Watumishi wa umma nchini Tanzania wanaongoza kutokuwa na furaha!
Na Ruston Msangi.
Hivi karibuni Tanzania imetajwa kuwa nchi ambayo watu wake hawana furaha duniani.
Tanzania imeshika nafasi ya 153 kati ya nchi 155. Hivyo watanzania hawana furaha kabisa katika maisha.
Licha ya ripoti hiyo kutotaja moja kwa moja kundi la watu wasio na furaha na viwango vyao nchini,
Inaelezwa kwamba watumishi wa Umma nchini Tanzania wanaweza kuwa watu wanaoongoza kwa kutokuwa na furaha zaidi.
Kwa muda mrefu sana watumishi wa umma wamekuwa hawana furaha kabisa, lakini katika kipindi cha October 2015, 2016 na 2017 kiwango vya kutokuwa na furaha kwa watumishi wa Umma kimeongezeka maradufu.
Na zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazoelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa watumishi wa Umma kutokuwa na furaha nchini Tanzania;-
1. Kusitishwa kwa ongezeko la la mshahara kwa mwaka (Salary Increment), kwa mujibu wa mkataba hufanyika kila July 1, na mara ya mwisho ilikuwa July 2015 wakati wa Kikwete.
2. Ongezeko la makato ya marejesho ya Bodi ya mikopo ya elimu ya juu. Kutoka 8% kwa mujibu wa mkataba hadi kufikia 15% kinyume na mkataba.
3. Michango ya mwenge kwa shinikizo. Baadhi ya maeneo wamechangia kuanzia 1000 hadi kufikia 10,000.
4. Madaraja ya mishahara ya walimu kusimamishwa kinyume na sheria, kanuni na taratibu.
5. Uhakiki usioisha uliogubikwa na unyanyasaji pamoja na usumbufu mkubwa sana.
6. Mazingira magumu na hatarishi yasiyo na vifaa wezeshi vya kazi.
7. Vyama vya wafanyakazi kuzidi kuwa dhaifu, bubu na daraja la unyonyaji wa haki za wanachama wao. Makato ya 2% kwa hivi vyama ni kwa ajili ya maslahi ya wachache tu.
8. Michango ya madawati kwa shinikizo, baadhi ya maeneo wamechangia kuanzia kiasi cha shilingi 5000.
9. Baadhi ya watumishi kutolipwa mishahara yao kwa wakati, hii ni kutokana na uzembe na makosa ya halmashauri na serikali kwa ujumla. Kuna baadhi wanadai zaidi ya mishahara ya miezi mitano (5).
11. Uonevu, unyanyasaji na udhalilishaji wa watumishi wa Umma kutoka kwa watendaji wa serikali. Mfano, wapo waliopigwa makofi, wapo waliotekwa, wengine kulazimishwa kupiga deki, na wengine kusimamishwa kazi au kufukuzwa kabisa kinyume na sheria za kazi nchini na mikataba ya kimataifa.
12. Michango ya maabara yenye shinikizo, baadhi ya maeneo watumishi wamechangia kufikia kiasi cha 20,000.
13. Watumishi wa umma kubebeshwa mzigo wote wa lawama pale panapokuwa na matokeo hasi kwenye kazi. Walimu kwa wanafunzi, madaktari kwa wagonjwa nk.
14. Kusimamishwa kwa uhamisho wa watumishi wa umma bila sababu za msingi kinyume na taratibu za kazi, hata pale mtumishi anapojigharamia. Ikumbukwe uhamisho ni haki msingi kwa mtumishi yoyote yule ilimradi taratibu zifuatwe.
15. Mafao ya watumishi wa umma wastaafu kucheleweshwa sana.
16. Kulimbikizwa kwa madeni mengi yasiyo ya mshahara, kama vile pesa ya likizo nk.
17. Kusimamia watumishi wa Umma kwa kutumia matamko pekee. Mfano hili la Waziri Angellah Kairuki kuhusu watumishi kutopanda madaraja ya mishahara na vyeo hadi pale watakapopata mafunzo maalumu.
Kwa hali hii, ni ngumu sana watumishi wa umma kuwa na furaha.
Pamoja na kwamba wananchi wengi hawana furaha ikiwemo wanasiasa, wafanyabiashara, wanamuziki, wakulima, wanafunzi nk, lakini watumishi wa Umma wanashika nafasi ya juu kabisa kwa kutokuwa na furaha nchini Tanzania.
Furaha hainunuliwi, bali hutengenezewa mazingira bora ya kuweza kuifanya iwepo miongoni mwa watu.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment