Uchambuzi wa kifasihi katika wimbo wa Roma na Stamina uitwao Parapanda!


NA RUSTON MSANGI.



Fasihi ni sanaa itumiayo lugha kufikisha ujumbe kwa hadhira/jamii iliyokusudiwa. Nyimbo ni aina ya sanaa katika fasihi ambayo hutumia lugha teule, sauti na kiimbo maalum.
Nyimbo huburudisha, kuelimisha, kusifia, kuliwaza nk.

Hivi karibuni msanii Roma kwa mara nyingine, na kwasasa akiwa na mwenzake Stamina wamekonga nyoyo za mashabiki wa muziki na fasihi kwa ujumla kutokana na wimbo wao maarufu wa Parapanda. Wafuatiliaji wa mashairi ya Roma kwa muda mrefu, watakubaliana nami kwamba Roma amepiga hatua kubwa sana hasa katika matumizi ya fasihi.

Katika wimbo huo wasanii Roma na Stamina wamekuja na aina tofauti kabisa. Wasanii hawa wamevaa uhusika wa watu wawili maarufu kwenye historia ya taifa letu, ambao kwa sasa hatuko nao hapa duniani. Yaani Baba wa taifa Mwal. Julius Kambarage Nyerere na Kingunge Ngombare Mwiru.
Roma akiwa ni Nyerere na Stamina akivaa uhusika wa mzee Kingunge.

Wasanii hawa wamefanya hivi kuvuta taswira juu ya mtazamo wa watu maarufu na wenye historia katika taifa letu, wanaitazamaje Tanzania ya leo huku wakilinganisha na matarajio yao.

Katika wimbo wa Parapanda kuna ujumbe na mafunzo mengi sana kwa jamii, wengi wameeleza katika namna tofautitofauti, na binafsi nimegundua mambo yafuatayo,-


1. Uwepo wa uhalifu na utekaji kwa wanasiasa, wanahabari pamoja na wasanii. Haya yanajidihirisha katika wimbo wa Parapanda pale mhusika Mwalimu Nyerere  (Roma) anapomuuliza mzee Kingunge (Stamina) kwamba ni nani wanaohusika katika uhalifu na utekaji, mfano, Lissu, Roma na waandishi wa habari. Majibu yanakuwa ni watu wasiojulikana. Hivyo hii inaonyesha uhalifu upo lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu hao.

2. Kukwamishwa kwa katiba mpya ya wananchi. Katika wimbo huu hili linajidhihirisha pale Mwalimu Nyerere anapomuuliza mze Kingunge kuhusu mchakato wa katiba ulipofikia, lakini majibu ya Kingunge yanaonesha kwamba mchakato uliharibiwa na baadhi ya wahusika walifanyiwa fujo. Mfano, Jaji Warioba alipofanyiwa fujo katika kongamano la katiba. Na hii ina uhalisia kwakuwa hadi sasa hakuna katiba mpya nchini.

3. Udhaifu wa baraza la sanaa nchini. Wasanii hawa pia wameonyesha kutotendewa haki na chombo hicho cha kusimamia sanaa nchini. Hii inajidhihirisha pale Mwalimu Nyerere anapomuuliza mzee Kingunge kuwa ni nani anayesimamia sanaa, na majibu yanakuwa ni kuwa kuna baraza lakini wasanii wanaishi uani. Hivyo hakuna ushirikiano wa dhati kati ya wasanii na baraza la sanaa.

4. Kutambua nguvu vyama vya upinzani. Hili pia limezungumziwa na wasanii hawa Roma na Stamina, pale ambapo Mwalimu Nyerere anauliza mtawala ni chama gani, akajibiwa bado ni CCM. Hapo inaonesha kwamba Mwalimu Nyerere alitegemea chama cha upinzani ndo kinaweza kikawa mtawala kwa miaka hii.

5. Wananchi kukosa haki ya kuona wawakilishi wao kutokana na bunge kutokuwa live. Hii inajidhihirisha pale mwalimu Nyerere anapomuuliza Mzee Kingunge kwamba anasikia bunge halionyeshwi, je wananchi wanaona vipi wawakilishi wao. Katika uhalisia kuonyeshwa kwa bunge ilikuwa ni njia nzuri ya wananchi kuona wawakilishi wao, hivyo wanakosa haki yao ya msingi.

6. Nguvu ya mitandao ya kijamii katika harakati mbalimbali nchini. Katika wimbo huu wasanii Roma na Stamina wameonyesha kuwa mitandao ya kijamii kama facebook, instagram, twitter, Whatsap nk. ina nguvu kubwa katika jamii. Hii imejidhihirisha pale ambapo mwalimu Nyerere anauliza vipi mitandao ya kijamii haisaidii, na Kingunge anajibu anasema kuna dada anaitwa Mange Kimambi. Hii ina uhalisia kwakuwa Mange amekuwa na nguvu kubwa kupitia mitandao kijamii.

7. Imani za kidini. Wasanii Roma na Stamina pia wameionyesha jamii kwamba kuna imani za kidini na watu mbalimbali wanatambua uwepo wa Mungu. Hii imejitokeza pale Nyerere anaposema huko alipo baada ya kifo ana mji wake wa kudumu na unaitwa Nyerere.
Vilevile alipomuuliza Kingunge shida nini hadi amekufa,  akajibu ni mipango ya Mungu. Hivyo Roma akamwambia Kingunge karibu kwenye makazi ya milele. Hii ni hali halisi katika jamii yetu.

8. Upendo wa dhati na kujali. Wasanii hawa pia wameongelea juu ya upendo na kujali. Hili linajitokeza pale ambapo Mwalimu Nyerere anauliza kuhusu mke wake anapata huduma vizuri kutoka kwa watawala, Kingunge anajibu anasema Mama Maria Nyerere anatunzwa vizuri. Vilevile upendo umejikeza pale Nyerere anapomwambia Kingunge kuwa amemuona shemeji wameongozana katika safari ya kifo yaani mke wa Kingunge, hivyo wanapendana sana. Hata katika maisha ya ndoa katika jamii inaakinika kifo ndicho kinachowatenganisha watu.

9. Kutambua uwezo wa mpinzani wako. Hili limejidhihirisha pale ambapo Kingunge (Stamina ) anaomuiliza mwalimu Nyerere alikuwa timu gani. Mwalimu Nyerere anajibu kwamba alikuwa anaipenda Yanga lakini Simba ni kisanga, akimaanisha  timu ya Simba iko vizuri sana. Hii inaifundisha jamii kwamba hata kama uko upande tofauti ni muhimu kutambua uwezo wa upande mwingine.

10. Kuwa na matarajio tofauti na hali ilivyo. Wasanii Roma na Stamina wamefanikiwa kuonyesha hili pale ambapo Mwalimu Nyerere anapouliza Rais ni nani, anajibiwa na Kingunge kwamba Rais ni John. Mwalimu Nyerere anauliza tena John Malecela? Anaambiwa John Magufuli, kisha anaonyesha hali ya mshangao ikiashiria hakutegemea kama itakuwa hivyo lakini ndivyo ilivyo.


Haya ni baadhi ya mambo yaliyojitokeza na kujadiliwa na wasanii Roma na Stamina kwa kuwatumia Hayati baba wa taifa Mwalimu Nyerere na Mzee Kingunge. Kupita mambo haya jamii inapata mafunzo mbalimbali katika maisha halisi.

Kwa ujumla Roma na Stamina almaarufu Rostam wameitendea haki fasihi kwa kutumia nyimbo hii na nyingine nyingi. Wanapaswa kupongezwa kwa kazi nzuri. Ile fasihi ya darasani ndo hii imewekwa katika uhalisia na wasanii hawa. Pongezi ziwafikie popote pale walipo.



rustonmsangi@yahoo.com
0684 731516

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI