SERIKALI INGEANZA KWANZA NA WALIMU
NA RUSTON MSANGI.
Taaluma ya ualimu ni mama na mhimili wa taaluma zote duniani. Hakuna Taaluma au fani isiyotokana na ualimu.
Ualimu ndio unaojenga daraja la uhusiano baina ya taaluma zote duniani.Kwamba watu waliopata taaluma au kusomea fani mbalimbali duniani walipikwa na kuivishwa kwenye chungu cha ualimu.
Ualimu ndio unaotengeneza ,wanasheria, wahandisi, wahasibu na hata mwandishi wa habari, wanasiasa.
Dhima ya ualimu ni kutoa au kufundisha maarifa, ujuzi na hekima. Ualimu ni mchakato wa kufundisha maarifa, ujuzi au hekima kutoka kwa mtu moja kwenda kwa mwingine. Mtoaji maarifa au hekima anaitwa mwalimu na mpokeaji ni mwanafunzi.
Wanafalsafa wa kale walifanya kazi ya ualimu kwa vitendo na walifanikiwa kuzalisha kizazi chenye hekima, maarifa na ujuzi tele. Waliacha urithi usiochakaa wala kuharibika vizazi na vizazi.
Mwanafalsafa Socrates aliyeishi Ugiriki ya kale kati mwaka 469-399 Kabla ya Kristo(B.K) aliishi kwa kutafakari ,kuhoji na kutafuta na kufundisha hekima na maarifa.
Socrates ni mwalimu aliyesaidia jamii yake kwa kutimiza jukumu la kupanda maarifa na hekima kwa wanafunzi wake.
mfano, Wanafalsafa wengine mashuhuri wa kale; Plato, Aristotle, Xenophon, Antisthenes na Aristoppus walijifunza kwa Socrates.
Ualimu wa Socrates baadaye uliwageuza wanafunzi hawa kuwa hazina ya fikra za kifalsafa na kisayansi hata leo.
Watawala hawakuthamini mchango wa Socrates,walimshitaki na kumpa adhabu ya kifo kwa makosa kuharibu fikra za vijana ili wapindue jamhuri-uhaini. Uhaini wa Socrates ulikuwa kuelimisha vijana.
Mwanafalsafa Socrates, alikufa lakini hakufa na maarifa na hekima.
Wala jamii yake haikubaki ukiwa,aliiachia jamii urithi wa hekima na maarifa kutoka na kutimiza wajibu wake akiwa hai.
Hata leo, jukumu kuu la ualimu ni kuacha urithi wa hekima na maarifa kwa kizazi kipya. Serikali inawajibika kuhakikisha inaweka mazingira ya hazina hii, inasalia kwenye jamii bila kutoweka.
Hili linawezekana tu kwa serikali kumua kuthamini kada ya ualimu kwa maneno na vitendo. Matendo hukidhi maridhawa kuliko maneno.
Kulingana na uzoefu na mitazamo tu iliyopo katika jamii, mwalimu amepewa nafasi na thamani hii:
Mosi, ni kioo cha jamii. Mwalimu ni mtu wa kuigwa na watu wote.Anapimwa na kupimika kwa ubora wa hulka,mwenekano na matendo yake.Anaaminika.Mwenendo wake,ni rahisi kuigika na wanafunzi na jamii.
kuiga, vivyo hivyo katika mavazi, Mwalimu akivaa vizuri na mwanafuzi wake na jamii kwa ujumla itaiga hivyo.
Vilevile kwa matendo mabaya ya Mwalimu kama ulevi, ugomvi, nk. mwanafunzi na jamii huiga kutoka kwa kioo chao ambacho ni Mwalimu.
Mtazamo huu husisitizwa sana na serikali, jamii na walimu wenyewe.
Pili, Ualimu ni taaluma ya kusomea.Ni ujuzi na usomi. Mtu anasomea ualimu,anahitimu na kutunukiwa cheti kama kigezo cha ubora wake .Kuna ngazi ya cheti, stashahada ,shahada,uzamili na uzamivu.
Fikra zinazotilia mkazo kuwa ualimu ni wito au zawadi kwa walioshindwa zimepitwa na wakati.
Baadhi ya walimu wanaona taaluma waliyonayo ni zawadi au wito.Hizi ni fikra mgando.Ni fikra za kuendeleza woga badala yakukazana kuda haki na stahiki za ualimu.
Tatu,ni kama kiwanda cha taaluma zote duniani.Ualimu ni taaluma mama inayozalisha taaluma zingine za sheria, uhasibu, udaktari na nyinginezo
Tatu, Mwalimu ni mzazi au mlezi . Mtoto anapotoka kwa wazazi wake nyumbani na kwenda shuleni.Akiwa shule,anakuwa mikononi mwa walezi wa shuleni ambao ni walimu katika tena kwa kipindi kirefu zaidi. Hivyo,walimu wanakuwa watu wa karibu wa mwanafunzi kimalezi pengine kuliko hata walezi wa nyumbani.
Nne, Ualimu ni utumishi wa Umma.Ni sawa kabisa na watumishi wa kada zingine kama ilivyo kwa wafanyakazi wote wa taasisi zilizo chini ya serikali, ambao kwa pamoja huitwa watumishi wa Umma.
Watumishi wote wa Umma ikiwemo walimu husimamiwa na kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa Umma, lengo kubwa ni kuutumikia umma wa watanzania na taifa kwa ujumla, hili husisitizwa sana serikali kwa walimu ili kumbana Mwalimu kuendana na masharti ya umma katika undendaji mzima wa kazi.
Utumishi wa Umma kwa walimu mara kadhaa hutumika kunyong'onyeza walimu katika maslahi Yao,
Kwa mfano, kuna walimu wanaidai serikali mishahara, pesa za likizo, na malimbikizo mbalimbali, Wakati wa kudai hutumika kauli maarufu kwamba mtumishi wa Umma ukiidai serikali pesa yako haipotei, lakini unakuta madeni yana zaidi ya miaka kadhaa kwa kisingizio kwamba ukiidai serikali hela haipotei, hii sio sawa.
Tano, Ualimu ni kazi. Mwalimu ni mfanyakazi kama zilivyo kazi nyingine zozote zinazofanywa na watu ndani ya Tanzania na ulimwenguni kote.
Baada ya kazi yoyote ile anayofanya mtu, mwisho wa siku hutegemea kupata kipato cha kumuwezesha kukidhi mahitaji yake katika maisha ya Kila siku.
Hivyo Mwalimu yeyote yule katika taifa letu la Tanzania ni mfanyakzi anayetegemea kupata kipato baada ya kutimiza majukumu yake.
Mtazamo huu unaonekana kuwa msingi mkuu wa Mwalimu kama ilivyo kazi yoyote ile, ambapo mwisho wa siku anategemea kuingiza kipato kwa ajili ya kuendesha maisha ya Kila siku.
Thamani ya mwalimu inajulikana.Lakini, kuna Changomoto lukuki zinazokabili kada ya ualimu.zinashusha heshima na thamani. Ni changamoto ambazo inabidi zifanyiwe kazi ili kukidhi mahitaji na thamani ya Mwalimu .Serikali na Wadau wa elimu kwa ujumla, wazingatie na kufanyia kazi yafuatayo:
Mosi, Kuwapatia walimu fursa za kupata ujuzi mbalimbali unaoendana na taaluma yao kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Hii itaongeza weledi wa taaluma ya ualimu na kuleta matokeo chanya kwa walimu wenyewe, wanafunzi wao, elimu na taifa kwa ujumla. Huku ndiko kuheshimu taaluma, kuiboresha na kuikuza. Na ndipo utaaluma wa Ualimu utadhihirika vyema.
Pili, Kuboresha maslahi ya walimu kwa kuangalia namna ya kuongeza mishahara au kuweka posho za aina tofautitofauti kwa taratibu zinazokubalika. Hii itamfanya Mwalimu kufanya kazi ambayo inamuingizia kipato kwa weledi na kujituma, Kwa kuwa ualimu ni kazi kwa walimu. Ili uifanye kazi vizuri ni muhimu hiyo kazi ikulipe.
Tatu, Kuandaa mazingira mazuri kwa makazi ya walimu ndani au nje ya shule, hii itasaidia kumfanya Mwalimu awe kioo cha jamii kwani ataishi kwenye mazingira bora ambayo yatachochea hata matendo mema na muonekano mzuri kwa jamii inayomzunguka.
Nne, Kuweka mazingira rafiki ndani ya eneo la kazi (shuleni) kwa maana ya zana za kufundishia, kujifunzia na mazingira rafiki ya kijamii ndani ya shule ambayo yatapekea Mwalimu kuwa mzazi na mlezi bora wa shule kwa wanafunzi wake.
Tano, Kutoa haki zote muhimu kwa Mwalimu kama mtumishi wa umma ( kwa wale serikali) , ikiwemo uhamisho wa vituo vya kazi, malipo ya likizo, posho za usumbufu, pamoja na kuondoa uonevu ndani na nje ya eneo la kazi, hivi vitamfanya Mwalimu kuwa mtumishi muaminifu wa Umma.
Kwa ujumla kila Mtanzania aliyewahi kupita kwenye mikono ya Mwalimu ni shahidi wa umuhimu wa Mwalimu kwa jamii na taifa, na hata ambaye hajapita kwa mwalimu anafahamu umuhimu huo kupitia ndugu, jamaa na marafiki.
Ili kumfanya Mwalimu awe na morali kwa kazi yake, na kufanya vizuri ni muhimu kuheshimu Ualimu wake kama kazi inayomuingizia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha.
Baada ya hapo itadhihirika wazi, Mwalimu ni mtumishi umma, ni mzazi, ni kioo cha jamii, ni mwanataaluma na
zaidi ni mfanyakazi.Ndio maana naona serikali ingeanza na walimu.
Mwandishi ni mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya Elimu.
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment