WALIMU SASA WATUMBUE JIPU LAO

Hili ni moja ya bango lilokuwa limeshikwa na wafanyakazi siku ya May Mosi mwaka huu 


Na Ruston Msangi.

Vyama vya wafanyakazi ni taasisi kongwe.Kulingana na historia,vilianzia Ulaya wakati wa mapinduzi ya viwanda Karne ya 18 na 19.

Mapinduzi ya viwanda yalitengeneza tabaka la wafanyakazi  walinyonywa na kukandamizwa na mabepari-wamiliki wa viwanda.

Wafanyakazi wa viwandani,walilazimika kufanya kazi muda mrefu na katika mazingira magumu kwa malipo ya mshahara mdogo.Kulitokea vuguvugu la wafanyakazi la kudai haki.

Vuguvugu hili la waajiriwa wa viwandani ndilo ambalo baadaye lilizaa vyama vya wafanyakazi wenye mshikamano wa kitaifa na kimataifa.


Mshikamano wa wafanyakazi kimataifa ni chimbuko la  kuanzishwa kwa shirika la kazi duniani(ILO).Uwepo wa Vyama vya wafanyakazi unatambuliwa kwenye katiba  za mataifa mbalimbali duniani.

Nchini Tanzania, Ibara ya 20 (1) ya katiba ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania(JMT) ya mwaka 1977, inatoa haki ya wafanyakazi kuunda vyama vya kutetea maslahi yao.

Serikali ya Tanzani pamoja na kuwa inaelezwa kutojali maslahi ya wafanyakazi, imeridhia mikataba ya ILO namba 87 & 98.Katika mikataba hiyo kuna “uhuru wa kushirikiana na kulinda haki ya kuunda umoja”

Kwa hiyo, njia ni nyeupe kwa wafanyakazi wa kada zote kuungana na kutengeneza chama au umoja wa kupigania na kutetea maslahi yao.

Baadhi ya vyama vilivyoanzishwa nchini, ni Umoja wa wafanyakazi afya wa serikali(TUGHE),Muungano wa wafanyakazi wa serikali za mitaa(TALGWU),muungano wa wafanyakazi katika sekta viwanda na biashara(TUICO ) na Chama cha walimu Tanzania( CWT).

Walimu ambao wanaangukia CWT ndio kada inayoongoza nchini kwa kuwa na wafanyakazi wengi lakini viongozi wake akiwemo Gratian Mkoba wameshindwa kutetea maslahi yao.


CWT ilisajiliwa  mwaka 2007 na kupewa namba TU 004. kauli mbiu yake inayovutia sana inasomeka “WAJIBU na HAKI”.Walimu wamekuwa wakitimiza majukumu yao kikamilifu bila kupatiwa haki zao kikamilifu.

Serikali inayojitapa kila mara kuwa ni “sikivu” inatamani  sana kuona walimu wanatimiza wajibu lakini wanapodai haki zao inaelezwa kuziba masikio na  kufikiria kuweka zuio la mgomo mahakamani.

Walimu walipogoma mwaka 2008 na 2012,serikali ilitumia nguvu za vyombo vya dola kuwasambaratisha.

CWT inayotajwa kunufaisha tu viongozi,haina msaada wowote katika kujenga mshikamano wa walimu kutetea kutetea haki na maslahi yao.


Viongozi wa CWT wanaovuma kwa wazembe na uwajibikaji duni,wamefaulu vizuri kuratibu  makato ya ile fedha ya kuchangia chama inayokatwa kwenye mishahara ya walimu ili watumie  kugawana posho.


Ndani ya Katiba ya CWT yameainishwa  madhumuni kwa ajili ya kutetea na kulinda maslahi ya walimu.Viongozi wameshindwa  ama wameamua kupuuza  ili walimu waendelee kudhulumiwa na kunyonywa katika taifa lao.


Baadhi ya madhumuni ambayo viongozi wa CWT wameshindwa kuyasimamia ya kuyatekeleza kwasababu ya uzembe na uwajibikaji duni ni kama vile:

Mosi,kuendeleza na kulinda hadhi ya kazi ya walimu pamoja na kusimamia viwango vya juu vya maadili, ufahamu, maarifa na ujuzi.

Pili,kusimamia, kuendeleza na kulinda maslahi ya walimu kwa kuhakikisha kuwa kuna vivutio na mazingira Mazuri ya kazi.
Tatu,kuishauri serikali juu ya mambo yanayohusu elimu.

Nne,kusuluhisha migogoro na kutatua malalamiko mahali pa kazi baina ya walimu na mwajiri.

Tano,kuhakikisha walimu wanapata huduma zote zinazostahili kiuchumi, kiafya na kijamii.


Kushindwa kwa CWT kumeacha walimu kwenye majonzi, mateso na manung’uniko yasiyo na mwisho.Kushindwa kwa CWT kunaonekana katika maeneo yafuatayo:


Mosi,kutowaunganisha  walimu ngazi ya halmashauri.katika ngazi ya halmashauri CWT haina msaada katika kutoa maelekezo ya msingi kwa walimu wapya.

Mara nyingi walimu wapya wanapokelewa kwa semina zinazoratibiwa na benki na mifuko ya jamii.Viongozi wa CWT hawana haja na walimu bali wana haja na makato tu.


Pili, Kuruhusu serikali ilimbikize mishahara ya walimu.Wakati viongozi wa cwt wakijichimbia kwenye kwenye gorofa la ofisi za walimu ilala na kufaidika na posho za makato ya mishahara,wamenyamazia serikali ili iendelee kulimbikiza mishahara ya walimu kwa miezi na miezi.


Tatu,Makato na michango ya kupitiliza kiasi.Nusu ya mshahara  unaishia kwenye makato na michango.Yawezekana CWT inafurahia mshahara wa mwalimu kuwa na  makato na michango ya kila aina.


Kwa mfano, baadhi ya makato ni kama inavyoonekana kwenye mabano;Mfuko wa hifadhi ya jamii (35,800 sawa na asilimia 5%), bima ya afya (21,480 sawa na asilimia 3% ), CWT (14,320 sawa na asilimia 2%), Bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu -HESLB (57,280 sawa na asilimia 8 %).Jumla ya Makato tu ni tsh 215,460/=.

Mwalimu anayelipwa mshahara wa  tsh 750000/=  anabakiwa na tsh.534,540/= kwa ajili ya kuchangia michango iliyowekwa kwa shuruti na kugharimia maisha yake.

Kuna baadhi ya maeneo walimu wanachangia mwenge shilingi 1000/=,hiyo ni kwa mwalimu wa kawaida,  mwalimu mkuu au mkuu wa shule amechangishwa shilingi 10,000.

Walimu wamechangia michango ya maabara katika maeneo mengi kiasi cha tsh 20,000 kwa kila mwalimu.Kadharika maeneo mengine baadhi ya walimu wameshinikizwa kuchangia tsh 5,000/= kwa ajili ya madawati.

Nne,Kucheleweshewa malipo ya mishahara.Siku hizi ni kawaida kwa mwalimu mpya anayeanza  ajira kutolipwa  mishahara kwa miezi miwili, mitatu, minne na wengine hadi mitano huku wakidhulumiwa pesa za kujikimu.

Manyanyaso haya kwa walimu yanatukumbusha mwaka 2009 february ambapo mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Bwana Albert Mnali  alipoamuru walimu wacharazwe viboko kama wezi kariakoo, katika shule ya msingi Kanazi, Katerero, na Kasenene. Huu ulikuwa ni udhalilishaji wa kiwango cha Juu na kinyume na haki za binadamu, na kinyume na sheria za kazi Tanzania na duniani kwa ujumla.

Mwaka 2016 imekuwa funga kazi kwa walimu walewale wa shule ya msingi Baada ya ofisa elimu msingi Bwana Peter Fusi kumzaba mwalimu vibao darasani tena mbele ya wanafunzi wake darasani. Huu ni upuuzi, ni fedheha, ni udhalilishaji, ni uhuni na ujinga. Hautakiwi kunyamaziwa, unatakiwa kupingwa vikali na kila aliwahi kupita shule ya msingi na jamii nzima kwa ujumla. CWT wanasema wamemkabidhi mkuu wa wilaya ushahidi wa kimaandishi wa tukio kuzabwa mwalimu Kijana makofi,  je walimu wazee itakuwaje huko vituoni? ????? CWT hiyo hatua haitoshi kabisa ni lazima muende mbali mtoe msimamo thabiti na dunia ijue.

 Leo ni mwalimu wa msingi, kesho itakuwa sekondari na kesho kutwa itakwenda mbali kwa taaluma nyingine. 2009 ilikuwa viboko, 2016 makofi, tukinyamaza baada ya hapa utakuja unyanyasaji wa aina nyingine zaidi ya uliowahi kutokea.

Umefika wakati kwa walimu kuwa jasiri na kusimama imara na  kuujenga mshakamano na umoja mpya wenye lengo la kutumbua jipu lao la CWT.


+255 684 731516
rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI