JE SERIKALI INA NIA YA DHATI NA THABITI KATIKA KUBORESHA SEKTA YA AFYA AU NI KIINI MACHO KWA WATANZANIA?




Na Kilawa Kilawa

Wahenga walisema "Mtaka cha uvunguni sharti ainame"  nami sina budi kuyaishi maneno haya yaliyosemwa na wahenga kwani "penye nia pana njia"
Naomba niaze na neno BIG RESULTS NOW (BRN) ambalo natambua kwa ujumla wake sio neno geni sana miongoni mwetu ,tuliowengi au tulio wachache bila kujali ni wasomi au sio wasomi ,masikini au matajiri,weusi au weupe, wanawake au  wanume.
Naomba tuelewe  kwamba wanaoratibu mpango huu ,wametafsiri neno hili kwa lugha rahisi sana  kwamba BRN ni "MATOKEO MAKUBWA SASA".
Lakini nakosa majibu kabisa katika sekta hii ya afya wanaposema matokeo makubwa sasa ilihali hadi sasa sekta hii inadolola na haina unafuu kwa Mtanzania.

Neno hili BRN limekuwa likitumiwa sana na wanasiasa wengi hasa wa chama tawala pia hata wataalamu mbalimbali katika sekta mbalimbali nchini wamekuwa wakilitumia

Bila kupepesa macho yangu upande wowote naomba niende moja kwa moja kwenye mjadala, kwa ujumla wake sekta ya afya ni moja ya sekta muhimu katika ustawi wa taifa lolote na watu wake duniani kote na haipaswi kuletewa mzaha na mtu yeyote hata kama ni mkubwa kuliko wengine, kwani afya ndio msingi thabiti wa mtu yeyote bila kujali cheo chake, elimu au pesa zake na ndio maana tunasema sekta muhimu kama hii inahitaji sera thabiti zinazotekelezeka na zenye tija kwa ustawi wa jamii huska.

Katika taifa hili kumekuwa na mwendelezo wa mikakati ambayo hubadilishwa jina tu kila kukicha, ila picha ni  ile ile  ya siku zote mfano MKUKUTA 1&2","MPANGO WA MIAKA MITANO (5),MPANGO WA MIAKA 25 " na mipango mingine kedekede kama vile hii'BIG RESULTS NOW'' (BRN) hata kabla mipango mingine haijafanikiwa na  haijamalizika.

Ukiangalia kwa makini BRN katika sekta ya afya wameainisha kutekeleza mambo mengi sana ambayo sitayaweka yote bayana kwa sababu napenda nijikite zaidi kwenye swala nzima la rasilimali watu.
BRN inaainisha kuwa na  mpango wa kuwa na Zahanati Vijiji vyote nchini, kuwa vituo vya afya Kata zote nchin na Hospitali Wilaya zote na kuzipa hadhi ya Rufaa hospitali za Mikoa zinazokidhi vigezo.
Sambamba na hayo yote pia walilenga kuboresha huduma za afya kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ili yawe rafiki kwa wagonjwa na wafanyakazi wa maeneo husika.
Walilenga kuboresha mazingira kwa kuhakikisha vitendea kazi vinakuwepo vya kutosha (uwepo wa dawa ,damu salama,maabara safi na vifaa vyote kulingana na hadhi ya ngazi ya kituo husika) na kuhakiksha upatikanaji wa rasilimali watu kama vile madaktari,wauuguzi,watalaamu wa maabara n.k,ili zikidhi vigezo na viwango vya kimataifa kama shirika la afya duniani (WHO) linavyoyataka mataifa kufanya hivyo.

Katika hili sina budi kuwapongeza kwani sasa vyuo vingi vinazalisha madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa kada nyingine zote japo kitendawili kipo kikubwa na hakuna wakukitegua hadi sasa.
Kwa kuangalia mambo yote niliyoainisha hapo juu nitajikita zaidi Tanzania bara kwa sababu swala la afya si la Muungano, Tanzania bara ina mikoa 25,wilaya 133 ,vijiji 19200 na kata elfu tatu na ushee pamoja na mipango yote thabiti hadi sasa tuna Hospitali 21 tu za Mkoa,86 za Wilaya,Vituo vya afya 578 na Zahanati zisizozidi 6,000.
Jiulize mwananchi mwenzangu wa bara Je,'BRN' inawasaidia wananchi? au ipo kwa maslahi ya wachache?Je BRN imefanikiwa? Je huduma za afya tunazopata zinakidhi hitaji letu sisi tuliowanyonge? Achilia mbali wanaokwenda kutibiwa Kenya, India na nchi nyingine za ulaya.
 Majibu unayo mwenyewe mimi sina jibu la kukupa.

Naomba nikukumbushe  tena jambo jingine la msingi zaidi katika sekta ya afya ni kwamba SHIRIKA LA AFYA DUNIANI (WHO) wameweka vigezo katika kila jambo kukidhi matakwa ya wananchi wote ,shirika hili la afya duniani linataka Daktari mmoja ahudumie wagonjwa 1000 kwa mwaka,(yaani 1:1000),lakini imekuwa kinyume katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania ambapo Daktari mmoja anahudumia wagonjwa zaidi ya 20,000 hii ikiwa na maana ya kwamba hatujakidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani mara 20 zaidi.
Lakini pia juzi nilipokuwa nikipitia hotuba ya kambi rasmi ya upinzani niliona kuwa  uwiano wa daktari na wagonjwa ni 1:100,000 hakika ni idadi kubwa sana na ni mzigo mkubwa kwa wafumishi hawa,je ni lini tutakidhi vigezo vya kimataifa vya WHO?

Japo kuwa madaktari hawa wanafanya kazi kubwa hawalipwi posho za nyumba, hawalipwi posho za usafiri wala posho za mazingira magumu ya kazi.
Kwa mjibu wa mahesabu niliyofanya kwa kuangalia malipo anayolipwa daktari hayalingani na kazi nzito anazozifanya.

Bila kujali anatumia akili kubwa kutafakari ili kumtibu mgonjwa daktari huyu analipwa tsh 35,200/= kwa siku ambapo kwa masaa nane ya kazini inakuwa sawa na 4,400/= kwa saa ambayo machinga anaingiza kwa dakika moja tu akiuza bidhaa moja au mbili.

Lakini pia daktari anaweza kukaa mda waziada (On call)  kuazia saa 3:30 jioni na kumaliza asubuhi saa 7:30 kwa Tsh 20,000/= ambayo ni sawa na tsh 1,176/= kwa saa bila kujali ni kazi ngapi amezifanya kwa mda huo.
Pamoja na mateso hayo daktari huyu anayoyavumilia ila thamani yake inaonekana ni ya kawaida sana.

 Ni nani wa kuwaondolea maumivu haya ndugu zetu wanaookoa maisha yetu? Ikiwa wanaotumikia nafasi za juu wapo waliosomea udaktari na wanajua adha hii ila hawajawakumbuka hata kidogo.
Japo kwa mstari mmoja sina budi kumpongeza Dr David Mwakyusa kwa machache aliyoyafanya kwa maslahi ya taifa kipindi alipotumkia nafasi nafasi hiyo ndani ya wizara ya Afya

Pamoja na uwepo wa madaktari wachache ukilinganisha na hitaji la kimataifa bado kumekuwa na wimbi kubwa la uwepo wa madaktari mtaani wasio na ajira, lakini pia wapo manesi, watu wa maabara n.k
Sasa sijui ni ukata wa serikali? Au serikali imeona afya sio muhimu na kuona ni bora  kuwasha mwenge na kuukimbiza nchi nzima ni mhimu kuliko Afya za wananchi waliowachagua?

Ni aibu kubwa kwa taifa lenye raslimali za kila aina kushindwa kuendeleza sekta hii ya afya. Kumekuwa na kilio cha miaka mingi kuhusiana na upungufu wa rasmali watu katika sekta hii ya afya lakini jambo la kushangaza ni kwamba kuna madaktari zaidi ya 1025 waliomaliza masomo yao mwaka 2014, wakajiunga na mafunzo kwa vitendoa (internship) na kumaliza mwaka 2015 mwenzi wa nane, tisa, na wa  kumi wapo mtaani wanafanya shughuli nyingine ambazo hawajasomea ili hali kodi zetu walalahoi tunaokosa huduma zimewasomesha kwa zaidi ya miaka sita halafu serikali inabaki na BRN na kuendelea kulalamika kama yatima hii ni aibu kwa taifa linalojitosheleza kwa utajiri mkubwa wa madini, mito, mbuga za wanyama, milima na mabonde.
Swali linabaki Je, pesa iliyotengwa kwenye bajeti ya 2015/2016 zilifanya kazi gani?

Jambo lilonishangaza zaidi Mh waziri wa Afya Ummy mwalimu kupitia ukurasa wake wa twitter alikiri kuwa serikali haina uwezo wa kuajili madaktari 1000, alisema wataajili madaktari,4,00 tu hivyo zaidi ya 625 watakuwa mtaani tena ukijumlisha na wanaomaliza intern mwaka huu watafika zaidi ya 2,000.
Taifa linakwenda wapi?

Mimi kama mwanaharakati namshauri  Mh. Rais Dr. Pombe John Magufuli:-
Mosi, aelewe kwamba kuweka mipango mingi isiyotekelezeka ni kazi bure na haitakuwa na msaada wowote katika kuboresha afya za wananchi anaoongoza.
Pili,kwakuwa tumeona akitumbua majipu sekta mbalimbali basi atumbue na wizara hii ya Afya ili apate undani ni kwanini Madaktari hawa 1025 hawajaajiliwa hadi leo ili hali pesa zilitengwa?.
Tatu,awaboreshee watumishi hawa katika sekta ya Afya mazingira bora ya kufanyia kazi.
Nne, Kwa kuwa naibu waziri wa Afya alitangaza wazi kuwa ajira za hawa madaktari na wengine katika sekta ya afya zitatolewa mwenzi wa tano basi Mh Rais Mtukufu kama naibu wake hatatekeleza ahadi hii ya wazi amchukulie hatua kama alivyowachukulia wengine
Naliombea taifa langu Amani ya kutukuka.
Mungu ibariki Afrika na Tanzania yetu.

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI