinasaba hivyo vya kulithisha uzao wetu tunavyo.
Nisingependa kujikita sana kuelezea kitaalamu zaidi,ningependa nijikite kwenye tatizo linalotusumbua nchini hapa.

          Kwanini mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi limeshamili sana?
kila mmoja anasema lake japo sina uhakika kama tafiti za kutosha zimefanyika juu ya tatizo hili kushamili ,tatizo hili limejitokeza mara kwa mara hasa kanda ya ziwa kuliko maeneo yote nchini Tanzania.
Watu wengi wanasema katika mitandao ya kijamii na vyombo  vya habari kwamba mauaji haya yanasababishwa na wanasiasa wanaotafuta madaraka kupitia kwa waganga wa jadi na pia inasemekana  kuwa wafanyabiashara wakubwa wanaamini ili wafanikiwe zaidi ni lazima watumie viungo vya maalbino kutokana na maelekezo ya waganga wao wa jadi.Sijui kwanini wanaaminishwa hivyo ,wengine wanaamini hata kufanya nao mapenzi tu wanakuwa matajiri na mambo mengi ambayo sitaweza kuyaandika yote hapa.
         Hizi zote ni imani potofu na hazikubariki kabisa na tuzipinge daima kwani zinapunguza nguvu kazi nchini.

           Nani mwenye jukumu la kuwaokoa watu wenye ulemavu wa ngozi?
Kwa ujumla jukumu hili ni letu sote ,nikiwa na maana ni jukumu langu mimi na wewe tunaoishi katika jamii yenye watu wenye ulemavu wa ngozi tunapaswa,kuwapenda kuwalinda na kuwathamini zaidi ya mboni za macho yetu.

           Lakini japo jukumu ni letu sote bado naendelea kujiuliza maswali kichwani kwangu.

Je serikali yetu sikivu ya CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) haijaguswa na tatizo hili na haioni tatizo hili linavyoshamili siku zote nchini kama imeona ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya ukatili  huu?
Wanaotekeleza unyama huu huwa wanakuwa wametumwa au ni wao wenyewe wanakwenda bila kutumwa na umoja huo wakikatili wanautoa wapi?
Ni kwanini Jeshi la polisi lisielekeze nguvu kubwa kuwalinda walemavu badala ya kuhangaika na wapinzani?
kwanini pesa zinazotumika kununua mabomu ya kuwalipulia wanaoandamana kudai haki zao zisingefanya kazi ya kutengeneza mazingira bora kwa walemavu?
Je serikali inampango gani kutokomeza unyama huu ?
Chama cha waganga wajadi pamoja na uwezo wao wakupiga ramli wameshindwa kufichuwa wenzao wanaowadanganya wananchi?
Je jamii inaelewa nini kuhusu tatizo hili?
Je kwani usalama wa taifa tulionao hawana mbinu za kitalaamu kuweza kubaini wanaopanga mipango hii ya kikatili na kuitekeleza bila tatizo?
Inamaana tumekosa wataalamu wanaoweza kupeleleza undani wa jambo hili au zipo intelelegensia za kuzuia maandamano tu?
Je ni wangapi wamekamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki toka tatizo hili kuaza nchini kwetu?
maswali ni mengi lakini sitaweza kuandika yote hapa nisikuchoshe udinichoshe tuone nini cha kufanya kulinusuru tatizo hili.
       
              Nini kifanyike sasa?
Ni dhahili kila mmoja mwenye upendo wa Agape na mwenye hofu na uwepo wa Mungu basi atakuwa tayari kupambana na kutokomeza mauaji haya.
          Mambo machache ninayofikiri nakudhani yanaweza saidia kutokomeza tatizo hili ni kama yafuatayo:-
       Kwanza kabisa serikali iweke sheria kali na inayotekelezeka ,katika sheria hiyo wasisahau adhabu ya kunyongwa hadharani wahusika watakaokamatwa katika upelelezi utakaofanyika na kukutwa na hatia kwamba ni kweli wao ndio waliohusika pasipo na shaka na shaka yoyote ile.
             Pili ,serikali iweke mikakati mizuri na endelevu ya kutambua idadi ya walemavu wa ngozi nchini .Kuanzia siku wanayozaliwa wafanyakazi katika hospitali au zahanati husika wakibaini hilo basi waweke kumbukumbu kuisaidia serikali, pia mahali  wanapoishi ijulikane.Watambulike wanaishi vipi na wawekewe ulizi maalumu ambao wenye nia ovu hawatatambua  uwepo wa ulizi huo mahali hapo.
                  Tatu,wananchi wapewe elimu yakutosha namna ya kupambana na wauaji hao na pia kutambua thamani ya maalbino hao katka jamii,Waelimishwe namna ya kuishi nao kwa upendo wa dhati bila utengano.
         Nne kwa kuwa nchi yetu ina wataalamu wa upelelezi basi wafanye upelelezi kwa mbinu madhubuti walizonazo ili kubaini wahusika bila kuingiza jambo hilo kisiasa kwani wanaweza kuwahusisha wapinzani wao kwa lengo la kuwachafua na kuwajenga wakuu wao tu.
          Mwisho niombe,wanazuoni,mashirika yasiyo ya serikali na viongozi wa dini zote washirikiane na wananchi kukemea unyama huo na waisaidie serikali katika kutimiza majukumu yao ya kuwalinda ndugu zetu maalbino.
Niwaombe tena tuwaunge mkono kwenye maandamano waliyopanga kuyafanya ilik kupaza sauti kwa Rais wa Jamhuri ya muungano Tanzania Mh. Pof.Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ,ni imani yangu atasikia kilio chao wala hapatatokea na wenye mioyo migumu kama Pharaoh katika maandamano yao.
Ninayo mengi ya kusema lakini kalamu yangu imeishiwa wino japo tamati sijafika.

MUNGU IBARIKI AFRIKA
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU WABARIKI WATU WAKE
MUNGU UWALINDE MAALBINO
AMENI.

Wako katika kutokomeza mauaji ya Albino
KILAWA SHINDO
0752115036

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI