Uhakiki unatumika kuminya haki za watumishi wa umma!

NA RUSTON MSANGI.

Mapema mwezi  Aprili na Mei 2017, serikali ilitangaza hadharani idadi ya watumishi wa umma wenye vyeti feki  (vyeti vya kughushi) na watumishi wanaotumia cheti kimoja kwa watumishi wawili na zaidi.

Taarifa ya serikali ilisema watumishi takribani 9,000 wamegundulika kutumia vyeti vya kughushi, wakati watumishi takribani 1,000 wanatumia cheti kimoja watu wawili au zaidi.

Sambamba na hilo la watumishi wenye mapungufu, Serikali ilitoa majina kwa kila mkoa ya watumishi waliohakikiwa na kuonekana wana vyeti halali kuanzia sekondari hadi vyuoni.

Zoezi hili lilitumia muda na pesa nyingi za watumishi, pamoja na pesa za umma.

Kipindi chote cha uhakiki, haki za watumishi wa umma hususani maslahi ya mshahara, madeni, nyongeza ya mwaka (salary increment), upandishaji wa madaraja nk. vyote vilisimama hadi sasa mwaka wa pili umetimia.

Kwa mantiki hiyo hawa watumishi kwa ujumla nchini ambao wameonekana kuwa na vyeti halali baada ya uhakiki wa muda mrefu kufanyika na kukamilika, walipaswa kuanza kupata haki zao za msingi ambazo zilisimama kwa muda wa miaka miwili tangu uongozi wa awamu ya tano uingie madarakani chini ya rais John Magufuli.

Hivi karibuni baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri, ambapo waziri George Mkuchika amechukua nafasi ya Angelah Kairuki katika wizara ya UTUMISHI, hali imekuwa tofauti na matarajio ya watumishi wa umma juu ya maslahi bora yameyeyuka ghafla.

Hii ni baada ya Waziri mpya wa sasa kuja na uhakiki mwingine tena. Waziri Mkuchika alinukuliwa na vyombo vya habari akidai serikali imebaini watumishi wa umma elfu arobaini walidanganya umri, hivyo alisisitiza kwamba huo ni uhakiki mwingine na hakutakuwa na nyongeza ya mshahara hadi hapo uhakiki huo utakapomalizika.

Waziri Mkuchika alidai kwamba wamebaini watumishi elfu arobaini wamedanganya  umri. Kwa maneno mengine Waziri anauaminisha umma wa watanzania kwamba watumishi hao waliodanganya umri wanajulikana kwa majina yao na vituo vyao vya kazi.

Kwa upande wa waziri na serikali wanaweza kujisifu wanafanya kazi, lakini kwa upande  mwingine wa watetezi wa watumishi wa umma na watumishi wenyewe, jambo hili linaonekana ni njia nyingine ya ucheleweshaji wa haki na maslahi ya watumishi wa umma kwa makusudi kabisa kwa sabubu zifuatazo;

Mosi, Waziri Mkuchika anadai wamebaini watumishi elfu arobaini wamedanganya umri. Sasa kama kweli hawa watu wanajulikana ni kwanini waziri anatangaza kusimamisha tena haki na maslahi ya watumishi wa umma kwa kisingizio cha uhakiki.

Kama watu wanajulikana na kama ni kweli wamefanya makosa na kuna nia ya dhati ya serikali basi kilichotakiwa ni kushughulika na hao watu, bila kusimamisha au kuathiri haki na maslahi ya wengine.

Mbili, tangu mwaka 2015 mwishoni hadi sasa kumekuwa na mfululizo wa uhakiki usioisha na mara nyingine ukijirudia bila utaratibu maalumu na kusababisha tu usumbufu usio wa kawaida, na mara nyingine hata kuathiri ufanisi wa kazi kwa watumishi wa umma.

Tatu, Kumekuwa na mfululizo wa nyaraka zenye masharti na vikwazo vingi vya kubana au kuwapa vikwazo vya utendaji wa kazi watumishi wa umma bila kujali wala kuzungumzia haki na maslahi yao.

Nne, Baada ya serikali kutangaza uhakiki umeisha, iliambatana na kauli mbalimbali za viongozi wakidai wametenga fedha kwa ajili ya madeni ya mishahara na malimbikizo yote ya watumishi wa umma na mapema wataanza kulipwa. Lakini ni miezi imepita sasa kimya kimetanda hakuna jipya.

Haya yote yanazidi kushusha morali ya watumishi wa umma kila kukicha.

Hii ni kwasababu hakuna mfanyakazi anayeweza kuwa na bidii ya kazi wakati haki na maslahi yake yanaminywa.

Wakati maslahi ya watumishi yapo chini, wanaendelea kuchangia taifa kupitia makato ya kodi. Income tax (PAYE) na michango mingine lukuki ambayo yanafanya mshahara usitamanike.

Haya yote ni ujumbe kwa vyama vya wafanyakazi, ambavyo vinaweka mifukoni asilimia mbili (2%) ya mishahara ya wanachama wao bila kuifanyia kazi inayotakiwa. Wanaishia kujinufaisha wenyewe.

Hizi 2% ni jasho la wafanyakazi. Kuila bila kuifanyia kazi hasa ya utetezi wa haki na maslahi ya wafanyakazi ni unyonyaji mkubwa sana.

Kuendelea kuwa bubu kwa vyama vya wafanyakazi ni kuruhusu uhakiki usioisha kuendelea kutumika kuchelewesha haki na maslahi ya watumishi wa umma. Hii haikubaliki.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI