Elimu bure imekuza tatizo la chakula mashuleni



NA RUSTON MSANGI.

Ubongo wa mwanadamu ili ufanye kazi sawa sawa na kwa ufanisi,unahitaji lishe.Ni muhimu kula vizuri na kushiba.


Mwanafunzi darasani,anatumia  akili nyingi.Ili aweze kufikiri vizuri na kuelewa anachofundishwa ni lazima apate chakula kwa muda sahihi na kushiba.Ni muhimu.


Kabla ya waraka wa elimu bure wa serikali ya awamu na tano  mwaka 2016, wanafunzi katika shule nyingi za serikali walikuwa wanakula shuleni kutokana na michango ya  wao.


Baada ya waraka wa elimu bure kuanza kutekelezwa rasmi mwaka jana 2016,kumetokea  mabadiliko makubwa ya hali ulaji wa chakula mashuleni.Wanafunzi hawali kama mwanzo.


Waraka wa elimu bure umeainisha  majukumu ya serikali,  wizara ya elimu, TAMISEMI, Halmashauri, Wakuu wa shule na walimu Aidha umeanisha majukumu ya mzazi katika kutekeleza elimu bure.


Mojawapo ya majukumu ya wazazi ni kuhakikisha mtoto/mwanafunzi anapata vifaa vyote muhimu vya shule kama madaftari na sare za shule .

jukumu jingine kubwa na muhimu kwa wazazi ni chakula kwa wanafunzi. Hapa ndipo tatizo lilipoanzia.

Waraka wa elimu bure ulitoa uhuru kwa wazazi na walezi kuamua namna wanayoona inafaa ya kuwapatia wanafunzi/watoto chakula.


Uhuru huo kwa mzazi kupitia elimu bure kama vile umeleta matatizo badala ya kuyamaliza.Umeleta matatizo  kwa kusababisha yafuatayo kutokea;

Mosi, kuna wazazi wameamua watoto wao wasile kabisa shuleni huku ratiba za shule zikiendelea kama kawaida. Hivi ninavyoandika kuna shule nchini hapa ambazo awali wanafunzi walikuwa wanakula, lakini hivi sasa wakati wa elimu bure hawali chakula shule, hii ina madhara
makubwa sana katika uanafunzi wa watoto wao.


Pili, imesababisha mgawanyiko na matabaka katika baadhi ya shule. Yaani kuna wazazi wanataka watoto wao wale shule na wamechangia kutokana na makubaliano yao, na kuna wazazi hawataki watoto wale shuleni na hawajachangia. Kwa mfano, kama shule ina wanafunzi 300, unakuta wanafunzi wasiozidi 50 ndo wanakula. Hii ni hatari nyingine katika elimu.

Tatu, baadhi ya wazazi wanachangia pesa nyingi ambayo haitofautiani na ilivyokuwa kabla ya elimu bure, kwa mfano kuna wazazi wanachangia shilingi elfu 70 kwa ajili ya chakula pekee.Hii ina maana kwamba ukijumlisha na mahitaji mengine ni pesa nyingi sana kwa mwaka kwa mwanafunzi mmoja hasa wakati huu wa elimu bure.

Nne, imesababisha baadhi ya wanafunzi kuwa watoro sugu wengine kukataa shule kabisa.Sababu kubwa ni ugumu wa elimu bure kwa kuwa wazazi wengi baada ya kusikia elimu bure wamewasusa watoto wao na kujivua majukumu kabisa.

Haya yote na mengine mengi yanatokana na elimu bure chini ya utawala huu wa awamu ya 5.

Zinahitajika juhudi za dhati ili kuweza kushughulikia tatizo la chakula mashuleni ili kuilinda elimu ya watoto wetu na taifa kwa ujumla.

Naishauri wizara ya elimu, serikali kwa ujumla, wazazi na wadau wote wenye  dhamana wafanyie kazi yafuatayo,-

Mosi, kwa zile shule ambazo wanafunzi hawali kabisa, baada ya muda wa masomo uliopangwa basi waruhusiwe kurudi nyumbani me kuwa hawaathiri ratiba yoyote ile. Kwa shule nyingi za serikali mwisho wa vipindi ni saa nane na nusu au saa tisa kasoro, hivyo ni halali kutoka baada ya muda wa vipindi.


Pili, wazazi wakae upya chini kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hisika ili kujadiliana na kuona namna bora ya kuwasaidia hawa watoto.


Tatu,Serikali ni muhimu sana kila inapofanya mabadiliko makubwa yoyote katika mfumo wa elimu, ishirikishe wadau muhimu kama walimu na wazazi kwa njia tofauti. Hii athari ya chakula inafika hadi kwenye matokeo, hivyo ni ajabu ukija kumlaumu Mwalimu wakati unajifanyia mabadiliko wenyewe.

Kwa kufanya haya na ushauri wa wadau wengine muhimu katika elimu na maendeleo ya taifa letu kwa ujumla, itasaidia kupunguza au kuondoa kabisa hili tatizo la chakula shuleni.

Jukumu hili la kupata sauti lisiachwe kwa watu wachache, kwa kuwa madhara yake yanaligusa taifa zima.

Elimu bure imekuwa furaha kwa wengi lakini matatizo yake ni makubwa sana katika ufanisi.

Suala la chakula shuleni linaweza kuonekana ni dogo, na utofauti wake ukachukuliwa kawaida, lakini utofauti huu tusipoufanyia kazi tuutegemee hadi kwenye matokeo ya mwisho ya wanafunzi wetu.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI