Wakuu wa shule wapata nafasi ya kukomoa walimu.
NA RUSTON MSANGI.
Ni wiki kadhaa sasa walimu wengi nchini wamekuwa katika msongo wa mawazo, hii ni kutokana na agizo la serikali linalotaka walimu wa sekondari wa stashahada na shahada wanaosemekana ni wa ziada kwa masomo ya sanaa wapelekwe shule za msingi.
Mapema sana nilionesha kutokukubaliana na agizo hili kwa kuwa ni kimyume na mkataba, humuathiri mwalimu kisaikolojia, humshusha mwalimu cheo, hunyima wahusika ajira, nk.
Katika utekelezaji wa agizo hili ambalo limepingwa na walimu wengi wenye akili, kumezuka matatizo makubwa zaidi.
Baadhi ya wakuu wa shule za sekondari nchini wamepata nafasi ya kuonyesha chuki za wazi kabisa kwa walimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa namna moja au nyingine wakuu wa shule wamehusika moja kwa moja katika zoezi la kuhamisha walimu kutoka sekondari kwenda shule za msingi.
Na ushiriki wa wakuu wa shule haujawa wa heri wala haki, bali imekuwa ni nafasi kwao kuadhibu, kukomoa na kuondoa watu ambao wanahisi ni kero kwao.
Nayasema haya kwa uhakika kabisa kwakuwa katika baadhi ya shule wakuu wa shule wamependekeza kuondolewa kwa baadhi ya watu kutokana na sababu zifuatazo,-
Mosi, walimu wengi waliopewa barua za kwenda msingi ni wale waliotofautiana kimawazo na mtazamo dhidi ya wakuu wa shule. Hapa kuna wakuu wanachukulia kutofautiana kimawazo ni uadui.
Mbili, Walimu wengi walioonesha nia ya kuhama vituo vya kazi na kufuata familia zao wamefanyiwa fitna na wakuu waende shule za msingi. Na baadhi ya wakuu wametamka wazi kabisa.
Tatu, Walimu walioonesha nia za kwenda kusoma ili kuongeza elimu zao, baadhi yao wamepewa barua za kwenda msingi.
Nne, Baadhi ya walimu wameonekana ni tishio kwa vyeo vya wakuu wao wa shule kutokana labda na uwezo wao na namna yao ya kuwaza, kutafakari na kupambanua mambo.
Tano, wale wote ambao hawamnyenyekei mkuu wa shule na kumlamba viatu wamepitiwa na kadhia hii. Wanawaza kwamba kunyenyekea ndo heshima na nidhamu. Wanaonyenyekea hata kama wana astashahada watabaki sekondari.
Sita, zoezi hili limegubikwa na ukabila wa hali ya juu. Kuna baadhi ya watu wanaozungumza lugha moja na wakuu wao wanabaki kuwa salama. Lakini wengine hawana haki.
Haya yote ni dhahiri kabisa yamefanywa ili kukomoa na kukatisha ndoto za walimu kwa kujua au kutokujua. Na inadhihiridha zoezi hili na batili na kinyume cha haki.
Wakuu wa shule za sekondari walioyafanya haya kwa matakwa yao ili kufurahisha nafsi zao na za wale walioshirikiana nao, nipende kuwaambia tu kwamba wasijisahau na kujiona malaika.
Wakumbuke nao ni walimu na ni binadamu ambao hawana tofauti na walimu hao waliowatendea huu unyama.
Wakae wakijua hakuna aliye salama, mambo yanabadilika na lolote linaweza kutokea wakati wowote ule.
Inaeleweka wazi wakuu wa shule wanaofanya haya kwa kushirikiana na wenzao, wanaona wameshamaliza na kukamilisha maisha yao, wana nyumba, wana posho ya laki mbili na nusu, wengi wanaishi na familia zao, watoto wao wako shule.
Hivi vyote vinawapa baadhi ya wakuu wa shule upofu wa kutokuona wala kujali na kuthamini maisha ya wengine ambao ndo kwanza hawana muda mrefu kazini na bado wanahitaji kujipanga kwa mambo mengi ya kiuchumi na kijamii.
Hivyo agizo hili la serikali kiujumla limezua matatizo makubwa sana ambapo athari zake haziwezi kuonekana kwa haraka.
Kwa mtindo huu kila kukicha linakuja jambo jipya kwa walimu, inaifanya kada ya ualimu kuzidi kuwa hatarishi zaidi kwa walimu. Hii ni kutokana na kwamba tangu siku ya kwanza ya ajira ni mateso yanayoongezeka kila siku bila kutulia wala kupata mtetezi wa kweli.
Wakati yote haya yanaendelea kuwabughudhi walimu, chama cha walimu nchini CWT, ni kama vile kiko likizo. Si kwamba hawajui wajibu wao lakini ni dhahiri wanafaidika na yanayoendelea kwa walimu.
Mtetezi wa kweli na thabiti juu haya ni walimu wenyewe, pale watakapoona uvumilivu umefika mwisho.
Vilevile pale walimu wengine wengi watakapojitambua na kujua thamani ya utu wao na taaluma zao.
Kuna methali inasema hakuna marefu yasiyo na ncha. Hivyo kutokujitambua kwa baadhi ya walimu kuna mwisho wake pia.
Siku hiyo ikifika kila mbaya wa mwalimu, kuanzia na baadhi ya wakuu wa shule watapata aibu. Mwisho wa ubaya ni aibu.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment