Walimu tujitafakari katika utoaji wa adhabu, hatma yetu iko mikononi mwetu
NA RUSTON MSANGI.
Kuna msemo unasema kinga ni bora kuliko tiba, yaani ni bora uwe na tahadhari ya kukabiliana au kujihami na jambo lolote na si kusubiria hadi tatizo lijitokeze.
Siku za hivi karibuni kumejitokeza matukio makubwa mawili nchini yanayohusisha walimu na wanafunzi.
Tukio la kwanza ni la Agosti 27, 2018 ambapo mwalimu Respicius Patrick na mwenzake Herieth Gerald wa shule ya msingi Kibeta mkoani Kagera, wanatuhumiwa kwa kumuadhibu hadi kumsababishia kifo mwanafunzi wao Sperius Eradius wa darasa la tano. Chanzo cha tukio hili inasemekana ni mwanafunzi huyo kuhusishwa na wizi wa pochi ya mwalimu. Na hadi sasa walimu hawa wamesomewa mashtaka ya kuua kwa kukusudia katika kesi ya mauaji namba 18 ya mwaka 2018.
Tukio lingine ni lile la mwalimu wa sekondari ya Kalangalala mkoani Geita aliyejulikana kwa jina la Rauson Lechapia anatuhumiwa kumshambulia kwa ngumi mwanafunzi wa kidato cha sita Jonathan Mkono hadi kupelekea kulazwa hospitali kutokana na maumivu makali. Kosa la mwanafunzi likisemekana ni kwenda bwenini wakati wa vipindi, na mwalimu huyu alikuwa mikononi mwa polisi.
Matukio haya mawili yameibua hisia za watu wengi nchini hususani hili la kifo cha mwanafunzi huko Kagera.
Hisia za wananchi wengi zimeleta mawazo na maoni mbalimbali ikiwemo yafuatayo,-
Kuna kundi linasema huyu mwalimu aliyesababisha kifo cha mwanafunzi anyongwe hadi kufa.
Wengine wanasema huyu mwalimu afungwe kifungo cha maisha jela.
Pia wapo wanaosema hao walimu nao wachapwe hadi kufa ili iwe fundisho.
Wanaotoa maoni hayo ni wazazi wenye wanafunzi, na wengine ni wananchi kwa ujumla.
Wote kwa pamoja tunakubaliana kwamba walimu ni watu wapekee ambao hukaa na wanafunzi/watoto kwa muda mrefu kuliko wazazi wao, hivyo pengine walimu wanawafahamu vizuri watoto kuliko wazazi wao. Wapo watoto wanavuta bangi, wapo walevi, wapo wezi, wapo wenye kila tabia mbaya. Lakini pia wapo watoto ambao wana tabia za kupendeza.
Kazi kubwa ya mwalimu ni kumpatia mwanafunzi maarifa ikiwa ni pamoja na kumlea katika maadili mema yanayostahili.
Hivyo walimu mbali na jukumu lao la msingi kubwa la kufundisha, pia huvaa majukumu ya mzazi katika malezi ya watoto hawa. Jambo hili hufanya huinufaisha jamii husika na si mwalimu.
Pamoja na mchango huo wa mwalimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, pale linapotokea tatizo kwa mwalimu hakuna mtetezi wa mwalimu.
Mwalimu anakuwa adui kwa taasisi zote, mwalimu anakuwa adui wa wazazi wote na adui wa jamii kwa ujumla. Mwalimu anakuwa mtuhumiwa wa mauaji.
Binafsi siungi mkono wanafunzi kushambuliwa kama wanyama au kwa adhabu zilizopitiliza viwango, pia nimesikitishwa sana kifo cha mwanafunzi.
Najua walimu wanapitia changamoto nyingi sana, na nyingine ziko juu ya uwezo wao wa kibinadamu. Ndani ya changamoto hizi zote mwalimu hukabiliana nazo kwa lengo kubwa moja tu, kufanikisha ndoto za wanafunzi kwa maslahi yao na vizazi vyao.
Lakini ni wakati sasa wa walimu kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Walimu nawaasa sana mtafakari na kufanyia kazi mambo ya msingi yafuatayo,-
Mosi, Jiepushe kabisa na suala la kutoa adhabu pale unapokuwa na hasira. Waswahili wanasema hasira hasara. Hata kama mwanafunzi amefanya kosa kubwa kiasi gani, pale mauti yatakapomkuta basi ni umeua wewe. Hakuna atakayekuelewa.
Mbili, Ni muhimu kuzijua kanuni za adhabu ya viboko kwa undani kwa kuiona, kuisoma na kuielewa. Kwamaana wengi wanasikia tu adhabu ni viboko kadhaa lakini hawajui ni kanuni gani. Kufahamu ili itasiadia sana katika utoaji wa adhabu au kuacha kabisa kama kanuni zinabana au zina masharti magumu.
Tatu, kila mwalimu katika taasisi aliyopo ni muhimu kuwa na mjadala juu ya suala la adhabu kwa wanafunzi. Je kwa mazingira halisi ya shule na mambo yanayojitokeza, suala la adhabu ya viboko lina umuhimu wa kuendelea kuwepo au lisiwepo?
Leo hii limetokea kwa walimu wa Kagera na Geita. Kesho na kesho kutwa linaweza kutokea kwa mwalimu yeyote yule. Mwalimu husika ana familia na inamtegemea. Kwa kesi ya mauaji ni wazi kwamba ndoto za familia husika zimeishia njiani kwa pande zote.
Walimu tujilinde wenyewe sisi pamoja na familia zetu kwa kufanya yale yanayostahili kwa kipimo stahiki. Pia tuzilinde ndoto za wanafunzi wengine kwa pamoja. Mtoto aliyeshindikana tafuta namna nyingine.
Kumbuka makosa ya mwalimu ni rahisi kuonekana kuliko ya daktari, polisi, mwanajeshi nk. Hii ni kwasababu ualimu ni kada pekee yenye watumishi wengi nchini.
Wazazi na jamii kwa ujumla msichukulie walimu ni kama watu wakatili na wauaji wasiofaa, hapana. Najua wapo walimu wenye mapungufu wahukumiwe kwa mapungufu yao na si kada nzima.
La msingi kinachohitajika ni mshikamano wa kweli wenye nia ya dhati baina ya walimu, wanafunzi, wazazi, serikali na jamii kwa ujumla. Hii itapunguza au kumaliza kabisa matatizo sugu mashuleni.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment