MAWAZIRI WA ELIMU WANAVYOKOROGA KWA ZAMU.
Anaandika Ruston Msangi.
Kila mwanadamu huzaliwa huru. Anapozaliwa haijulikani mara moja atakuja kuwa nani au mwenye taaluma/ fani gani. Lakini kutokana na malezi ya wazazi, mazingira, na jamii inayomzunguka mtoto huanza kutamani kuwa mtu flani hapo baadae.
Kutoka ngazi ya jamii, ndoto za mtoto huamia shuleni ambapo ndipo hasa eneo la muhimu katika kujenga misingi ya daktari, Mwalimu, mwanasheria, Mhasibu, Askari, mwanajeshi, mwanahabari nk. wa kizazi kijacho.
Uwezo wa mtoto kimasomo Kulingana na fani itakayo hujulikana akiwa shule. Kila mtoto anakuwa na uwezo kwenye eneo Lake Kulingana na kipaji chake.
Hivi vyote vinatokana na misingi ya Taifa, sera, mikakati, mipango ya muda mrefu na mazingira rafiki yenye mahitaji yote muhimu ya kujifunzia ndivyo ambavyo humuwezesha mwanafuzi kutimiza ndoto yake. Ndoto ya mwanafunzi ikitimia basi na ndoto ya Taifa itakuwa imetimia kwa kupata wataalamu viwandani na maeneo yote muhimu. Hivi ndivyo ambavyo wataalamu hupatikana ulimwenguni kote.Si kwa matamko ya kushinikiza au kulazimisha wanafunzi au wasimamizi wa Elimu.
Ni kwa bahati mbaya sana nchini Tanzania , ni sehemu pekee ambapo kwa vipindi tofauti serikali imekuwa ikifanya makosa ya kiufundi katika eneo nyeti la ELIMU, tena kupitia matamko.
Itakumbukwa mwaka 2005 wakati ndugu Mungai akiwa waziri mwenye dhamana katika elimu alifanya mabadiliko makubwa sana ya muda mfupi na yasiyo na maandalizi ya kutosha, ikiwemo yafuatayo:-
Mosi, Alifuta elimu ya ufundi katika shule za ufundi. kwa mfano wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2008 Shule ya ufundi Ifunda na shule nyingine za aina hii, ndio wanafunzi pekee ambao walinyimwa fursa ya kusoma ufundi kwa matakwa ya mtu mmoja, kisha kidato kilichofuata kikaendelea na utaratibu wa zamani. kwakweli Mungai alikoroga mambo ya elimu sana.
Pili, Mungai hakuridhika,aliendelea kukoroga. Alifuta somo la kilimo ambalo lilikuwa somo muhimu sana kwa watanzania.
Kulingana na takwimu wengi wanaishi vijijini wakijishughulisha na kilimo.Mungai aliona haina maana kwa watoto wa mkulima kujifunza kilimo.
Tatu,Mungai aliunganisha kemia na fizikia kuwa somo moja (Physics with Chemistry)
Haya ni baadhi aliyoyafanya Mungai. Wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2008 ni mashahidi wazuri wa hili.
Leo ni zamu ya Mh. Waziri elimu Prof. Joyce Ndalichako kukoroga kwenye elimu. Ndalichako mekuja na mpya kuhusu elimu kwa mtindo wa matamko kama ilivyo ada ya mawaziri wa serikali. Anasema kuanzia sasa masomo ya Sayansi ni lazima kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne. Tamko la waziri Ndalichako linafuta utaratibu wa awali wa uhuru wa mwanafunzi kuchagua masomo (sayansi, biashara au Sanaa) anapofika kidato cha tatu.
Msingi wa hoja ya Ndalichako ni "kupata wanasayansi wengi kuendana na Tanzania ya viwanda."
Nimesoma maoni ya watu mbalimbali mitandaoni na kusikia mtaani, wengi wao wako tofauti sana na hili tamko la waziri, wanasema ni vizuri Mtu kuchagua anachokiweza. Na hii ndo kanuni ya mafanikio kwamba watu wengi hufanya vizuri zaidi lile jambo analolipenda, vivyo hivyo kwenye masomo.
Tamko hili ni gumu kutekekezeka, na hata likitekekezeka zifuatazo ni changamoto Zake,
Mosi, Kuongeza mzigo kwa walimu wa sayansi, ambao ni wachache kwa kufundisha wanafunzi masomo ambayo hawako tayari kuyasoma na hawayawezi, kutokana ni misingi waliyoipitia.
Pili , Kutokea kwa matokeo mabaya zaidi.Hali ya wanafunzi ni mabaya sana. Kuna wanafunzi wa kidato cha tatu wanashindwa kusoma vizuri kiswahili lugha ya taifa, leo ukimlazimisha kusoma kemia, fizikia bila misingi tunategemea kupata matokeo gani?
Tatu, Tamko hili linaondoa uhuru wa kuchagua kile mwafunzi akipendacho bila kuweka misingi kuanzia chini.haiwezekani kufanikiwa bila kuanza na Msingi.
Nne, Tamko hili linaweza kuzalisha wataalamu feki wakaja kuligharimu taifa baadae, kwa kuwa itamlazimu mwanafunzi asome ili afanyie mtihani tu na sio kuwa Mtaalamu wa viwango vinavyostahili.
Tano, Tamko hili linaendeleza dhana ya kuwatenga walimu ambao ndio wahusika wakuu wa muhimu katika kufanikisha. walimu hawashirikishwi.
Kutokana na changamoto hizo za kauli ya waziri, nashauri serikali kupitia wizara ya elimu na wataalamu wa elimu nchini, ifanye yafuatayo;-
Mosi, Kuandaa sera ya elimu iliyofanyiwa iliyofanyiwa utafiti wa kutosha, ambapo itaeleza mambo yote muhimu na muelekeo wa taifa kielimu na tunavyotaka kwa kushirikisha wadau wote muhimu ikiwemo walimu, ambapo naamini tutakuwa na mipango ya miaka mingi ijayo mbele.
Pili, Kuandaa walimu wa sayansi wenye weledi wa kutosha, mazingira mazuri na yenye vifaa vya kutosha kujifunzia na kufundishia. Bila kusahau maslahi ya Mwalimu huyo na mazingira bora ya kuishi.
Tatu, Kuandaa mazingira mazuri katika hatua zote mwanafunzi anazopitia katika kukua kuanzia chini hadi juu , na kuweka maabara za kemia na fizikia zenye vifaa vyote muhimu wakati wote.
Nne, Kuwashirikisha walimu ambao ndo watekelezaji Wakuu wa mipango yote ihusuyo elimu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Maoni ya walimu yanaweza kuwa na mchango mkubwa sana katika elimu ya Tanzania.
Kwa kuzingatia haya machache, na mengine mengi ambayo wataalamu mbalimbali wamekuwa wakishauri katika elimu, Tanzania yetu inaweza kupata madaktari bingwa, mainjinia mahiri na wabobezi, wataalamu wa kilimo, wahasibu wazuri na wengineo bila hata kulazimisha, matokeo yake wanafunzi wenyewe watakuwa wa kwanza kuipenda fizikia na kemia na matunda yataonekana.
Binafsi kama Mtanzania mzalendo natamani taifa langu Liwe taifa la viwanda lenye wataalamu na wagunduzi na wavumbuzi wa kutosha, kama yalivyo malengo ya waziri na serikali kwa ujumla.
Kulingana na uhalisia duniani ya sasa, wataalamu wote wa sayansi na wasio wa sayansi hupatikana kwa mfumo maalumu ulioandalia vizuri kwa misingi imara toka chini mpaka juu, na sio kwa KULAZIMISHA.kwa namna mawaziri wanakoroga elimu kwa zamu. Sasa ni zamu ya Prof. Ndalichako kukoroga.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Ruston Msangi
Patience pays
0684 731516
rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment