Mwenge unavyoumiza walimu.

   

NA RUSTON MSANGI.


Mwenge ni kitu mfano wa kikombe chenye mpini mrefu na utambi ambacho huwashwa na kukimbizwa katika kusherekea au kutukuza jambo fulani. (Kamusi ya kiswahili sanifu, toleo la pili 2004).

Mwenge huweza kufananishwa na koroboi/kibatari lakini mwenge ni mkubwa kwa umbo.


Nchini Tanzania tuna mwenge wa uhuru ambao azimio la kuuwasha lilitangazwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1959.

Kwa mara ya kwanza ulipandishwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro usiku wa Desemba 9, 1961.
Hii ilikuwa ni siku ambayo Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa waingereza.

Mwenge huu ukiwa ni ishara ya uhuru, upendo, utu na matumaini.
Kila mwaka huwa kuna mbio za Mwenge, ambapo mwenge hutembezwa kila kona ya nchi, ukibeba ujumbe tofautitofauti wa kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Malengo na ujumbe wa Mwenge huwa mzuri, lakini shida ni katika utekelezaji wake na matumizi ya pesa.
Inaelezwa kwamba Mwenge hauna bajeti maalumu inayopangwa bungeni, lakini ni mojawapo ya tukio linalogharimu taifa kwa kufuja pesa za umma.

Vilevile miradi mingi inayofunguliwa kwenye mbio za mwenge inaonekana kuwa na thamani ndogo sana kuliko gharama za ukimbizwaji wa Mwenge.

Pamoja na mwenge kutumia pesa nyingi za umma, pia umekuwa ukiminya watumishi wa umma na wananchi wengine kwa kuuchangia, na mara nyingine ikiwa ni lazima.


Katika watumishi wanaominya, kunyanyaswa na kuonewa, WALIMU wamekuwa wahanga wakubwa katika masuala ya michango ya mwenge pamoja na kuhudhuria kwenye tukio.

Manyanyaso ya mwenge kwa walimu yanajidhihirisha katika baadhi ya Halmashauri nchini kama ifuatavyo,-

Mosi, Halmashauri ya wilaya ya Kahama kupitia kwa mkurugenzi katika barua ya Septemba 7, 2016 kwenda kwa Wakuu wa shule, ilielekeza kila Mwalimu ashone sare ya mwenge kwa kununua kitambaa kutoka kwenye ofisi ya ugavi ya wilaya. Vitambaa hivyo mbali na mashono, bei zake zilieoneshwa kuwa shilingi 30000, 15000 na 10,000.

Mbili, Halmashauri ya wilaya ya Mbozi kupitia barua ya afisa elimu sekondari ya Mei 18, 2016 ilielekeza kila mwalimu kuchangia mchango wa mbio za mwenge shilingi 3000.

Tatu, Halmashauri ya Mwanga kupitia barua iliyoelekezwa kwa wakuu wa shule,  ilionesha kuomba mchango kwa kila mwalimu shilingi 2000 na shilingi 10000 kwa kila mkuu wa shule.


Nne, Halmashauri ya wilaya ya Sengerema katika tangazo la mkurugenzi la Agosti  7, 2016, liliagiza watumishi wote ikiwemo walimu wote kufika kwenye mkesha wa mwenge bila kukosa.

Na tangazo likaenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba kutakuwa na kitabu cha mahudhurio saa 6 usiku, saa 3 usiku na saa 12 asubuhi. Haikuishia hapo, tangazo lilisisitiza kuwa watoro wote watachukuliwa hatua za kinidhamu.


Tano, Halmashauri ya jiji la Tanga kupitia barua ya mkurugenzi wa jiji ya Aprili 19, 2016 kwenda kwa Wakuu wa shule, ilielekeza walimu kuchangia mbio za mwenge kwa kutoa shilingi 1000 kila mmoja na walimu wakuu kuchangia shilingi 10000 kwa kila mmoja.


Maelekezo na matukio yote katika Halmashauri hizo na nyingine nyingi nchini, yanayohusisha mwenge kwa walimu, pamoja na kukiuka sheria husababisha yafuatayo kwa walimu,-

Mosi, huleta usumbufu mkubwa na usio wa lazima kwa walimu katika eneo la kazi na nje ya eneo la kazi. Hii hutokana na kutumika kwa nguvu katika kutekeleza shughuli hiyo ya mwenge.

Mbili, huweza kuleta migogoro katika familia za walimu kwa namna mbalimbali, kwa mfano walimu wa waliolewa wana majukumu mengi ndani ya familia ikiwemo kulea watoto, sasa kumlazimisha Mwalimu kama huyu kukesha kwenye mwenge sio sawa hata kidogo na haikubaliki.


Tatu, husababisha kutokuelewana baina ya walimu dhidi ya waajiri wao na Wakuu wa idara kwa kuwa hakuna ushirikishwaji, na matokeo yake waajiri hutumia ubabe kuminya haki za walimu. Imewahi kusemekana waliowahi kukataa mara nyingine hukatwa kwa lazima kwenye mishahara yao.

Nne, humbebesha mwalimu michango lukuki isiyo na sababu.
Hii ni kwasabau mbali na mchango wa mwenge, kumekuwa na michango mingine mingi kama vile ya maabara, madawati nk.


Kwa baadhi ya matokeo hayo hasi yanayotokana na michango ya mbio za mwenge isiyo na utaratibu kwa walimu, Nashauri mambo yafuatayo yafanyike ili kupunguza, kuondoa na kukomesha kabisa uonevu huu kwa walimu,-

Mosi, Waratibu wa mbio za mwenge ni muhimu kuwashirikisha walimu kwa kuwaomba huu mchango, na mwalimu atakayetoa iwe ni hiari yake na sio kwa shinikizo lolote wala kupangiwa kiwango kutoka kwa viongozi wa serikali na halmsahauri kwa ujumla.

Mbili, Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake ifikirie utaratibu mwingine wa kusherekea mbio za mwenge, kwa mfano mwenge unaweza kuwashwa kuweka sehemu moja maalumu na kusherekewa siku ya kusherekea uhuru na shughuli nyingine za kufungua miradi zikaendelea mikoani kote kwa kauli mbiu ya mwenge.

Hii itaondoa usumbufu kwa walimu na watumishi wengine, vilevile itapunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa pesa za umma.

Tatu, Chama cha walimu nchini C.W.T kitoke hadharani na kutoa tamko la kupinga unyanyasaji huu kwa walimu wake, mojawapo ya kazi ya chama cha walimu ni kutetea haki za walimu, sasa matukio kama haya yanapotokea na CWT iko kimya haingii akilini hata kidogo.

Ni sawa na hakuna viongozi kuanzia wilayani hadi taifa, kwa kuwa mbio za mwenge zinaratibiwa taifa na kushuka halmashauri.

Nne, Walimu wote nchini katika vituo vyao vya kazi ni muhimu kuhoji haya mambo kwa nia njema kabisa, sio kila agizo linaloletwa ni halali na haki, hivyo walimu wakiwa imara katika kujisimamia haki zao hata haya manyanyaso yatakoma kabisa.


Ishara ya kuwashwa na kukimbizwa kwa mwenge wa uhuru ni kuashiria uhuru wa nchi na watu wake, upendo, umoja, utu, matumaini na maendeleo kwa ujumla.

Kwa ishara hizi kila mtazania ikiwemo walimu wataunga mkono, lakini utaratibu unaotumika kuleta usumbufu kwa walimu na kufuja pesa za umma lazima ukosolewe kwa kila mwananchi mwenye nia njema kwa taifa hili pendwa.

Hivyo unyanyasaji, ukandamizaji na kuumizwa kwa walimu ni kinyume kabisa na malengo ya mwenge ulioasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa pamoja lazima tuseme hapana imetosha maumivu haya ya mwenge kwa walimu wote nchini.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI