Upungufu wa madaktari,serikali inahusika



NA RUSTON MSANGI

Watu husema “mtu ni afya.” Ina maana,afya ya mtu ikizorota kwa magonjwa au majeraha,shughuli au kazi zake za maendeleo hukwama.Nafsi mtu inaweza kupotea.Taifa linapoteza nguvu kazi.

Afya ya binadamu ni muhimu.Daktari ni mtaalamu wa afya anayeweza kutibu,kuimarisha,kurejesha afya ya binadamu.kupuuza daktari ni kupuuza afya ya binadamu.

Mahali kokote duniani,haiwezekani kujadili suala la afya ya binadamu bila kumtaja mtalaamu wa afya au daktari.

Madaktari au wataalamu wa afya,wana umuhimu mkubwa kwa  afya ya binadamu.Haiwezekani kumtenganisha daktari na afya ya binadamu.

Tanzania yenye idadi kubwa ya watu,ni miongoni mwa nchi zinaongoza kwa upungufu mkubwa  watalaamu wa afya kwenye  taasisi zake.

Kwa Tanzania,Upungufu huu, unachangiwa na serikali kuwapuuza madaktari.Hata wachache waliopo kazini, wanamekuwa wakilalamikia kupuuzwa na serikali.

Matokeo yake;maelfu ya watu wanaugua na kuteseka kwa kukosa  huduma bora.Baadhi,wamepoteza maisha wakiwa ndani ya  vyumba vya hospitali zenye upungufu wa madaktari.

Serikali inajua kuwa uhaba wa madaktari unasababisha kukosekana kwa huduma au kupata huduma mbovu.Aidha, unasababisha vifo ambavyo kwa namna moja au nyingine vingeweza kuepukika.

Tatizo hili ni kubwa zaidi maeneo ya vijijini ambako baadhi ya wanawake wajawazito, wanaelezwa kujifungulia au kufia barabarani kutokana na upungufu wa huduma.

Kulingana na  viwango vya  shirika la Afya Duniani (WHO),daktari moja anatakiwa kutibu wagonjwa 10,000  kwa mwaka(1:10,000).

Uhaba wa madaktari nchini Tanzania,unakiuka uwiano huu uliowekwa na WHO.Ukiukaji huu, unalazimisha madaktari wachache waliopo  kufanya kazi ambazo zingefanywa na madaktari wawili au watatu  kwa malipo ya mshahara uleule.

Kwa mujibu wa WHO,nchini,Tanzania,uwiano wa daktari kwa mgonjwa ni 1:26,000-daktari mmoja  anafanya kazi ya kuhudumia  wagonjwa 26,000 kwa mwaka peke yake.Uwiano huu,ni mara mbili na nusu ya ule uliowekwa na WHO.

Upungufu wa madaktari umekithiri zaidi katika mikoa ya Tabora,Kigoma na Mara na mikoa ya pembezoni.Inaelezwa,katika  baadhi ya mikoa hiyo,uwiano wa daktari kwa mgonjwa ni 1:50,000.

Tatizo la Upungufu  wa madaktari, linafugwa na  serikali ambayo inafanya makosa yafuatayo;

Mosi,kuchelewa kuwaajiri kwa wakati madaktari waliomaliza masomo yao na mafunzo kwa vitendo.

Kwa mfano, madaktari zaidi ya 1,000 walihitimu mwaka 2014 na kujiunga na  mafunzo kwa vitendo (intership) ya mwaka mmoja.Licha ya kumaliza mafunzo kwa vitendo mwaka 2015,bado serikali haijawaajiri mpaka leo.

Viongozi wa serikali ni wajuzi wa kuzungumza kuliko kutenda.Ahadi ya Naibu waziri wa afya,Hamis Kigwangalla februari 2016, kuwa wangeajiriwa mapema iwezekanavyo haijatekelezwa.

Tatizo la kutoajiri madaktari kwa wakati linaweza kuwa kubwa zaidi  kutokana Madaktari wengine zaidi ya 1000 walihitimu mwaka 2015 kutarajiwa kumaliza mafunzo kwa vitendo Agost mwaka huu.

Hali hii,inasababisha  madaktari wengi kuamua kwenda kufanya kazi kwenye mashirika au taasisi binafsi.Waliobahatika,wameajiriwa nchi za nje.

Pili, idadi ndogo ya wanafunzi wanaohiliwa kwenye vyuo katika fani ya udaktari.Kipindi cha nyuma hali hii ilichangiwa vikwazo viliwekwa katika kiwango cha ufaulu.Ilikuwa ni Lazima anayejiunga na masomo ya udaktari chuo kikuu awe na ufaulu wa daraja la kwanza.

Kwa sasa,idadi ndogo ya wanafunzi wanaodahiliwa kujiunga na fani ya udaktari inasababishwa na kutokuandaliwa mazingira mazuri na misingi imara kwa ajili ya wanafunzi wenye malengo ya  kuwa madaktari. matokeo yake, wengi wanakata tama na  kubadilisha fani.

Tatu,Mishahara isiyoendana na ugumu wa kazi.Daktari anayehudumia wagonjwa 26,000  badala ya 10,000 kwa mwaka,anafanya kazi za madaktari wawili wanaotakiwa kuajiri.Malipo ya mishahara yasiyoendana na uzito wa kazi yamesababisha madaktari wengi kumbilia na kuajiriwa nchi za nje.

Ili kukabiliana na upungufu huu wa madaktari wa kujitakia,lazima serikali ikubali kujifunza na kubadilika.

Kwanza, serikali inapaswa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kuajiri madaktari wanaomaliza mafunzo kwa vitendo mapema iwezekanavyo.

Pili,serikali iboreshe mazingira ya kazi,vitendea kazi,mishahara  makazi yao na vitendea kazi kwa ajili ya madaktari. Hii  inafaa ifanyike katika mikoa yote ili kuondoa dhana ya madaktari wengi kupenda kufanya kazi Dar Es Salaam, Arusha, Mwanza, Kilamanjaro na  Mbeya.


Tatu,kushirikiana na Wadau wa afya wa ndani na nje ya nchi,katika kuandaa misingi mizuri mapema kwa wanafunzi wenye nia na uwezo wa kusomea fani ya udaktari.

Bila afya njema kwa wananchi, taifa haliwezi kusonga mbele kimaendeleo.Kwa hiyo Daktari si wa kupuuzwa.

Kuwatumikia watanzania ni pamoja na kulinda, Kujali na kuimarisha afya zao. Hivyo,isiendekeze tatizo la upungufu wa madaktari bali iwajibike kulimaliza.

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu.Anapatikana mkoani Kilimanjaro.
Namba ya simu;+255 684 731516
barua pepe;rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI