KUCHELEWA KWA AJIRA KUNAVYOUMIZA WALIMU
NA RUSTON MSANGI.
Kada ya ualimu ndiyo yenye watumishi wengi nchini kuliko kada yoyote ile.
Licha ya kada hii kuwa na watumishi wengi,takwimu zinaonesha bado kuna upungufu wa walimu nchini hasa walimu wa sayansi . Waziri mwenye dhamana ya elimu,Profesa Joyce Ndalichako akijibu swali katika kikao cha bunge kilichopita, alibainisha upungufu wa walimu wa Sayansi 22,460.
Miaka kadhaa iliyopita,watu wengi wamepata hamasa ya kusomea fani ya ualimu ili waajiriwe na serikali.Hakika walimu wamekuwa wakiajiriwa moja kwa moja katika shule katika shule za msingi na sekondari na vyuo .
Walimu wamekuwa wakiajiriwa kwa vipindi tofauti mara wa wanapohitimu.
Kwa mfano, walimu waliohitimu mwaka 2012 walipangiwa vituo vya kazi mwezi Februari 2013. Waliohitimu mwaka 2013 walipangiwa mwezi Machi 2014 na waliomaliza mwaka 2014 walipangiwa mwezi wa tano 2015.
Lakini mamia ya walimu waliohitimu mwaka 2015 ,hawajaajiriwa,wanaendelea kusota mitaani.Kuchelewa sana kwa ajira za ualimu kumekithiri katika utawala huu wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.
Walimu waliohitimu mwaka 2015,wako mtaani bila ajira kwa zaidi ya mwaka sasa. Hawaijui kesho yao. Mamia ya walimu wengine waliohitimu mwaka huu 2016,wanaungana na wenzao kusota mitaani bila ajira.
Inadaiwa kuwa jumla ya wahitimu wa 2015 na 2016 ni zaidi ya walimu elfu sitini nchini .Makadirio haya yanajumuisha wahitimu ngazi ya cheti, stashahada na shahada.Hawa wote walikuwa wanasubiri ajira zilizositishwa na serikali.
Serikali ilisitisha ajira zote za serikali ikiwemo walimu, kwa lengo la kuhakiki watumishi umma ili kubaini watumishi hewa, mishahara hewa na watumishi wasio na sifa.
Lengo la serikali ni zuri, na kila mwenye mapenzi mema na Tanzania ataunga mkono hili la kupambana watumishi na Mishahara hewa.
Pamoja na nia hiyo njema, tatizo linaonekana katika njia ya kufanikisha na kufikia lengo hilo.Kadhalika ,tatizo ni namna zoezi hili linavyozidi kuchelewa , linaleta madhara katika elimu yetu ya leo na huko baadae.Inaathiri uchumi wa wahitimu wenye sifa ya kuajiriwa.
Hivyo ajira za walimu kuzidi kuchelewa kutokana na uhakiki, kunaweza kuleta madhara yafuatayo:
Mosi, Kupoteza weledi wa walimu. Kama ilivyo kwa taaluma nyingine ulimwenguni, namna unavyokaa muda mrefu bila kufanyia kazi ndivyo ambavyo utaalamu hupotea siku hadi siku.
Kwa walimu hawa waliosomeshwa kwa pesa za watanzania masikini za mkopo na wazazi, utaalamu wao unazidi kupotea kiasi kwamba hata akija kupata hiyo ajira kuna vitu muhimu vitakosekana kwao.
Pili, Kuongeza zaidi tatizo la ajira nchini. Hii inasababishwa na hali ya mrundikano mkubwa wa vijana wasio na ajira kutokana na kwamba kundi kubwa kutoka vyuoni, lipo mtaani bila shughuli rasmi ya kufanya, kama ajira hakuna hata uchumi utatetereka.
Tatu, Kusabanisha familia za wahusika kuishi katika mazingira magumu maradufu. Familia nyingi hutumia rasilimali zao kuwekeza kwenye elimu ya vijana wao, ikiwemo kuuza mashamba na kufanya biashara, kwa matarajio kwamba wakihitimu na kupata ajira mambo yatakuwa mazuri, lakini hali ikiwa tofauti kama hivi familia za wahusika huishi kwa dhiki sana.
Nne, Inaweza kuwa sababu ya walimu wengi kwa kipindi hiki kuamua kuachana kabisa na ualimu kwa kwa maana ya kufundisha , Na kuamua kufanya shinguli nyingine binafsi au kwenye mashirika mbalimbali. Hii sio dalili nzuri.
Tano, Hali hii ikiendelea hivi itasababisha walimu wengi wenye weledi wa kutosha kuamua kufanya kazi na shule za binafsi, kuna walimu wengi wamesita kusaini mikataba shule binafsi, lakini hali ikiendelea hivi wengi watamwaga wino kusaini mikatana shule binafsi.Shule za serikali zitaendelea kuwa na uhaba wa walimu.
Sita, Husababisha kuwanyima haki wanafunzi ya kufundishwa kwa kuwa na walimu waliopo kwenye ajira hawatoshi kukidhi mahitaji.
Saba, Kusababisha migogoro isiyo ya lazima baina ya walimu wanaosubiri ajira dhidi ya serikali.
Kwa madhara haya yanayotokea na yanayoandaliwa kutokea zaidi, ni vizuri Serikali, wahitimu na CWT kufanyia kazi yafuatayo:
Mosi, Serikali ifanye juu chini iajiri walimu hawa katika mfumo mpya hata kama zoezi la uhakiki halijaisha, hii inawezekana kwa kuwa uhakiki unawahusu watumishi waliopo kazini, hivyo ajira mpya inaweza kuendelea kwa utaratibu wao mpya ambao hautaleta usumbufu wala kuathiri zoezi hilo.
Pili, Serikali kupitia wizara ya elimu kwa kushirikiana na taasisi za elimu nchini ihakikishe inaanda mfumo maalumu utakaowawezesha wahitimu wote ikiwemo walimu, kuwa na ujuzi ambao hautategemea sana ajira ili kuendesha maisha, Hii itapunguza mzigo kwa serikali juu ya kutoa ajira kwa wahitimu wengi.
Tatu, Chama cha walimu Tanzania( CWT), kiunde mfumo maalumu utakaosaidia kushughulika na walimu wanaosubiri ajira. Walimu hawa wamekuwa kama yatima na wanyonge hawana Msemaji wala mtetezi.Viongoz wa CWT wanadaiwa kuwa walaji tu wa posho zinatokana na makato kwenye mishahara ya walimu.
Nne, Walimu wanaosubiri ajira kutafuta fursa zingine. Hii itasaidia sana kuendesha maisha yetu ya kila siku bila kutegemea ajira ya serikali wala yeyote yule. Kwa kuwa likijitokeza tatizo kama hili mambo yote yanasimama.
Yakifanyika haya na mengine ambayo wahanga wamekuwa wakipaza sauti zao kuyasema kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ,itasaidia sana.
Sisi kama watanzania wenye nia njema na tunaopenda taifa liwe na nidhamu ya utumishi wa umma, tunaunga mkono uhakiki kufanyika .Tunasisitiza zoezi hili kuendelea kwa kufauata kanuni, sheria na taratibu za nchi. Lakini isiwe sababu ya walimu kuteseka kutokana na kuchelewa kwa ajira.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment