Mwanafunzi Alivyochochea Hasira za walimu.
➡Siku ya walimu yaingia dosari.
NA RUSTON MSANGI.
Kulingana na maelezo ya Kamusi ya kiswahili sanifu, toleo la pili, 2004,dosari ni kasoro,walakini.Dosari ni hali ya kutokuwepi kwa ukamilifu wa kitu.
Octoba 5 ya kila mwaka ni siku ya walimu duniani. Katika siku hii maalum, Walimu wote ulimwenguni kwa kushirikiana na mashairika pamoja na Wadau wa elimu huadhimisha na kusherekea siku hii kwa namna mbalimbali.
Hufanyika matukio kama mikutano, vikao na shughuli nyingi ambapo walimu na Wadau hushiriki.
Mafanikio na changamoto Katika kada ya ualimu na mchango wake katika elimu ya taifa fulani hujadiliwa na kuchambuliwa.
Aidha,wakati wa siku hii,walimu na wadau wa elimu, hujikita katika mjadala wa namna ya kutatua kero mbalimbali ili kuleta ufanisi kwenye elimu na taalauma ya ualimu. Walimu hubadilishana uzoefu.
Nchini Tanzania, walimu wamekuwa mjadala.Mjadala juu ya walimu unatokana na tukio la kushambuliwa kikatili kwa mwanafunzi anayedaiwa kugoma na kupiga mwalimu wa mafunzo kwa vitendo. lililostaajabisha na kuiacha jamii na maswali mengi pasipo majibu.
Ilikuwa hivi:Usiku wa kuamkia Octoba 6 ilisambaa video katika mitandao ya kijamii ikionesha mwanafunzi akishambuliwa na watu kwa kipigo,awali washambuliaji walitajwa kuwa ni walimu wa shule ya kutwa ya Mbeya mkoani Mbeya.Haikuwa sahihi.
Baada ya tukio hili kufuatiliwa kwa makini, ilitolewa taarifa ilyodai kuwa aliyeonekana kupigwa ni mwanafunzi wa kidato cha 3 mkondo ''A'' kwa jina la Sebastian Chikungu, ambaye mnamo Septemba 28 inaelezwa aligoma kufanya zoezi somo la Kiingereza lililotolewa na mwalimu na aligoma hadharani kuadhibiwa na mwalimu aliyetaka kumwadhibu kutokana na kutofanya kazi.Aidha,inaelezwa mwanafunzi huyo,alikunja ngumi na kumshambulia mwalimu wake mdomoni.
Hatua hii, iliamsha hasira za walimu wanafunzi waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo katika shule hiyo ya kutwa ya Mbeya, ambao ni Frank Msigwa, John Deo, Sante Gwamaka na Evans Sanga .Walimshambulia mwanafunzu kwa zamu.
Hawa wote kwa pamoja walionekana katika video wakimpiga mwanafunzi mithili ya mwizi.
Kinachohojiwa na kulaaniwa na watu wengi ni kipigo cha kikatili alichopewa mwanafunzi anayeelezwa kugoma kufanya kazi.Watu wanahainga na matokeo kuliko chanzo.
Inadaiwa mwanafunzi alipewa zoezi katika somo la kiingereza na hakufanya.
Mwalimu mhusika ambaye ni Frank Msigwa alipohoji na kumpiga kibao, mwanafunzi alionesha dharau na kushikana na mwalimu huyo kimapambano kwa kukabana.
Ndipo kwa kushirikiana na walimu wengine walimchukua mwanafunzi hadi ofisini na tukio lililofuata ni kama linavyoonekana kwenye video, iliyorekodiwa na mwalimu mwanafunzi mwenzao ambaye ndiyo chanzo cha kusambaa kwa video hii kwenye mitandao ya kijamii.
Kufuatia tukio hili tumesikia watu wengi na viongozi mbalimbali nchini wakilisemea kwa nguvu zote na kulifanya lisambae sana.
Waliokwisha zungumzia suala hili ni Mwigulu Nchemba Mb, waziri wa mambo ya ndani, Amos Makala mkuu wa mkoa wa Mbeya, George Simbachawene waziri OR TAMISEMI, na waziri mwenye dhamana ya elimu Profesa Joyce Ndalichako.
Hivyo waziri wa elimu siku ya Octoba 6, 2016 ametangaza kuwafukuza chuo wanafunzi hao wa chuo waliohusika katika tukio hili la kumpiga mwanafunzi. (Japo siyaoni mamlaka ya waziri kufukuza wanafunzi chuo, kwa kuwa kuna taratibu zake na vyuo husika vina mamlaka kamili)
Taarifa nilizo nazo ni kuwa ni mwanafunzi mmoja tu katika shule mzima ya Mbeya Day aliyepigwa kipigo cha mtu mwizi.Ina maana huyu waliopiga walilazimishwa na tabia ya mwanafunzi.
Mimi binafsi kwa upande wangu kama mdau wa walimu na elimu nchini, ninaungana na mamilioni ya watanzania na dunia kwa ujumla kupinga vikali tukio hili la kikatili na kinyama kwa watekelezaji wote, ikiwa ni pamoja na aliyerikodi na kusambaza.
Mbali ya kuwa tukio la kikatili, pia linasababisha yafuatayo, -
Mosi, tukio hili limefedhehesha walimu wote nchini, japo limefanywa na walimu wanafunzi lakini limetokea katika mazingira ya shule ambalo ni eneo la kazi la walimu.
Mbili, huweza kuleta mgogoro mkubwa baina ya walimu dhidi ya wazazi, wanafunzi, serikali na jamii kwa ujumla kwa kuwa linaleta tasfsiri kwamba eneo la shule sio salama.
Tatu, huweza kuwafanya wanafunzi kuwa na jeuri na wenye nayo kuizidisha maradufu.
Kwa kuwa baada ya tukio hili baadhi ya wanafunzi wanaweza kuamini hata usipofanya kazi ya darasani ni ngumu kupata adhabu, au kumtengenezea mwalimu makusudi ili apate kipigo akiamini msaada upo.
Nne, huweza kurudisha nyuma maendeleo ya elimu pale ambapo baadhi ya walimu wataona haina maana ya kutoa adhabu hata kama ni ile inayofuata taratibu, kanuni na sheria. Hii ni kwasabau ikitokea bahati mbaya mwanafunzi akaumia ni ngumu kuangalia chanzo, na matokeo tu ndiyo huangaliwa.
Pamoja na kutokukubaliana na tukio hili la kinyama na kikatili kuwahi kutokea nchini tena lililitokea sambamba na siku ya walimu duniani, pia ni muhimu kwenda mbali zaidi kwa kuangalia mazingira na vyanzo vinavyoweza kupelekea matukio ya aina hii kutokea ili yakomeshwe.
Vilevile nashauri mambo kadhaa yafuatayo yafanyiwe kazi ili kurudisha hali ya ushwari kwa walimu na jamii kwa ujumla,-
Mosi, chama cha walimu nchini CWT, kitoke hadharani na kisemee tukio hili watanzania wasikie, pamoja na kulipinga pia CWT iweke wazi kwa watanzania kwamba waliofanya tukio hili sio walimu ila ni wanafunzi- walimu waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo kutoka vyuoni.
Pili, Walimu wote nchini wawe makini na utoaji wa adhabu kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa na mamlaka husika.
Kuna namna ambayo inaweza kuepusha haya kwa kutoa adhabu nyingine au ya kiboko yenye kufauata kanuni, na ikumbukwe kuwa hasira hasara, na tukio likimpata mwalimu anaachwa kama mkiwa.
Tatu, serikali kupitia vyombo vyake na watendaji mbalimbali, watumie nguvu ya aina hii hii au zaidi kwa matukio mengine ya udhalilishaji na ukatili yanayowakuta walimu kutoka kwa viongozi, wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Nne, wanafunzi na wazazi wote nchini waelewe kwamba mwalimu sio adui wa wanafunzi na hata siku moja hatakuwa adui, ni mzazi na mlezi. Hivyo ni vyema kujiepusha na uchonganishi wa aina yoyote ule.
Tano, taasisi za elimu ya juu zote nchini ambazo zinatoa mafunzo ya taaluma ya ualimu, ni muhimu kuwapa semina maalumu wanafunzi wao kabla ya kuondoka kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo ili wajue ni nini cha kufanya kwa namna gani na nini sio cha kufanya.
Hii itasiadia kupunguza na kuondoa kabisa matukio ya aina hii au yafananayo na haya.
Haya machache kwa namna moja au nyingine yatasaidia kuondoa na kufuta kabisa matukio ya kinyama kwa wanafunzi, Walimu na jamii kwa ujumla.
Tunaamini binadamu wote ni sawa mbele ya sheria, bila kujali dini, cheo, uwezo wa fedha, kabila au elimu. Hivyo msumeno ukate pande zote pindi tukio la kikatili na kinyama linapompata yeyoye yule.
Kwa dosari hii katika wiki ya kuadhimisha siku ya walimu duniani, naamini ni funzo kwa walimu- wanafunzi na jamii kwa ujumla. Na haiondoi umuhimu wa walimu nchini na duniani kwa ujumla.
Kwa pamoja tupinge kwa dhati unyanyasaji na ukatili kwa vitendo, na sio kwa njia za kuviziana na kukomoana.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment