Pigo jingine kwa walimu na watumishi wa umma kwa ujumla




NA RUSTON MSANGI.


Katika watumishi wa umma, ualimu ni kada pekee yenye watumishi wengi kuliko kada yoyote ile nchini.

Ni kada mojawapo yenye changamoto nyingi pengine kuliko kada yoyote ile.

Tangu utawala wa awamu ya 5 uingie madarakani chini ya Rais Magufuli, matatizo ya watumishi wa Umma hususani walimu yamekuwa maradufu ya mwanzo.

Mtakumbuka kwamba tangu kuanza kwa zoezi la uhakiki usioisha, haki nyingi za walimu zimesimamishwa bila kufanyiwa kazi huku kukiwa na manyanyaso, ukandamizwaji na uonevu usio na mwisho kupitia kwa watendaji mbalimbali serikali kuu, halmshauri na baadhi ya maeneo kutoka kwa serikali za kata na vijiji.

Madaraja ya mishahara yamesimama, uhamisho umesimama, ongezeko la mshahara (salary increment ) kwa mujibu wa mkataba wa kazi umesimama, madeni hayalipwi, makato yameongezeka maradufu.

Mbali na yote hayo, walimu wameendelea kutimiza wajibu wao na hata kulaumiwa kwa matokeo mabovu ya shule za serikali.

Kabla ya hata kupanda kwa  makato ya 15% ya HESLB hayajapoa, Waziri wa Utumishi Angellah Kairuki amekuja na mpya.

Waziri wa Utumishi Angellah Kairuki amenukuliwa na vyombo vya habari ikiwemo ITV, siku ya Alhamis March 23 akisema kwamba, kuanzia sasa mtumishi wa umma yoyote yule HATAPANDISHWA CHEO wala DARAJA LA MSHAHARA bila kupitia mafunzo maalumu.

Hii inamaana kwamba bila hayo mafunzo aliyosema waziri Kairuki mtumishi wa umma atapata mshahara anaoupata hadi siku atakayostaafu au kuacha kazi. Hakika hili janga kwa walimu na watumishi wa umma wote kwa ujumla.


Tamko hili la waziri wa Utumishi, mbali na kuzua taharuki baina ya watumishi wa umma pia limeacha maswali mengi yasiyo na majibu yenye tafsiri mbalimbali,-

Mosi, Inaonesha serikali hii ya sasa ni kawaida sasa kuendesha mambo kwa matamko pekee.

Hii ilianza kwa Profesa Ndalichako na tamko la kuhusu wanafunzi kusoma masomo yote kwa lazima, sasa ni kwa Kairuki, na huko nyuma miaka ya 2005 ilitokea kwa hayati Joseph Mungai akiwa waziri wa elimu.

Mbili, Serikali inayotakiwa kusimamia sheria na haki za wananchi wake, ndiyo ya kwanza kuvunja mikataba ambayo iko kisheria tena kupitia matamko pekee.


Tatu,  Tamko hili la waziri Kairuki linawavunja moyo walimu na watumishi kwa ujumla katika kutimiza majukumu yao ya kutoa maarifa kwa wanafunzi wetu. Hii itaangamiza taifa sio mbegu nzuri inayopandwa.

Nne, Hii itawafanya watumishi wengi wa serikali ikiwemo walimu kuacha kazi serikalini na kutafuta shughuli nyingine za kufanya, Hii pia itawafanye Wale wote waliopo nje ya mfumo wa serikali kutotamani kuingia serikalini kwakuwa hakuna afadhali yoyote.

Tano, Haieleweki hayo mafunzo maalumu ili mtumishi apande daraja au cheo ni mafunzo ya aina gani? yanatolewa na nani? yanatolewa wapi? Kwa vigezo gani? Kwa muda gani? Kwa cheo gani? Daraja gani?

Sita, Ni muendelezo ya kutoshirikisha wadau muhimu au wahusika katika jambo linalowahusu,  Katika hili wadau Wakuu ni watumishi wote wa umma ambao wanaonganishwa na vyama vyao na umoja wao.

Ni ajabu sana kufanya maamuzi juu ya jambo linalomhusu mtu nakumuumiza bila kumshirikisha na mwisho wa siku utegemee ufanisi kutoka kwake. Haikubaliki.

Haya yote kwa ujumla wake yanasababisha usumbufu mkubwa sana usioelezeka kwa watumishi wa umma, na inahitajika juhudi za dhati kabisa kuweza kukabiliana na hili na mengine yanayofanana na haya kwa baadhi ya njia zifuatazo;-

Mosi, Umoja wa vyama vya wafanyakazi(TUCTA) kwa kushirikiana na vyama vyote vya wafanyakazi kama CWT,MAT, TUGHE nk, kupitia viongozi wake wanapaswa kujitafakari kwa hili na mengine mengi ya ajabu sana yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa.

Kama wameshindwa kutetea wafanyakazi ni bora wakaachia nafasi walizonazo zishikwe na wengine, na sio kutumia michango ya wanachama bure bila kufanya kazi inayoridhisha.

Mbili, Kambi rasmi ya upinzani bungeni kupitia kwa waziri kivuli wa Elimu Mama Suzan Lyimo kwa kushirikiana na waziri kivuli wa utumishi, wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya haya yanaendelea kwa walimu na watumishi  wa umma kwa ujumla.

Inaaminika kwamba serikali kivuli ni serikali mbadala kwa wananchi, hivyo inapaswa kubeba hoja za watumishi na wananchi kwa ujumla.

Tatu, Serikali ya awamu ya tano inapaswa kutambua kwamba watumishi wa umma wameajiriwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, na sio matamko ya kwenye warsha na semina.

Hivyo kwa mabadiliko yoyote yale inapaswa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kurejea mikataba ya kazi ya watumishi wa umma.

Nne, Watumishi wa umma wanapaswa kujitambua, kuwa majasiri na kuelewa haki zao ikiwa ni pamoja kufahamu sheria zinazowalinda. Watumishi wa umma wengi hawajitmbui, hawajui haki zao, na ni wapiga vigelegele hata kwa mambo yanayowaumiza. Watumishi wa umma wamekuwa wakitumiwa na serikali kama dodoki na baadae kutupwa, Hii inajidhihirisha katika kupiga kura uchaguzi mkuu, Serikali za mitaa na chaguzi ndogo, katika kuandikisha wapiga kura, katika sensa ya watu na makazi nk.

Shughuli hizi zote kwa kiasi kikubwa hufanywa na watumishi wa umma lakini hali zao zinazidi kuwa mbaya kila kukicha.

Tano, Taasisi zote za kiraia zitambue kuwa zina wajibu mkubwa katika kupigania maslahi na haki za watumishi wa umma, ili kujenga jamii yenye maarifa, maendeleo na maadili.Ni muhimu kuiga mfano wa kituo cha sheria na haki za binadamu nchini LHRC.


Hili jukumu la kupigania haki na maslahi ya watumishi wa umma, ni letu sote likianzia kwa watumishi wenyewe kuonesha kuonesha kuchukizwa na mabaya yanayoendelea kutokea nchini.

Hakuna malaika atashuka kuja kuwasaidia watumishi wa umma, bali umoja wao, kujitambua kwao, kuchukizwa kwao na uonevu na kuchukua hatua kunaweza kuleta faraja na mabadiliko makubwa sana kiuchumi, kijamii na kitaaluma.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

  1. Uchambuzi mzuri bwana Msangi, bila shaka walimu na watumishi wengine wa umma wamekuelewa.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Tunashukuru kwa maoni yako ndugu msomaji wa blog yetu tutazidi kuelimishana zaidi na zaidi

      Delete

Post a Comment

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI