SERIKALI INAVYOZIKA NDOTO ZA KUPATA ELIMU BORA
Na Ruston Msangi.
Elimu ni muhimu na nguzo kwa watu na taifa lolote duniani.
Siri ya mataifa mengi yaliyoendelea kama Marekani, Uingereza, Urusi, Japan, China, Ufaransa, Ujerumani na mengineyo,Ni elimu bora.
Maendeleo ya mataifa hayo yanatokana na kuwekeza katika elimu bora ambayo baadae imewaletea wataalamu wengi, teknolojia na maendeleo kwa ujumla.
Utambulisho mojawapo wa nchi maskini,zinazoendelea kama vile Tanzania, ni elimu duni.
Wakati rekodi zinaonesha elimu ndio mhimili wa Maendeleo duniani, Tanzania na nchi nyingine maskini zinaelezwa kuzika elimu kaburini.
Mikakati, mipango na utekelezaji wake, vimekuwa vikisusua sana. Inarudisha nyuma ubora wa elimu.
Kwa mfano nchini Tanzania kumekuwa na mipango mingi ya kuboresha elimu, japo mipango mingi imeonekana kushindwa.
Leo tuangalie MABADILIKO MAKUBWA YA MFUMO WA MTIHANI WA KIDATO CHA PILI.
Hivi karibuni Wakuu wa shule mbalimbali nchini wamepokea waraka kutoka kwa Katibu tawala wa mkoa kupitia kwa wakurugenzi na maafisa elimu, waraka huo ukieleza juu ya mfumo mpya wenye mabadiliko makubwa ya mtihani wa kidato cha pili,
Kwa kifupi waraka huo unaeleza yafuatayo,-
Mosi, mtihani wa kidato cha pili utatambulika kama mtihani wa upimaji wa kitaifa wa Kati.
Mbili, Upimaji huo hautakuwa na MCHUJO.
Tatu, Mtihani utaandaliwa na baraza la mitihani NECTA kwa kushirikiana na taasisi ya elimu Tanzania.
Nne, Shule zitapokea nakala moja ya kila somo.
Tano, Kila shule itazalisha nakala Zake kwa idadi ya wanafunzi kwa kutumia Fedha za ruzuku.
Sita, Usimamizi na usahishaji utafanywa na walimu wa shule husika kulingana na Masomo Yao.
Kwa maelezo hayo hapo juu tunaona jinsi gani elimu yetu inavyochimbiwa kaburi kwa sasa,
Kwamba mtihani wa kidato cha pili umekuwa hauna maana tena kwa kuwa mwanafunzi hata akipata sifuri ni lazima aendelee, huku tukitegemea aje kuhitimu kidato cha nne.
Vilevile Mwalimu yuleyule ambaye amesahaulika kwa kufanya kazi katika mazingira magumu, kutolipwa malimbikizo yake, kutolipwa mishahara yake, kodi kubwa, makato lukuki, huku mshahara ukiwa palepale bila nyongeza yoyote, Ndo mwalimu huyohuyo anapewa jukumu la kusimamia na kusahihisha mitihani iliyotungwa na NECTA.
Pia tunaona jinsi gani tunaruhusu dhana ya kucheza mchezo na kujisimamia wenyewe, yaani ni sawa bondia anayepambana na mwenzake awe refa wa pambano, hapo unategemea matokeo gani?
Nashauri serikali kupitia wizara ya elimu ifanye yafuatayo, -
Mosi, Irudishe utaratibu wa mchujo kwa mtihani wa kidato cha pili kama zamani, Kwa kuwa mwanafunzi anapojua kuwa kuna mchujo kutokana na kiwango fulani cha alama za ufaulu, basi husaidia kwa mwanafunzi husika kuongeza juhudi katika Masomo na kufanya vizuri hadi kidato cha nne.
Mbili, Serikali ifikirie upya utaratibu wa Usimamizi na usahishaji wa mitahini hii, kuacha hili jukumu kwa walimu tu tena kwa taarifa bila ya walimu husika ambao ndiyo walengwa kushirikishwa katika hatua yoyote ile ya utaratibu huu mpya, ni hatari sana kwa maslahi ya elimu pale unapoamua jambo juu na kutoa tu taarifa kwa watekelezaji bila kusikia maoni Yao.
Tatu, Serikali itazame upya utaratibu wa nakala za mitihani kutolewa mashuleni, itakumbukwa kwamba kwa mitihani tu iliyokuwa inaletwa mashuleni ikiwa tayari kulikuwa na tatizo la udanganyifu, je hii ya kutolea nakala shuleni tunategemea miujiza gani ya kuzuia udanganyifu?
Watanzania wazalendo, wanaharakati na wapenda elimu wote kwa ujumla wao wanapenda kuona elimu bora ikitolewa Tanzania na sio bora elimu, Elimu bora ni pamoja na mifumo imara ya upimaji kwa wanafunzi wetu ili kuandaa kizazi imara cha leo, kesho na baadae.
Kwa mabadiliko haya ya mtihani wa kidato cha pili, nachelea kusema hili ni kaburi la elimu tunalolichimba wenyewe kwa Tanzania yetu ya vizazi vya Leo na baadae.
Ruston Msangi
0684 731516
Patience Pays!
Comments
Post a Comment