Lugha za kimakabila zina athari kwenye elimu yetu!



NA RUSTON MSANGI.

 Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa fulani au kundi fulani kwa ajili ya kuwasiliana.


Lugha inayotumiwa rasmi na watu wa taifa fulani huitwa lugha ya taifa na ile inayotumiwa kundi fulani la watu hasa makabila ni lugha za kimakabila.Kuna lugha huitwa lugha mama.Kila mtu mwenye uwezo wa kuzungumza ana lugha  mama.

Lugha mama ni ile lugha ambayo mtoto anapozaliwa hukutana nayo na ndiyo lugha ya kwanza kujifunza kuzuizungumza kuitumia kuwasiliana.Pia,inajulikana kama lugha ya kwanza.


Kwa mfano, mtoto akizaliwa leo  katika jamii ya watu wanaotumia kiswahili,akajifunza na  kuweza kukitumia kwa mawasiliano,basi hiyo ndiyo lugha yake ya mama.

Au mtoto aliyezaliwa leo na kujifunza kuwasiliana kwa lugha ya  kisukuma,  akaweza,hiyo ndiyo lugha mama kwake.Watanzania wengi lugha zao mama ni zile za kimakabila.


Katika mfumo wetu wa elimu nchini Tanzania tunazitambua lugha mbili.Kiswahili kinatumika kufundishia elimu ya awali na msingi isipokuwa somo na kiingereza kinatumika kufundishia sekondari hadi chuo isipokuwa somo la kiswahili na lugha nyingine za kimataifa.



Japokuwa lugha za makabila zinatutambulisha na  tamaduni zetu na kuonesha asili na hata kuwa marejeo katika tafiti kwa  baadhi ya masomo, lakini haitambuliki kama lugha ya kufundishia au kujifunzia.

Hata hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi inayosifika kwa kuwa na makabila mengi, inakadiriwa kuna makabila zaidi ya 100.


Ikiwa   Lugha mama au lugha ya kwanza ni  lugha za makabila huleta shida sana kwa jamii. Hii huenda mbali zaidi hadi kuathiri mfumo wa elimu wa wanafunzi wetu katika baadhi ya maeneo ambayo lugha za makabila zimekithiri na kuwa kama nguzo kuu ya mawasiliano.Nataka ijulikane kuwa lugha mama ina nguvu miongoni kwa watoto wa shule kwa sababu ni lugha yao ya kwanza.


Hii inajidhihirisha Katika baadhi ya maeneo nchini, kama vile usukumani(kanda ya ziwa) upareni(same) umasaini(kaskazini) uchagani,unyihani(Mbozi) ufipani(sumbawanga).



Lugha za makabila zinapokuwa ndio lugha mama au lugha ya kwanza huweza kusababisha yafuatayo,-



Mosi,Baadhi ya walimu hasa wenyeji wa maeneo husika kufundisha na kuwasialiana na wanafunzi kwa lugha za makabila. Hii ina athari kubwa kwa wanafunzi kuwa hakuna mtihani inajibiwa kwa lugha ya kabila lolote.



Pili, Inawafanya wanafunzi kutumia lugha za makabila kwa kiasi kikubwa maeneo ya shule hadi darasani na hata nyumbani, hii huwajengea mazoea mabaya katika uelewa wa kiswahili au kiingereza.
JPM ambaye ni mwalimu kitaaluma amekuwa akitumia Sana lugha za makabila kwenye majukwaa ya siasa.Huenda alijifunza kwenye  shuleni ambazo walimu au wanafunzu wanatumia lugha za kimakabila



Tatu, Katika baadhi ya maeneo watoto wengi na wanafunzi kwa ujumla inawafanya kutofahamu lugha ya kiswahili kabisa,  wakati ndiyo lugha ya masomo ya awali na msingi.



Nne, Inachangia kuwepo kwa matokeo mabaya ya mitihani kwa shule za msingi ambapo kiswahili ndicho hupaswa kutumika isipokuwa kwa somo la kiingereza,  pia hata sekondari huchangia kuwepo kwa matokeo mabaya kwa kuwa kutokana na kuzoea lugha ya makabila, wanafunzi wanapata tabu kukifahamu kiswahili na kiingereza.

Kwa mapungufu haya na athari hizi ni muhimu sana kwa mamlaka husika kuchukua hatua  kutafuta suluhu ya kudumu.Nashauri yafuatayo:



Mosi, Serikali na Halmashauri husika zinapaswa kuboresha miundombinu hasa ya barabara, hii itasaidia mwingiliano wa jamii zilizopo kando sana na miji. Kwa mwingiliano huu, kutokana na shughuli mbalimbali itasababisha matumizi ya lugha tofautitofauti ikiwemo kiswahili, hivyo jamii husika haitazungumza lugha za makabila pekee. Hii itasaidia wanafunzi na elimu yetu kwa ujumla.



Pili, Serikali na taasisi zisizo za kiserikali zinapaswa kutoa elimu kwa jamii husika juu ya umuhimu wa kutumia lugha mchanganyiko ikiwemo kiswahili, mbali na Lugha za makabila. Hii itasaidia watoto, jamii na wanafunzi katika elimu na mawasiliano mengine.



Tatu, Wizara ya elimu kwa kushirikiana na walimu wote nchini, kubuni mbinu mbalimbali zitakazowashawishi wanafunzi wanaotumia lugha za makabila kuweza kubadilika na kutumia lugha nyingine kama kiswahili na kiingereza



Tukiweza kufanyia kazi haya machache na mengine mengi, itasaidia watoto, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuweza kuzimudu lugha nyingine kimawasiliano na zaidi kitaaluma.


Ieleweke kwamba lugha za makabila sio mbaya na hatuwezi kukwepa asili yetu, lakini ni muhimu sana kuitengenezea mazingira ya lugha hizi kutoleta athari kwenye  elimu yetu inayotumia kiswahili na kiingereza kama lugha za kufundishia.

Hivyo, ni muhimu kuona fahari na kuzienzi lugha zetu za makabila kama utambulisho wetu  bila kuathiri elimu ya vizazi vya leo na kesho.



Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya Elimu.
Namba yake ya simu:0684 731516
Barua pepe:rustonmsangi@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

MAANA HALISI YA USHOGA WA KISIASA, OGOPA KAMA UKOMA, EPUKA KUTUMIKA

KILIMO CHA NYANYA

SABABU ZA WASOMI KUWA MASIKINI