Vyama vya wafanyakazi vijifunze kwa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu LHRC!


NA RUSTON MSANGI.


Ni jukumu la kila chama cha wafanyakazi nchini  kusimamia, kulinda, kuboresha maslahi, na kuhakikisha haki za wanachama wake hazivunjwi, wala kukiukwa kwa namna yoyote ile.

Majukumu hayo ya chama chochote cha wafanyakazi hayaepukiki kwa kuwa wanachama huwa na utaratibu maalumu wa kuchangia kwa njia ya ada, ili kufanikisha shughuli za chama husika.

Mfano wa vyama vya wafanyakazi nchini ni kama Chama cha walimu Tanzania (CWT), Muungano wa wafanyakazi katika sekta ya viwanda na biashara (TUICO), Umoja wa wafanyakazi wa afya wa serikali (TUGHE), Muungano wa wafanyakazi wa Serikali za mitaa (TALGWU).

Mwezi huu umekuwa ni pigo kwa wafanyakazi nchini, hasa wale walionufaika na mikopo ya elimu juu wakati wa masomo yao.

Maumivu haya makubwa ni kuhusu mabadiliko ya sheria yaliyopelekea kuongezeka kwa makato ya marejesho ya mikopo, kutoka 8% ya awali hadi 15% iliyoanza kukatwa mwezi huu wa pili.

Suala hili kiukweli limewaacha wafanyakazi wengi nchini na maumivu makali yasiyovulimka hata kidogo, sio walimu, sio madaktari, sio mawakili, wala wafanyakazi wengine hakuna aliyefurahia uvunjwaji huu wa mkataba. Hawa wote tangu awali zilivyoanza tetesi walipiga kelele kupinga na kuonesha hisia zao za kukataa, lakini vyama vya wafanyakazi vyote vilionekana kukaa kimya kabisa bila kuonesha juhudi zozote za kupinga na kuhoji uhalali wake.

Tukumbuke kwamba hivi vyama vya wafanyakazi vipo kwa ajili ya maslahi ya wafanyakazi, kuwatetea kwa namna yoyote katika kila jambo ambalo linakwenda kinyume na haki za msingi za mfanyakazi katika eneo la kazi na nje ya eneo la kazi.

Mbali na kelele nyingi za wafanyakazi maofisini, mitaani, mitandaoni na hata majumbani,  wengi wameonesha kukata tamaa na kazi wanazozifanya.

Jambo La kufariji ni kwamba mapema sana baada ya makato haya mapya kuanza kutekelezwa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kimeonesha nia ya dhati kulipigania suala hili katika mkondo wa sheria kupitia mahakama.  Haya yamebainishwa na mmoja wa wanasheria kutoka LHRC. Huku wakitoa wito kwa mawakili wote walioguswa na suala hili la 15% wafike ofisini kwao LHRC Kijitonyama siku ya jumanne ili kuandaa taratibu za kufungua kesi, kutokana na ukiukwaji wa mkataba ya HESLB na wanufaika wa mkopo ambao kwa sasa ni wafanyakazi katika taasisi mbalimbali.

Wakati LHRC wakiwa katika utaratibu wa kufungua kesi, mmoja wa viongozi wa chama cha wafanyakazi kutoka chama cha walimu CWT Mwal. Ezekiah T. Oluoch ambaye ni Naibu Katibu mkuu, amekuja na tamko la maelekezo kwa makatibu wa CWT mikoa.

Maelekezo haya kutoka kwa Naibu Katibu mkuu wa CWT yanaonekana wazi kabisa Kwamba yana nia ya kurudisha mapambano nyuma katika kudai haki za walimu na wafanyakazi kwa ujumla. Ujumbe huo unaeleza baadhi mambo yafuatayo,-

Mosi, anasema kwamba suala la makato ya 15%  lipo kisheria.
Mbili, anasema anahitaji makatibu wa mikoa watume majina ya walimu na sahihi zao ili iwe kama kielelezo kwa ambao hawajaridhika.
Tatu,  anasema kwamba watakwenda kuishawishi serikali kama itakubali.

Pamoja na maelezo mengine mengi, Mimi binafsi naungana na walimu pamoja na wafanyakazi wote nchini ambao hawajapendezwa na hili suala la ukiukwaji wa mkataba, kwa kusema Naibu Katibu mkuu wa Chama cha walimu maelezo yake yanarudisha nyuma mapambano ya walimu na wafanyakazi wengine kwa ujumla.

Aelewe kwamba chama cha walimu kama vilivyo vyama vingine kiko kwa ajili ya kutetea maslahi ya walimu, na sio tu hadi walimu watoe malalamiko na kusaini majina, inatakiwa kutetea sehemu yoyote ile ambapo kuna uonevu na manyanyaso, ilimradi yathibitike.

Aelewe kwamba Bodi ya mikopo ya elimu ya juu HESLB, Iko chini ya Serikali na kwa walichokifanya hawajafanya peke yao bali kuna baraka za waziri husika, na hadi rais wa nchi ambaye ndiye mtu wa mwisho kuifanya sheria iitwe sheria kwa kutia sahihi katika muswada wa sheria ambao hupita bungeni kwa kuletwa na waziri husika.

Aelewe kwamba walimu huku chini na wafanyakazi kwa ujumla hawana furaha na kazi kabisa, yaani hata Wale waliokuwa imani kidogo imepotea, yaani kwa kifupi wafanyakazi hawana imani na serikali wala vyama vyao, na sio tu suala la 15%, kuna mengine mengi kama ongezeko la mshahara (salary increment) tangu 2015, madai ya misharaha kibao, malimbikizo mengine mengi, na mazingira magumu. Mapambano haya yawe mwanzo wa kudai na haki nyingine zote za msingi.

Aelewe kwamba katika mihimili mitatu ya utawala yaani serikali na Bunge (hivi havina msaada kwetu), tumebakiwa na mahakama peke yake pamoja na nguvu ya wafanyakazi wenyewe kuanzia kwenye vituo vya kazi. Hivyo Naibu katibu mkuu nitamuona shujaa kama tashawishi CWT iungane na vyama vingine vya wafanyakzi ili kupeleka mawakili ili kuungana na LHRC ili kudhibiti huu unyanyasaji na ukandamizaji kwa walimu na wafanyakazi wote nchini.

Ushauri wangu kwa vyama vya wafanyakazi vyote nchini na taasisi mbalimbali,-

Waungane ili kuunganisha nguvu kama ambavyo LHRC  ilivyoonesha njia katika utaratibu wao wa kuandaa kwenda mahakamani juu ya jambo hili la 15%.

Vyama vya wafanyakazi vitambue kwamba ile 2%  ya makato ya mshahara kutoka kwa wanachama kwa wao kwa ajili ya shughuli za vyama, sio kwa ajili ya kukaa ofisini, kula viyoyozi, na kujinufaisha wao na familia zao, Bali ni kwa ajili ya kutetea haki za wafanyakazi nchini kwa namna yoyote ile.

Naomba mawakili wote nchini mnaopenda haki kama ambavyo taaluma yenu inavyojidhihirisha, jitokezeni kusaidia wafanyakazi kupitia LHRC na taasisi nyingine zilizo tayari kwa mapambano.

Mwisho, lakini sio mwisho kwa ufahamu napenda kuwashukuru marafiki zangu mawakili wafuatao walioonesha nia ya kuungana na LHRC katika mapambano haya ya 15%, Wakili msomi Dickson Matata, Wakili msomi Chance Luoga,  Wakili Msomi Emmanuel Clarance. Mungu awabariki sana katika haya mapambano.

Naomba ieleweke wazi kwamba mapambano haya sio ya mtu mmoja, ila ni ya kila mtu, Kila mfanyakazi na wananchi wapenda haki kwa ujumla. Lakini pale serikali inapowatupa wafanyakazi,  basi vyama vya wafanyakazi viwe jirani kuwatetea wanachama wao.

Ufanisi wa kazi unakwenda sambamba na malipo mazuri pamoja na mazingira yanayovutia katika kazi kwa ujumla.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI