Ulipaji wa madeni ya watumishi wa umma, ufanyike kwa kasi kama uhakiki wa vyeti ulivyofanyika!
NA RUSTON MSANGI.
Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mwezi octoba 2015, takribani miaka 2 hadi sasa kumekuwa na misamiati maarufu kama UHAKIKI na UTUMBUAJI majipu.
Hivi vyote vikienda sambamba kwa lengo la kuhakikisha watumishi wa umma waliopo makazini wana vigezo vyote ikiwemo kigezo kikuu cha kitaaluma.
Lengo lake ni zuri japo ya mapungufu na usumbufu mkubwa uliojitoekeza kwa watumishi wa umma hasa wale waliokidhi vigezo vyote. Uhakiki umepelekea wengi kufukuzwa, kuacha kazi lakini na wengine kubaki kwenye nafasi zao.
Uhakiki kwa watumishi wa umma ikiwemo walimu ambao ndio watumishi pekee wengi nchini kuliko kada yoyote ile, umesababisha usumbufu mkubwa sana hasa wa kiuchumi na haki nyingi za msingi za kisheria kusimamishwa, wakati watumishi wakiendelea kutimiza wajibu wao wa kazi katika majukumu ya kila siku. Mfano walimu wastaafu na waliostahili kupanda madaraja pekee wanaidai serikali zaidi ya bilioni 300.
Mbali na usumbufu huu kwa watumishi wa umma na kusimama kwa haki nyingi ikiwemo kutokupanda madaraja, kutolipwa malimbikizo ya mishahara, kusimama kwa uhamisho, malipo ya likizo nk, Serikali kupitia viongozi wake kwa nyakati tofauti imekuwa ikisema kwamba mambo yote yatakwenda Sawa na haki zote zitatimizwa baada ya zoezi la uhakiki kukamilika.
Hivi karibuni serikali imetangaza hadharani idadi ya watumishi wenye vyeti feki (vyeti vya kughushi) na watumishi wanaotumia cheti kimoja kwa watumishi wawili na zaidi.
Hadi sasa watumishi takribani 9,000 wamegundulika kutumia vyeti vya kughushi, wakati watumishi takribani 1,000 wanatumia cheti kimoja watu wawili au zaidi.
Sambamba na hilo la watumishi wenye mapungufu, Serikali imetoa majina kwa kila mkoa ya watumishi waliohakikiwa na kuonekana wana vyeti halali kuanzia sekondari hadi vyuoni.
Kwa mantiki hiyo hawa watumishi kwa ujumla nchini ambao wameonekana kuwa na vyeti halali baada ya uhakiki wa muda mrefu kufanyika na kukamilika, wanapaswa sasa kupata haki zao za msingi ambazo zilisimama kwa takribani miaka miwili sasa.
Ni wakati sasa wa madeni ya watumishi wa umma kulipwa kwa kasi kama uhakiki wa vyeti ulivyofanyika.
Ni wazi kwamba madai haya ya wafanyakazi yameshawasilishwa, kuhakikiwa na kufuatiliwa kwa muda mrefu sana na mara kwa mara hasa katika Halmashauri husika ambazo ndizo kiunganishi kati ya serikali kuu na watumishi husika.
Ni wakati pia wa Mh. Rais Magufuli kufanyia kazi maneno yake ili yaonekane katika matendo kwa wafanyakazi nchini.
Kwa nyakati tofauti Rais Magufuli amenukuliwa akisema ili afanye mambo mazuri kwa wafanyakazi ni lazima wale wasio na sifa hasa za kitaaluma wabainike na kuondoka kwanza.
Hata katika mei mosi ya mwaka huu 2015 kule Moshi mkoani Kilimanjaro alisema baada ya huu uhakiki kukamilika ni wakati wa kutimiza yale aliyoyaahidi muda mrefu wa wafanyakazi sambamba na madai mengine yaliyosimamishwa.
Waingereza wana msemo usemao, '' actions speak louder than words'' kwa maneno haya ni matumaini kwamba watumishi wa umma wajiandae kwenda ATM tu.
Mbali na hapo uhakiki huu uliochukua muda mrefu na kusimamisha haki za watumishi wa umma utakuwa hauna maana na morali ya wafanyakazi itazidi kushuka kwa kasi sana.
Kauli mbiu ya chama cha walimu nchini CWT inasema Haki na Wajibu. Naamini kauli mbiu hii inafanya kazi kwa watumishi wote nchini kwamba wajibu unakwenda sambamba na haki, pale kimoja kinapopuuzwa mambo hayawezi kusonga mbele hata kidogo. Huu ni wakati wa watumishi wa umma kupata haki zao.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com
Comments
Post a Comment