Hitaji la walimu sio bati.
NA RUSTON MSANGI.
Kila chama cha wafanyakazi nchini kina jukumu la kusimamia, kulinda, kuboresha maslahi, na kuhakikisha haki za wanachama wake hazivunjwi, wala kukiukwa kwa namna yoyote ile.
Majukumu hayo ya chama chochote cha wafanyakazi hayaepukiki kwa kuwa wanachama huwa na utaratibu maalumu wa kuchangia kwa njia ya ada.
Michango hii kwa baadhi ya vyama huwa ya lazima hata kama haujajiunga wala kufahamu utaratibu wowote wa namna chama kinavyoendeshwa.
Mfano mzuri ni Chama cha Walimu Tanzania CWT, walimu wengi hawajajiunga kwa kuridhia, bali kwa lazima na kuanza kukatwa pesa 2% ya mshahara mara moja.
Mojawapo ya dhumuni muhimu la chama cha walimu Tanzania limeelezwa kwenye katiba ya CWT toleo la 2004, katika sehemu ya kwanza, 4 (s)Kuwekeza katika vitega uchumi vitakavyoboresha ustawi wa wanachama ingawa si Chama cha kibiashara.
Kwa msingi huu wa kikatiba tungetegemea vitega uchumi vya CWT kunufaisha walimu na si viongozi pekee.
Pamoja na makato hayo ya 2% ya mshahara ya lazima kwa CWT, walimu hawana faida kubwa yoyote moja kwa moja, zaidi ya kuambulia T-shirt na kofia kila mwaka katika sikukuu ya wafanyakazi mei mosi.
Na wengine hata hicho kidogo wanapata kwa kuchelewa au hawapati kabisa.
Nimeguswa kulizungumzia hili baada ya taarifa ya habari za saa iliyoripotiwa na kituo cha habari cha TBC, September 29, 2016 siku ya alhamisi.
Taarifa hiyo iliripoti kwamba, CWT wamegawa bati 20 kwa kila mwalimu mstaafu huko Nachingwea.
Kupewa bati sio ajabu lakini, haiendani na michango ambayo Mwalimu amechangia kwa kipindi chote alichofanya kazi.
Kwa mfano, Mwalimu anayepokea 700,000 kwa mwezi, akikatwa 2% ya CWT kila mwezi ni shilingi 14,000, kwa mwaka 14,000 × 12 = 168,000, kwa miaka ya utumishi 20 tu kwa mfano, ni sawa na 168,000 × 20 = 3,360,000 kwa mmoja tu.
Hapa ieleweke ni mfano tu, ila makato ni makubwa kwa kuwa mshahara hubadilika.
Hivyo kuna walimu hadi kustaafu kwao wanajikuta wamechangia C.W.T kiasi kikubwa cha pesa hadi kufikia millioni kumi (10,000,000) na zaidi kwa Mwalimu mmoja kwenye hiyo 2%.
Hizo bati 20 za CWT, kwa wastani wa 15,000 kwa bati × 20 = 300,000 (laki tatu)
Huu ni utani na fedheha kwa walimu kwakweli.
Walimu wengi wamekuwa wakiikosoa CWT kwamba haina msaada wowote kwa walimu katika kazi, kiuchumi, kitaaluma na hata kijamii, ikiwemo hili la bati 20.
Binafsi naungana na maelfu ya walimu nchini kuonesha kutoridhishwa na huu utaratibu wa bati 20 za CWT kutokana na sababu zifuatazo,-
Mosi, gharama ya bati ishirini haiendani hata kidogo na kiasi cha mchango, ambacho mwalimu anachangia chama tangu kuanza kukatwa 2% ya mshahara kwa mwezi hadi siku anapostaafu. Huu ni unyonyaji wa wazi kabisa.
Mbili, hakuna ushirikishwaji juu ya maamuzi muhimu kama haya yenye maslahi ya moja kwa moja kwa walimu. Jambo lolote jema linahitaji maamuzi sahihi baada ya kusikiliza maoni ya wanachama ambao ndiyo walengwa na wachangiaji wa chama.
Tatu, inajenga na kukomaza utamaduni wa walimu wengi kuamini kwamba, baada ya kustaafu ndiyo wakati sahihi wa kujenga nyumba.
Hii inatokana na kwamba utoaji wa bati ni ishara ya ujenzi, hivyo kwa baadhi ya walimu wanaweza kusubiria hizo bati ndipo waanze ujenzi, Huu ni utamaduni mbaya sana.
Nne, inasababisha matabaka baina ya viongozi wa chama cha walimu CWT na walimu wenyewe ambao ni wanachama.
Hii ni kutokana na kwamba inaaminika viongozi wa CWT wanakula tu hela za walimu, na kurudisha kiasi kidogo cha makato kupitia njia ya kutoa hizo bati 20.
Hata kama lengo la CWT ni zuri kiasi gani, lakini lina mapungufu makubwa sana kulinganisha na wajibu wa chama kwa wanachama wake pamoja na michango ya wanachama hao.
Ili kurekebisha mapungufu haya makubwa, CWT inapaswa kufanyia kazi mambo kadhaa,-
Moja, kukutana na walimu katika kila wilaya, ili kujadiliana kwa kina juu ya namna gani mwalimu anaweza kunufaika kiuchumi kutokana na michango anayochangia kipindi chote cha utumishi wake hadi kustaafu.
Hii itasaidia kujua nini hasa walengwa wanahitaji kufanyiwa.
Mbili, CWT Kuweka wazi vitega uchumi vyote vya walimu nchini, hii itaambatana na mapato pamoja na matumizi kulingana na idadi halisi ya wachangiaji.
Kwa kufahamu haya itapelekea kufamu tulichonacho na idadi ya walimu ndipo tujue matumizi yake.
Tatu, CWT kwa kushirikiana wadau wa ndani na nje ya nchi wabuni mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa chama, kiuongozi, kijamii, kiuchumi na kitaaluma.
Kupitia mbinu hii walimu watakuwa na uelewa mpana wa masuala mengi juu ya kazi yao na nchi kwa ujumla. Pia itawapatia walimu fursa za kupata elimu katika taasisi za nje na ndani, kwa kuwa maarifa ni bora kuliko bati.
Nne, Kuboresha mapema iwezekanavyo huu utaratibu wa utoaji wa bati kipindi ambapo bado unatumika hadi pale utakapobadilika, kwa kuongeza idadi ya bati kwa mwalimu na kuzitoa mapema kwa wahusika kabla hata ya muda wa kustaafu kufika.
Kwa kufanya hivi mwalimu ataweza kutengeneza maisha yake vizuri hata kabla ya kustaafu.
Nia njema yoyote isiyoshirikisha watu wala kuonesha uhalisia wa mambo, hutengeneza mazingira ya kushindwa au kutoridhisha wahusika.
Hivi ndivyo ilivyo kwa CWT kwenye huu utaratibu wa utoaji wa bati.
Ieleweke kwamba mwalimu anakumbana na changamoto nyingi sana, zinazohitaji kufanyiwa kazi kwa wakati.
Na kwa kila siku iitwayo leo CWT inahitajika kuonesha uwezo wa kufanya kazi na kutetea kwa dhati kabisa wanachama wake.
Ili kuweza kufanikiwa kwa walimu, ni wakati sasa wa kuungana pamoja na kupaza sauti.
CWT iambiwe kwamba hitaji kubwa la walimu sio bati 20 pekee, kuna mengi ni wakati muafaka sasa wa kushuka chini kwa wanachama.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment